LIGI Kuu Bara imesimama kwa wiki mbili, lakini mastaa wa timu mbalimbali wa timu za ligi hiyo kwa sasa wapo katika majukumu la kimataifa na juzi usiku baadhi yao walikiwasha wakiwa na timu za mataifa yao katika mbio za kuwania tiketi ya fainali ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) 2025 zitakazofanyika Morocco.
Wachezaji wa Simba, Yanga, Singida Black Stars, Namungo ni kati ya waliitwa timu za taifa na kwa mechi zilizopigwa usiku wa juzi, kuna mastaa walioliamsha na kuweka heshima katika mechi hizo za Afrika.
Nyota wa Yanga, Djigui Diarra na Khalid Aucho wamezipeperusha vyema bendera za timu zao za taifa za Mali na Uganda huku wakiwa ni mastaa wa nje wa Ligi Kuu Bara waliocheza dakika zote 90 katika mechi hiozo wakiwa na timu za taifa za Mali na Uganda zilizotoka sare kila moja.
Diarra aliiongoza Mali katika mchezo wa kundi I dhidi ya Msumbiji uliomalizika kwa sare ya 1-1, huku kwa upande wa Aucho akiiongoza Uganda ‘The Cranes’ katika kundi lao la ‘K’ na kutoka sare pia ya mabao 2-2, dhidi ya Afrika ya Kusini, wenyeji wakichomoka katika kipigo dakika za lala salama Afrika Kusini.
Nyota mwingine aliyecheza kwa dakika zote 90 ni kipa wa Singida Black Stars, Mohamed Kamara aliyeiongoza timu ya taifa ya Sierra Leone kutoka suluhu na Chad katika mchezo wa kundi ‘G’ linaloongozwa na vinara Ivory Coast yenye pointi tatu.
Kiungo wa Yanga raia wa Kenya, Duke Abuya anafuatia kwa kucheza dakika 86 akifuatiwa na nyota wenzake, Prince Dube wa Zimbabwe aliyecheza kwa dakika 82 katika mchezo baina ya timu hizo wa kundi ‘J’, uliopigwa Kenya na kumalizika suluhu.
Mshambuliaji wa Yanga, Kennedy Musonda amecheza kwa dakika 75 akiwa na kikosi cha Zambia ambacho kiko kundi ‘G’ kwenye kusaka tiketi ya kufuzu michuano hiyo ambapo kilikutana na dhahama ya kuchapwa mabao 2-0, dhidi ya vinara, Ivory Coast.
Nyota wa Simba, Steven Mukwala amecheza dakika 72 akiwa na Uganda kilicholazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2, dhidi ya Afrika Kusini huku Clatous Chota Chama wa Yanga anayekipiga kikosi cha Zambia akicheza dakika 65.
Kiungo mshambuliaji wa Singida Black Stars na timu ya taifa ya Niger, Victorien Adebayor amecheza kwa dakika 31 katika mchezo wa kundi ‘F’ ambao kikosi hicho kilipoteza kwa kufungwa bao 1-0, dhidi ya Sudan, Septemba 4.
Mastaa wengine walioitwa timu zao za taifa ila hawajacheza mechi hizi za kwanza za kufuzu AFCON ni kipa wa Simba, Moussa Camara na mshambuliaji wa Singida Black Stars, Abdoulaye Yonta Camara ambao wote kwa pamoja wanaichezea timu ya Guinea.
Wengine ambao hawakucheza ni Stephane Aziz KI wa Yanga anaichezea Burkina Faso na Marouf Tchakei anayekichezea kikosi cha Togo.