Arusha. Mahakama ya Rufaa nchini imebariki uamuzi wa Bodi ya Rufaa za Kodi (TRAB) na Baraza la Rufaa za Kodi (TRAT) ya kukataa madai ya Kampuni ya Aggreko International Projects Limited ya kurejeshewa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ya zaidi ya Sh3.560 bilioni.
Kampuni hiyo ambayo ni tawi la Aggreko International Projects Limited lenye makao yake nchini Uingereza, inajishughulisha na uzalishaji wa nishati ya umeme wakati wa dharura nchini Tanzania.
Katika ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo, ilielezwa kuwa mwaka 2011, mteja pekee wa kampuni hiyo alikuwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Na kampuni hiyo ilikubaliana na Tanesco kuzalisha megawati 100 za umeme, kazi ambayo ilitekelezwa na kukamilishwa kama ilivyopangwa.
Lakini pia, kumbukumbu ya rufaa inaonyesha kulikuwa na mazungumzo kati ya Kampuni hiyo na Tanesco kuhusu uwekaji wa ziada wa megawati 50, ambayo hayakufanikiwa kwa wakati huo.
Hata hivyo, imeelezwa kabla ya kukamilika kwa mazungumzo hayo, kampuni hiyo iliendelea kuagiza jenereta na kulipa kodi ya Sh3.560 bilioni.
Imedaiwa mwaka 2014, TRA ilifanya ukaguzi kwa kampuni hiyo kujiridhisha kuhusu masuala ya kikodi na katika ukaguzi huo, ikabaini kuna kodi ambayo Aggreko ilikuwa imedai irejeshewe kwa kuwa jenereta hizo zilizonunuliwa nje ya nchi zilikuja kwa ajili ya biashara iliyotarajiwa kufanyika.
Kampuni hiyo ilikata rufaa kwa TRAB ikipinga uamuzi wa Kamishna Mkuu wa TRA wa kukataa kuilipa.
Rufaa ya kwanza ilisikilizwa TRAT, haikufaulu kwa sababu mrufani hakuwa na haki ya kurejeshewa kodi hiyo anayodai.
TRA ilifanya ukaguzi kwa kampuni hiyo mwaka 2014 ili kujiridhisha kuhusu masuala ya kikodi. Katika ukaguzi huo, ilibainika kwamba kuna kodi kampuni hiyo ilikuwa imeomba irejeshwe, kwa kuwa jenereta zilizonunuliwa nje ya nchi zilikuwa zimetarajiwa kutumika kwa shughuli za biashara.
Katika Mahakama ya Rufani, rufaa ya madai namba 364 ya mwaka 2021 ilisikilizwa na jopo la majaji watatu, Barke, Dk Paul Kihwelo na Gerson Mdemu, ambao walitoa uamuzi wao Agosti 6, 2024, nakala ya uamuzi huo inapatikana kwenye tovuti ya Mahakama.
Rufaa hiyo ilitokana na hukumu na agizo la TRAT iliyotolewa Aprili 21, 2021, katika rufaa ya kodi namba 34 ya mwaka 2020.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Mahakama ya Rufani iliunga mkono uamuzi wa TRAT na TRAB, na kuikatalia kampuni hiyo madai ya kurejeshewa kodi iliyolipwa kwa jenereta hizo.
Katika uamuzi wake, TRAB ilikubaliana na Kamishna wa TRA na kukataa kurejesha kodi hiyo, ikitupilia mbali rufaa hiyo. Katika ukurasa wa 757 wa kumbukumbu za rufaa, ilielezwa kuwa jenereta hizo hazikuwa kwa madhumuni ya biashara.
Hata hivyo, Jaji alisema kampuni hiyo ilikata rufaa dhidi ya Kamishna Mkuu wa TRA ikipinga uamuzi wa mwaka 2021 kwa madai ya tafsiri isiyo sahihi ya kifungu cha 16 cha Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ya mwaka 1997 (Sheria ya VAT).
Katika rufaa hiyo, kampuni hiyo iliwakilishwa na mawakili Allan Kileo na Norbert Mwaifwani, ambao waliwasilisha hoja tatu kuu.
Miongoni mwa hoja hizo ni madai kuwa kulikuwa na upotoshaji wa ushahidi kwenye rekodi na TRAT katika kushikilia msimamo kwamba jenereta zilizoingizwa nchini hazikuwa kwa ajili ya biashara, hivyo hazistahili kukatwa kodi ya ongezeko la thamani kwa mujibu wa kifungu cha 16 (1) (b) cha sheria husika.
