Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetaka uchunguzi wa kina ufanyike kubaini wahusika wa mauaji ya kada wa Chadema, Ally Kibao siku moja baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana majina yao wala walipotokea.
Wito wa LHRC unaungana na wa Chama cha ACT-Wazalendo, kilichohoji maswali kadhaa, ikiwemo nani anayefanya matukio hayo huku kikitaka Jeshi la Polisi kuwasaka wahusika.
Kauli za wadau hao, zinakuja baada ya kupatikana kwa mwili wa Kibao, katika eneo la Ununio jijini Dar es Salaam akiwa ameuawa na uso wake ukiwa umejeruhiwa kiasi cha ndugu zake kushindwa kuutambua.
Mwili wa kibao, umekutwa katika hali hiyo siku moja baada ya kuripotiwa kuchukuliwa katika eneo la Tegeta, mbele ya Jengo la Kibo Complex, baada ya basi la alilokuwa amepanda, kuzuiwa na magari mawili.
Kibao anadaiwa jioni ya Septemba 6, 2024 maeneo ya Kibo Complex Tegeta jijini Dar es Salaam, akiwa safarini na basi la Tashrif akitoka Dar es Salaam kuelekea mkoani Tanga alishushwa kwenye gari hilo la kuchukuliwa na watu wasiojulikana majina yao wala wanapotokea.
Tayari mwili wake umefanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Mwananyamala, Kinondoni jijini hapa. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akizungumza na viongozi na wanachama wa chama hicho, ndugu, jamaa na marafiki hospitalini hapo amesema taarifa ya uchunguzi itatolewa kesho Jumatatu, Septemba 9, 2024.
Kutokana na tukio hilo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kikiisihi Serikali ifanye uchunguzi wa kina na haraka kubaini wahusika na wachukuliwe hatua.
Kituo hicho kimesisitiza uchunguzi huo unapaswa kuwa wa wazi ili kuondoa sintofahamu na kurudisha imani ya wananchi kwa vyombo vya ulinzi na usalama.
Kadhalika, kimezitaka mamlaka husika zielekeze juhudi kudhibiti matukio ya namna hiyo ili kupunguza taharuki kwa jamii.
“Jeshi la Polisi lithamini na lidhibiti mianya ya uhalifu ndani ya vyombo vya dola, kuhakikisha watu wasiokuwa dhamana hawapati nafasi ya kujipenyeza na kufanya uhalifu wakijifanya sehemu ya vyombo vya ulinzi,” kimeeleza katika taarifa yake kwa umma.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Anna Henga imetoa rai kwa Rais Samia Suluhu Hassan kutoa tamko la kukemea matukio hayo ya utekaji na mauaji yanayoendelea nchini.
Mbali na LHRC, Chama cha ACT-Wazalendo nacho, kimelaani tukio hilo, kikisema kunaongeza hofu juu ya usalama na amani na kuchafua imani iliyopo kwa wananchi.
“Maswali tunayojiuliza hivi ni nani anayeweza kufanya matukio haya siku zote hizo bila kukamatwa? Je, vyombo vyetu vinazidiwa uwezo na watekaji? Majibu ya wananchi ni kudai kuwa vyombo vyetu ndiyo vinahusika ndio maana haviwezi kujiwajibisha vyenyewe.”
“Tunajiuliza utekaji unafanyika kwa masilahi ya nani? Na kwa lengo lipi?” kimehoji.
Sambamba na hoja zake hizo, kilimtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi, Camilius Wambura awaeleze wananchi wanaohusika na vitendo hivyo, huku Bunge likitakiwa kuunda kamati maalumu kuchunguza mauaji yote ya raia.
Kiongozi mstaafu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter) amelaani tukio hilo na kumtaka Rais Samia kuchukua hatua ikiwemo kuunda tume ya kijaji ili kuchunguza tukio hilo la Kibao na matukio mengine ya watu wanaodaiwa kutekwa ama kupotea.
Jitihada za kulipata Jeshi la Polisi akiwemo IGP Wambura ili kuzungumzia tukio hilo bado zinaendelea.
Hali ilivyokuwa Mwananyamala
Hali ya sintofahamu ilizuka katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam, baada ya mchakato mrefu wa makabidhiano ya mwili wa Kibao.
Sintofahamu hiyo imetokana na urefu wa kikao kilichoketiwa na maofisa wa chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo kinachojadili hatua ya kuukabidhi mwili wa Kibao kwa ndugu na wafuasi wa Chadema kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Hali hiyo imesababisha mvutano kati ya makada wa chama hicho na maofisa katika hospitali hiyo, wana-Chadema wakishinikiza kukabidhiwa mwili na kama kuna uchunguzi mwanasheria wao, Hekima Mwisapu awepo kushuhudia.
Mzozo uliibuka baada ya maofisa wa hospitali hiyo, kumzuia Mwisapu kuwa mmoja wa watakaoshuhudia uchunguzi wa mwili huo, huku makada wa chama hicho wakishinikiza aruhusiwe.
Msimamo wa makada hao, ulitokana na kile kilichoelezwa na baadhi yao kuwa ni muhimu wakili huyo ashiriki ili kupata uhalisia wa kitakachoelezwa na madaktari baada ya uchunguzi.
Wafuasi hao, wakiongozwa na Meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob walianza kugonga mlango wa chumba hicho kulikokuwa kunafanyika uchunguzi na kusababisha mlinzi atoke nje.
Hali hiyo iliibua mabishano kati ya mlinzi na wafuasi wa Chadema, wanachama wakitaka wakili aingie.
Lakini, mlinzi huyo alikaza uzi akisema wanaopaswa kushuhudia uchunguzi huo ni ndugu wa Kibao pekee na si mwingine yeyote.
Baada ya mabishano ya dakika kadhaa, hatimaye walinzi waliridhia mwanasheria huyo aingie katika chumba hicho kushuhudia uchunguzi wa kitaalamu.
Malalamiko ya kikao hicho kuchukua muda mrefu yaliendelea kutolewa na baadhi ya makada wa Chadema na wengine walikwenda mbali zaidi hadi kugonga mlango wa chumba hicho.
Wakati hayo yakiendelea Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, John Mnyika na Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Dorothy Semu waliingia kwenye gari kujadiliana wakionekana kuchoshwa na mchakato huo.
Hata hivyo baadaye walikabidhiwa mwili huo kwa ajili ya taratibu za maziko.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa zaidi