Tabora. Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Maimbo Fabian ameeleza kushangazwa na kasi ya makasisi na vijana kuacha imani ya Kikristo na kukimbilia maombezi ya kupata mafanikio kwa miujiza bila kufanya kazi.
Akizungumza leo Jumapili Septemba 8, 2024, kwenye kongamano la nne la kitaifa la Kanisa la Anglikana Tanzania lililojadili masuala mbalimbali ya kimaendeleo na kijamii, Askofu Fabian amesema ongezeko la watumishi wanaoacha kanisa ni la kutia wasiwasi.
“Kumekuwa na kundi kubwa la makasisi pamoja na vijana ambao hawasimami na Kristo; badala yake wanakimbilia kwenye makanisa ambayo siwezi kuyataja, wakitafuta miujiza. Kwa kuwa hawajui kinachofanyika pale ni maigizo, wanajikuta wanatumika vibaya,” amesema Askofu Fabian.
Amesema makasisi wengi wameliacha kanisa na kuhamia huko na wengine wamehama dini na kuukana msalaba.
Askofu huyo amesema imefika wakati watu wanasahau mafundisho na kufanya wanavyojua. “Juzi nilikuwa naangalia kesi ya Sumbawanga, mabinti watatu waliozeshwa ndani ya saa moja na wote wakabadilishwa dini. Hii ni hali ya kushangaza na inapaswa kukemewa kwa nguvu zote,” amesema.
Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Tabora, Dk Elias Chakupewa amesema kuna haja kwa Serikali kuingilia kati kwa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya makanisa yanayofanya upotoshaji.
“Ipo haja kwa Serikali kuchukua hatua za kisheria dhidi ya makanisa yanayoendesha ibada za kupotosha. Mafundisho ya kwamba watu wanaweza kupata utajiri kwa kuomba ni potofu. Biblia iko wazi, Mungu alipomuumba mwanadamu alimpa bustani ya Edeni ailime na kuitunza; hakuna sehemu Mungu alisema mtu atapata utajiri bila kufanya kazi,” amesema.
Amesema mafundisho haya potofu yanayowafanya watu wasifanye kazi na badala yake wanashinda kanisani wakitarajia miujiza.
Adventina Mkosya, muumini wa kanisa hilo, amesema maombezi potofu ambayo yameshika kasi kwenye makanisa yanapaswa kuchukuliwa hatua.
Amesema kizazi kinaangamia kwa kukosa maarifa; “Maombezi haya yanadanganya sana. Mtu anaambiwa apokee kazi ya ukurugenzi wakati amesoma hadi darasa la saba. Serikali inapaswa kuchukua hatua maana kizazi kijacho kitakuwa kinashinda kanisani bila kufanya kazi,” amesema Mkosya.
Naye George Simon, muumini wa Kanisa la Anglikana kutoka Zanzibar, amesema kinachoendelea nchini kuhusu ukuaji wa dini zinazoendesha mafundisho potofu kinapaswa kudhibitiwa na Serikali.
“Tumeona hata juzi kule Rwanda, Rais Kagame alifungia baadhi ya makanisa yanayoendesha ibada za kupotosha. Hivyo, hata hapa kwetu uchunguzi ufanyike na watakaobainika kuombea watu kwa maigizo wachukuliwe hatua kali za kisheria,” amesema.