KOCHA Mkuu wa JKT Tanzania, Ahmad Ally amesema, anafurahishwa na mwenendo wa kikosi hicho japo jambo analolifanyia kazi katika kipindi hiki cha kupisha michezo ya kimataifa ni kutengeneza balansi kwenye eneo la kujilinda na kushambulia.
Kocha huyo aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu baada ya kuachana na Tanzania Prisons alisema, wachezaji wengi ni wapya ndani ya timu hiyo hivyo wanahitaji muda kidogo kuzoeana, japo michezo ya hivi karibuni imempa taswira halisi kikosini.
“Tumeanza Ligi Kuu Bara na mchezo mgumu dhidi ya Azam FC, malengo yetu yalikuwa ni kushinda ingawa tunashuruku kupata pointi moja kwa sababu ukiangalia haikuwa rahisi, ni kweli tulizuia vizuri japo tulifanya pia makosa binafsi,” alisema.
Ahmad aliongeza, licha ya kutoruhusu bao katika mchezo na Azam ila mapungufu hayo yalijitokeza kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Simba iliyopigwa jana Jumamosi na kusababisha kikosi hicho kuchapwa mabao 2-0, hivyo kumpa picha ya kukabiliana na hilo.
“Bao la kwanza lilikuwa la penalti kwa maana eneo la kujilinda lilikosa utulivu lakini hata ukiangalia la pili utaona ni makosa binafsi ya mmoja mmoja, japo kuna maendeleo mazuri ambayo tunazidi kuyafanyia kazi siku baada ya siku kikosini.”
Kocha huyo wa zamani wa Marsh Queens, Mbao na KMC ni miongoni mwa makocha bora nchini kwa sasa na baada ya kulazimishwa suluhu mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam, JKT itaanza safari ya Bukoba kucheza na Kagera Sugar Septemba 16.
Mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Bara baina ya timu hizo uliopigwa Uwanja wa Kaitaba uliisha kwa sare ya bao 1-1, Machi 2, mwaka huu.