UNAKUMBUKA Mwanaspoti mapema wiki hii tuliwajulisha juu ya mipango waliyonayo Azam FC ya kumleta Kocha wa zamani wa Raja Casablanca na klau nyingine kadhaa, Rachid Taoussi? Basi hivi unavyosoma, jamaa keshatua nchini leo mchana tayari kuanza kazi na klabu hiyo.
Azam ilikuwa ikimalizana na kocha huyo ikielezwa atapewa mkataba wa miaka miwili kuchukua nafasi ya Msenegal, Youssouf Dabo aliyetemeshwa kibarua kutokana na matokeo mabaya iliyopata timu hiyo katika mechi za mwanzoni mwa msimu huu za ndani na zile za kimataifa.
Azam iliyokuwa ikishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ilitolewa raundi ya kwanza na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 2-1, huku ikishindwa kufurukuta katika fainali ya Ngao ya Jamii kwa kufumuliwa 4-1 na Yanga iliyorejesha taji hilo kutoka kwa Simba, lakini ikalazimishwa suluhu na JKT Tanzania katika Ligi Kuu.
Kitendo hicho kiliwafanya mabosi wa Azam kumtema Dabo na wasaidizi wake, kisha kuwatangaza Kassim Liogope kukaimu nafasi hiyo huku ikiendelea kumsaka kocha mkuu na Mwanaspoti ikafichua klabu hiyo ilikuwa ikijiandaa kumshusha Taoussi ambaye alitua saa 8 mchana akitokea Morocco.
Licha ya mabosi wa Azam kufanya siri juu ya ujio wa kocha huyo, lakini Mwanaspoti lilipenyezewa juu ya ujio huo na kuwahi Uwanja wa Ndege na kubahatika kumwona mmoja wa vigogo wa klabu hiyo aliyempokea Taoussi kabla ya kuondoka naye uwanjani hapo kwa kilichoelezwa alikuwa akienda Mzizima kwa ajili ya kumaliza mazungumzo na kusainishwa mkataba na walikuwa wakipanga kumtangaza rasmi jana usiku.
Mwanaspoti lilipata nafasi ya kuzungumza na kocha huyo, baada ya kutua uwanjani hapo, alisema Azam ni timu iliyo na mipango mikubwa, hivyo anajua ana kazi ya kuzipigania ndoto zao.
“Natambua Azam ina wachezaji wazuri, najua wanawaza kufanya vitu vikubwa kwa maendeleo ya soka Tanzania. Kwa ujumla Ligi Kuu ya Tanzania ni ngumu ina ushindani mkubwa, tumekuja kupambania malengo ya klabu.
Kocha huyo aliongozana na benchi lake la ufundi akiwamo kocha msaidizi, kocha wa viungo na kocha wa makipa waliotua juzi Ijumaa wakipokelewa na Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’ na Afisa habari Zaka Zakazi. Taoussi raia wa Morocco aliyezaliwa Februari 6, 1959, enzi za uchezaji alikuwa kiungo mahiri na rekodi zinaonyesha amezifundisha timu mbalimbali zikiwamo za taifa za vijana za Morocco U17, 20 na 23 mbali na klabu kadhaa zikiwamo Raja Casablanca, RS Berkane, FAR Rabat na nyingine.
Mbali na kuhudumu katika timu hizo za kwao Morocco ila Taoussi amewahi kuifundisha ES Setif ya Algeria aliyoitumikia kwa kipindi cha miezi mitano tu kuanzia Julai 1, 2018 hadi Novemba 23, 2018 kisha kutimkia Klabu ya Olympique Khouribga.
Mafanikio makubwa kama kocha ni kunyakua mataji matano tofauti akiwa timu tofauti ikiwamo Maghreb de Fes cha Morocco alichoipa ubingwa wa Trone 2011 sambamba na Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huo huo huku 2012 akichukua taji la CAF Super Cup, pia alitwaa ubingwa wa Afrika U20 akiwa na Morocco 1996-97 na enzi za uchezaji alitwaa ubingwa wa Morocco akiwa na FAR RAbat mwaka 1988-89.
Ni mzoefu wa soka la Afrika na akishiriki mara kadhaa na timu tofauti michuano ya CAF kuanzia ngazi za klabu hadi taifa, hivyo kwa Azam itakuwa imelamba dume kwa Taoussi.