Nyingine iliilenga Mahakama ikidai kwamba ilikosea kisheria kwa kushindwa kutambua kuwa muda wa uagizaji wa bidhaa kutoka nje haukuwa muafaka, ili kuweza kudai kurejeshewa kodi ya ongezeko la thamani kwa ununuzi wa bidhaa hizo.
Rufaa hiyo, iliyosikilizwa Agosti 16, 2024, ilishirikisha upande wa Kamishna wa TRA (mjibu rufaa) ambao waliwakilishwa na mawakili watatu wa Serikali, wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Juliana Ezekiel.
Katika mawasilisho yake, Wakili Allan alidai kuwa jenereta zilizoagizwa kutoka nje zilikuwa kwa ajili ya kuendeleza biashara, na hivyo kampuni ilipaswa kuruhusiwa kukatwa kodi ya ongezeko la thamani. Aliendelea kueleza kwamba jenereta hizo zilikuwa na lengo la uzalishaji umeme na zilihusiana moja kwa moja na biashara ya kampuni hiyo, ambayo ilikuwa imejisajili kibiashara.
Wakili Allan aliongeza kuwa wakati mazungumzo ya mradi wa nyongeza wa megawati 50 na Tanesco yalipositishwa, kampuni ilikuwa tayari imeagiza jenereta hizo, na zilifika bandari ya Dar es Salaam Novemba 17, 2011, huku mazungumzo hayo yakisitishwa rasmi Novemba 21, 2011.
Kwa upande wake, Wakili Juliana alieleza kuwa kampuni hiyo ililipa kodi hiyo kama ilivyotakiwa kisheria kwa kuwa jenereta zilizoagizwa zilikuwa za matumizi binafsi na si kwa ajili ya kuendeleza biashara, ambayo ingempa haki ya kufaidika na msamaha wa kodi. Alielekeza Mahakama kwenye kumbukumbu za rufaa, akibainisha kuwa hakukuwa na shughuli au matarajio ya kibiashara kati ya kampuni na Tanesco kufuatia kufutwa kwa mradi wa megawati 50.
Wakili Juliana pia alisisitiza kuwa kwa kuwa hakukuwa na mkataba rasmi wa kibiashara uliokamilishwa, kifungu cha 16 (1) (b) cha Sheria ya VAT hakitaki kuwepo kwa mkataba wa biashara ili kodi itozwe au kusamehewa.
Jaji Mdemu alianza kwa kueleza kuwa wamezingatia mawasilisho ya mawakili na kumbukumbu nzima za rufaa, na kuwa wanadhani sababu zilizotajwa za rufaa zinatokana na tafsiri ya kifungu cha 16 (1) (b) cha Sheria ya VAT.
Alieleza kumbukumbu za rufaa ukurasa wa 314 inaonyesha awali kulikuwa na mazungumzo kati ya Tanesco na AIPL TZ ambayo hayakufanyika kufuatia kufutwa mradi wa ziada wa megawati 50.
“Tunabainisha zaidi kwamba, ushahidi wa kutokuwepo kwa biashara ulikuwa katika ufahamu wa mrufani (kampuni), kwa sababu uamuzi wa mrufani wa kuagiza jenereta ulikuwa kwa kuzingatia vipengele viwili.”
“Moja kwamba, ilikuwa hitaji la umeme wa dharura na mbili, kwamba, mazungumzo yalikuwa yanaendelea vyema. Uelewa wetu wa Sheria ya VAT juu ya uagizaji bidhaa kutoka nje hutokana na uendeshaji wa sheria,” aliongeza.
Jaji Mdemu alisema wanakubaliana na Wakili Juliana, kwamba wajibu wa kulipa kodi hiyo wakati wa uingizaji wa jenereta ulikuwa wa kisheria.
“Kama ilivyoonyeshwa na TRAT katika ukurasa wa 846 wa rekodi ya rufaa, ambayo tunaona kuwa ndiyo msimamo sahihi, hapakuwa na biashara wala matarajio ya kibiashara kati ya Tanesco na mrufani kuhusu kuongeza uzalishaji wa umeme wa dharura wa megawati 50.”
“Hatuoni kosa lolote katika matokeo ya TRAT kwamba kifungu cha 16(1) (b) cha Sheria ya VAT hakiwezi kutumika kwenye kodi ya VAT kwa sababu jenereta zilizoingizwa nchini hazikuwa kwa ajili ya kuendeleza biashara kati ya Tanesco na mrufani, hivyo tunaiondoa rufaa kwa gharama,”alihitimisha jaji huyo.