Dar es Salaam. Kushamiri kwa mahubiri potofu ya dini na kuibuka kama uyoga kwa makanisa na wahubiri, kumemuibua Askofu wa Jimbo Katoliki Kayanga, Almachius Rweyongeza akipendekeza kufanyika mabadiliko ya Ibara ya 19 ya Katiba.
Ibara hiyo ndogo ya (1) na (2) imetoa uhuru kwa mtu kuchagua dini aitakayo na kubadilisha dini au imani yake na kwamba kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiyari ya mtu binafsi.
Askofu Rweyongeza anaona ibara hiyo inaifanya Serikali kutochukua hatua kikamilifu kudhibiti kushamiri kwa vitendo hivyo, kwa kuwa inasema shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za Serikali.
Kiongozi huyo wa kiroho, amesema hayo Ijumaa Septemba 6, 2024 katika Jubilee pacha ya miaka 50 ya Padri na miaka 25 ya uaskofu wa Askofu Desdelius Rwoma wa kanisa hilo, Parokia ya Rutabo Jimbo la Bukoba. Maaskofu, mapadri, watawa wa kiume na kike na waumini walishiriki.
Katika maelezo yake, Askofu Rweyongeza alisema ibara hiyo ndio kiini cha tatizo la sasa.
Hali hiyo kwa mujibu wa askofu huyo, inatokana na kuwapo kwa uhuru wa kuabudu kwa mujibu wa Katiba na kuizuia Serikali kuingia shughuli hizo kumesababisha kuwapo kwa manahodha wengi wanaofanya chombo (imani) kwenda mrama.
Ili kuthibiti mambo yanayoendelea sasa nchini, Askogfu huyo ameishauri Serikali kuiga kile kinachofanywa na mataifa mengine kama Togo na Rwanda, ambayo yameweka vigezo cha mtu kusomea Thiolojia kabla ya kuanzisha kanisa.
Askofu huyo alienda mbali na kukemea miujiza ya uongo ya uponyaji inayofanywa na baadhi ya wahubiri hao na kusema kama kweli wanatenda miujiza ya uponyaji wa kweli, basi wapelekwe chumba cha watu mahututi (ICU) hospitalini kutibu.
Kauli ya Askofu Rweyongeza imekuja kipidi ambacho Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ameitaka Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Ofisi ya Msajili wa Jumuiya za Kiraia, kusimamia kikamilifu Sheria ya Usajili wa Taasisi za Dini.
Pia, Dk Mpango amewasihi viongozi wa dini kuungana na Serikali kukemea vikali mafundisho na matendo yasiyofaa katika jamii na yasiyozingatia sheria za nchi, yakiwamo yanayofanywa na baadhi ya viongozi hao wa dini maeneo mbalimbali.
“Miaka ya karibuni imeshuhudiwa kuongezeka kwa wahubiri wanaojilimbikizia fedha na mali binafsi kutokana na sadaka na mauzo ya vitu mbalimbali na wengi wa waathirika wa mahubiri ya aina hiyo ni wananchi wanaokabiliwa na shida au matatizo mbalimbali ya maisha,” alisema Dk Mpango.
Dk Mpango alitoa kauli hiyo jana Jumamosi, Septemba 7, 2024 mkoani Arusha, ikiwa tayari Serikali imeshachukua hatua ya kulifunga Kanisa la Christian Life na kiongozi wake mkuu Mchungaji Domique Kashoix Dibwe maarufu Kiboko ya Wachawi raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuondolewa nchini.
Kiongozi huyo alidaiwa kutoa mafundisho yenye kuleta taharuki katika jamii na mahubiri ambayo ni kinyume cha maadili, mila, desturi na utamaduni wa Kitanzania na matakwa ya kifungu cha 17 cha Sheria ya Jumuiya.
Madai mengine ni kutoa mahubiri yanayodhalilisha watu madhabahuni, kutoa mahubiri chonganishi na kuhamasisha waumini wa kanisa lake kuua watu kwa dhana au tuhuma za uchawi au ushirikina.
Hatua ya kulifunga kanisa hilo na kumuondoa nchini kiongozi wake mkuu ilikuja siku kadhaa baada ya gazeti la Mwananchi kuchapisha mfululuzo wa habari kuhusu kuwapo viongozi wa makanisa wanaotoza fedha waumini wao na kuwahadaa huku wakijipatia ukwasi mkubwa.
Hata baada ya kanisa lake kufungiwa na yeye kuondolewa nchini, gazeti la Mwananchi lilifichua kuwa Kiboko ya Wachawi aliendelea kutoa huduma akiwa DRC akiwataka watoe fedha ili awafanyie maombi huku akitoa kauli za kejeli.
Akihubiri katika jubilee hiyo, Askofu Rweyongeza amesema uhuru wa kuabudu uliotolewa kwa mujibu wa Katiba ibara ya 19 unatumiwa vibaya na baadhi ya watu.
Amesema ili kudhibiti hali hiyo, ni vyema Serikali na Bunge kuingilia kati lakini ili hilo lifanikiwe ni lazima mabadiliko yafanyike katika kipengele cha 2 cha ibara hiyo inayozungumzia uhuru wa kuabudu.
Kipengele cha pili cha ibara hiyo kinasema: “Bila ya kuathiri sheria zinazohusika za Jamhuri ya Muungano, kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari ya mtu ya binafsi, na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi.”
