DPP atia mguu shangingi la wahamiaji haramu

Dar es Salaam.  Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), amewasilisha pingamizi mahakamani akipinga maombi ya Mtanzania aishie Afrika Kusini, Jackson Ngalya anayedai gari lililokamatwa na wahamiaji haramu mkoani Kilimanjaro ni mali yake.

Katika pingamizi hilo, DPP ameiomba Mahakama isisikilize maombi ya msingi na badala yake iyatupilie mbali kutokana na kugubikwa na kasoro za kisheria.

Gari hilo T888 BTY Toyota Landcruiser V8 lilikamatwa Juni 4, 2024 eneo la Njipanda ya Himo, mkoani Kilimanjaro, likiwa na wahamiaji haramu saba, raia wa Ethiopia waliokuwa wakisafiri kuelekea Afrika Kusini.

Tangu kukamatwa kwa gari hilo na baadaye Mahakama kulitaifisha kuwa mali ya Serikali baada ya kukubaliana na ombi la DPP, hakuna mtu aliyejitokeza kudai ni mmiliki hadi Julai 31, 2024 alipojitokeza Ngalya.

Gari hilo liliingizwa na kusajiliwa mwaka 2011 kwa jina la mbunge mmoja wa CCM, lakini umiliki ukahama Juni 24, 2024 kwenda kwa Ngalya, ikiwa ni baada ya kupita siku 20 tangu likamatwe umefanyika likiwa mikononi mwa vyombo vya dola.

Hoja ya ‘mmiliki’ mpya

Katika kiapo cha maombi yake dhidi ya DPP na waethiopia hao saba, Ngalya anaeleza kuwa kuanzia mwaka 2016 hadi sasa, amekuwa akiishi Afrika Kusini na kwamba aliliacha gari hilo nyumbani kwake nchini Tanzania, chini ya uangalizi wa mlinzi.

Kwa mujibu wa kiapo chake hicho, anadai Juni 2024, alijulishwa kuwa gari lake hilo lilikuwa halijulikani lilipo na Juni 3, 2024 alikwenda kituo cha Polisi Oysterbay, Jijini Dar es Salaam na kutoa taarifa ya kupotea kwa gari hilo.

Baada ya hapo, ameeleza kuwa kupitia vyombo vya habari alibaini lilihusika kusafirisha wahamiaji haramu na linashikiliwa kutokana na kesi hiyo ya jinai 16397 ya mwaka 2024 iliyokuwa ikiwakabili wahamiaji hao.

Kulingana na maelezo yake, alishangaa baada ya ufuatiliaji kuwa limehusika katika kesi hiyo ya jinai, huku akisisitiza gari hilo ni mali yake na hana ufahamu wa aina yoyote na jinai iliyotendwa na watuhumiwa hao.

Hata hivyo, DPP ambaye ni mjibu maombi wa kwanza katika shauri hilo, amewasilisha mahakamani pingamizi la awali (PO), akiiomba Mahakama hiyo isilisikilize, badala yake ilitupilie mbali kutokana na kasoro za kisheria.

Habari ambazo Mwananchi imezipata kutoka chanzo cha kuaminika kuhusiana na pingamizi hilo, DPP ameiomba Mahakama hiyo itupilie mbali bila kumsikiliza mwombaji hoja zake katika maombi yake ya msingi kwa kuwa limefunguliwa kinyume cha matakwa ya masharti ya kisheria.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, Hakimu Mkazi, Opotuna Kipeta wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, anayesikiliza shauri hilo ameelekeza pingamizi hilo lisikilizwe kwa njia ya maandishi na mjibu maombi (DPP), alitakiwa kuwasilisha mahakamani hoja zake kuhusu pingamizi hilo Septemba 5, 2024.

Gari lilivyokamatwa, kutaifishwa

Baada ya gari hilo kukamatwa, Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Fakih Nyakunga alisimulia namna wahamiaji hao walivyokamatwa wakiwa katika gari hilo. Hata hivyo, dereva aliyekuwa akiliendesha alitoroka.

“Jana (Juni 4, 2024), tukiwa kwenye majukumu yetu ya kazi maeneo ya Himo, tulikamata raia saba wa Ethiopia waliokuwa wakielekea Afrika Kusini. Tunaendelea na taratibu za uchunguzi na baadaye kuwafikisha mahakamani.

“Mpaka sasa tunaendelea na uchunguzi kufahamu mmiliki wa gari ni nani, kwani dereva alikimbia na kwa mujibu wa sheria za nchi, gari likibainika kutumika kusafirisha wahamiaji haramu litataifishwa na kuwa mali ya Serikali,” alieleza Nyakunga.

Wahamiaji hao walifikishwa mahakamani Juni 14, 2024 na kusomewa mashtaka mawili na mwendesha mashtaka, wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya mashitaka (NPS), Issack Mangunu, ambapo walikiri kutenda makosa hayo.

Washitakiwa hao ni Tensa Matwis, Abi Arose, Buruk Helobo, Arigudo Aromo, Sisy Abera, Mirhetu Sulore na Sharifan Betiso.

Katika shtaka la kwanza, ilidaiwa Juni 4, 2024 eneo la Njiapanda katika Wilaya ya Moshi, washtakiwa hao wakiwa raia wa Ethiopia, waliingia nchini kinyume cha sheria, wakitumia gari T888 aina ya Toyota Land Cruiser.

Katika kosa la pili, ilidaiwa siku hiyo hiyo katika eneo hilo, walikutwa kinyume cha sheria wakiwa ndani ya ardhi ya Tanzania, bila kuwa na hati halali za kusafiria au nyaraka yoyote ya kisheria inayowaruhusu kukaa nchini.

Julai 2, 2024, Hakimu Mkazi, Rehema Olambo akawahukumu raia hao wa Ethiopia kulipa faini ya Sh500,000 kila mmoja au kwenda jela mwaka mmoja. Walishindwa kulipa faini hiyo na kupelekwa gerezani.

Baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, wakili wa Serikali, Agatha Pima kutoka ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), aliiomba Mahakama itoe amri ya kutaifishwa kwa gari lililotumika kuwasafirisha, ombi ambalo Mahakama ililikubali na kutoa amri hiyo.

Related Posts