Askofu huyo amesema: “Bunge na Serikali iangalie upya kwa makini na busara na haraka sana kipengele namba 2, yaani mamlaka ya nchi kutoingilia uhuru wa kuabudu, kuna utata wa nahodha wengi chombo huenda mrama.
“Kuna wababaishaji kwenye viongozi wa dini, sisi mapadri na maskofu tumesoma, mwingine analala usiku anaamka asubuhi ni askofu mnamfuata.”
Akionyesha sura na sauti ya msisitizo, amesema: “Uhuru wa kuabudu ambao hauzingatii kanuni, sheria na desturi si uhuru. Mamlaka za nchi, Serikali haitakiwi kujiweka kando. Iingilie kati mara moja ili amani ya Taifa itawale.”
Akiitolea mfano wa dini zinazovuruga imani, amesema miongoni mwake ni zile zinazohamasisha watu kukanyaga mafuta, huku akisema jambo hilo limewahi kufanya watu kukanyagana, kupoteza maisha na kufanya Taifa kupoteza nguvu kazi ya Taifa.
“Serikali iko kimya na viongozi wa dini wanajiweka kando, baadhi ya dini zinaabudu mashetani na kutoa kafara watu ili watajirike, baadhi wanakesha usiku kucha wakiomba pesa zishuke kama mvua, hawahimizwi kufanya kazi,” amesema Rweyongeza.
Amesema kuna mambo mengi ya ajabu yanayofanyika mitaani na wachungaji kutoka nchi mbalimbali:“Rais (Samia Suluhu Hassan) tunaomba uige mfano wa Togo hawa ndiyo komesha ya utapeli, kiongozi wao aliona watu wanaibiwa na manabiii, mitume kutoka Nigeria akapitisha masharti saba ambayo kila mtu anayetaka kufungua kanisa lazima awe amezitimiza.”
Masharti ni kuwa na cheti cha kuhitimu chuo cha biblia, kuonyesha utaratibu uliotumika kumpa unabii, uchungaji au uaskofu, aoneshe anawajibika kwa nani au chombo gani, mali ni ya nani na akifa atarithi nani, jamii inanufaikaje na uwepo wa kanisa lake kupitia huduma za kijamii kama afya, elimu, maji.
“Kama mtume anasema anafufua watu aende monchwari ya hospitali ya serikali akafufue na apewe cheti kuwa anaweza kufufua watu, kama anaweza kuponya apelekwe ICU au vituo vya walemavu aponye,” amesema Askofu Rweyongeza.
Amesema kupitia hilo kumeifanya Togo kuwa nchi pekee ambayo haina utapeli unaofanywa kupitia makanisa na hata TB Joshua hakuwahi kuthubutu kutia mguu wake.
Nchini Rwanda pia Rais wake, Paul Kagame alifunga nyumba za ibada zaidi ya 7000.
“Kwanini Serikali yetu inapata kigugumizi, kwanini inaona kigugumizi, uhuru wa kuabudu umeporomosha amani ya Taifa kilichobaki ni wimbo, Tanzania kisiwa cha amani,” amesema.
Wakati Dk Mpango akisema hayo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni akizungumza wakati wa sherehe za ufungaji wa makambi ya Waadventista Wasabato jijini Arusha jana Jumamosi, Septemba 7, aliwataka watu wote wanaojihusisha na shughuli za kidini kufuata sheria za nchi.
“Hivi karibuni kuna mchungaji mmoja tulimuondosha nchini kutokana na kukiuka sheria za usajili na mmeshuhudia huko alikokwenda amekuwa akisambaza video kuthibitisha kwamba yale aliyokuwa akiyafanya yalikuwa kinyume kabisa na mafundisho ya kitabu cha dini.
“Yakiwemo masuala ya utapeli, kuwatoza watu fedha kinyume cha utaratibu na kuwaaminisha watu kwamba miujiza inaweza kuwafanya wawe matajiri au kupata ufumbuzi wa matatizo yao,” amesema Masauni.
“Nitoe wito kwa watu wote walioamua kufanya shughuli za kidini kufuata misingi ya kisheria ambayo inalenga dhamira ya kuhakikisha kwamba inafuata mafundisho ya vitabu vya Mungu.
Uhuru wa kuabudu kwa mujibu wa Katiba upo lakini hautakiwi kuvuka mipaka hadi kuvunja sheria za nchi yetu. Hili sizungumzii kwa wageni tu bali hata kwa wenyeji ziko sheria ambazo ni lazima zifuatwe,” amesema.
Hivi karibuni kupitia video kadhaa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Kiboko ya Wachawi alionekana akiwakejeli Watanzania akieleza namna anavyozikosa fedha alizokuwa akiwatoza ambazo anazitumia kwa ajili ya kufanya uwekezaji nchini kwake.
Katika moja ya video hizo, Kiboko ya Wachawi anaonekana akihesabu fedha, huku akisema bado anakumbuka Sh500,000 alizokuwa akiwatoza waumini wake ili awaombee.
Julai 25, 2024 Serikali ilipolifunga kanisa lake lililokuwa Buza, wilayani Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam, katika barua ya kufutwa usajili wa kanisa hilo iliyotolewa na Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa ilitaja suala la kutoza fedha kuanzia Sh500,000 kwa waumini ili awape huduma ya uponyaji wa kiroho, akisema inakiuka matakwa ya kifungu cha 17 cha Sheria ya Jumuiya, Sura ya 337 kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria ya Mabadiliko ya Sheria mbalimbali Namba 3 ya Mwaka 2019.