MTOA HUDUMA ZA AFYA ATAKAYESABABISHA KIFO CHA MGONJWA KWA UZEMBE NITAMTENGUA – MHE. MCHENGERWA

NA MWANDISHI WETU, PWANI.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI),Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema, yeyote atakayeshiriki kufanya uzembe katika vituo vya afya, zahanati na hospitali nchini atachukuliwa hatua kali.

Ameyasema hayo Septemba 7,2024 katika Hospitali ya Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa na vifaa tiba kwa ajili ya huduma kwa watoto waliozaliwa kabla ya wakati (watoto njiti) na watoto wachanga wagonjwa na wenye uzito pungufu.

Vifaa na vifaa tiba hivyo vimefadhiliwa na Taasisi ya Dorice Mollel Foundation.

“Kila anayekwenda kupata huduma za afya kama ni kituo cha afya kama ni zahanati na kama ni hospitali za halmashauri, kila mtoa huduma aende akatoe huduma hii kwa kila Mtanzania kwa wema akimkaribisha vizuri, akimskiliza kero yake vizuri na kumuhudumia mara moja.

“Haya tumekwisha kubaliana na tumepeana mipaka kwamba yeyote atakayeshiriki kufanya uzembe, mwananchi asipate huduma vizuri ikapelekea uzembe wa kifo cha Mtanzania yeyote hospitali yoyote maana yake mganga mkuu wa wilaya, mganga mkuu wa mkoa ninawatengua kesho yake.

“Na hii tumeshakubaliana, sitarudi nyuma kwa hili, ninadhani umenisikia Dkt.Mfaume nikisikia popote Mtanzania amekwenda kupata huduma hajapata huduma vizuri nitachukua hatua.

“Nikisikia popote Mtanzania au mama mjamzito amefariki kwa uzembe au mtoto amefariki kwa uzembe kwa sababu hakuhudumiwa au hakupewa rushwa mtoa huduma kama ilivyotokea kule Kahama na maeneo mengine maana yake wahusika wote pale watakuwa hawana kazi tena, mganga mkuu wa wilaya, mganga mkuu wa mkoa ninawatengua mara moja wala sitanii.

“Na wale waliohusika katika eneo hilo tutachukua taratibu za kinidhamu, sisi kwa kushirikiana na Wizara ya Afya ili kuhakikisha yeyote aliyefanya uzembe mtoto akafariki, mama mjamzito akafariki awe ni daktari awe na degree moja au mbili au tatu tutakamata cheti chake.

“Hatafanya kazi tena katika nchi hii au hata akitoka nje ya mipaka ya mipaka hii hataruhusiwa kufanya kazi ya uganga au kutoa huduma katika Sekta ya Afya maana yake cheti chake kitakuwa kama pambo anaweza kupamba nyumba yake wala hatuna tabu.

“Lakini hataruhusiwa kutoa tiba ndani ya nchi hii na nje ya mipaka ya nchi hii, tutasitisha kila kitu ndiyo utaratibu na wao wanajua, wana viapo.

“Mtanzania anapokwenda kupata huduma lazima asikilizwe na lazima ahudumiwe vizuri, kwa sababu hawa ndiyo wanatufanya tuendelelee kufanya kazi bila wao wannchi hakuna nchi, bila wananchi hakuna Serikali.

“Kwa hiyo huo ndiyo ukweli kwa hiyo kila mtumishi lazima tujishushe na sitanii kwa hili, sitanii hata kidogo atakayejiingiza kwenye mtego huu kesho yake hana kazi wala sitanii.

“Kama ni mganga mkuu wa wilaya tumewapa magari, tutawany’ang’anya magari na tutawarudisha kwenye nafasi zenu za kuwa daktari wa kawaida, wala sina mchezo kwa hili awe mganga mkuu wa mkoa nitafanya hivyo hivyo.

“Na kwa sababu ni mamlaka yangu nitatengua siku inayofuata ninaweka pembeni,tunateua mtu mwingine kufanya kazi katika eneo hili kuwahudumia Watanzania hili sitanii.

“Tumeshakubaliana na Mkurugenzi wa Afya na Naibu Katibu Mkuu Afya muende mkalisimamie, kaeni na wataalamu zungumzeni nao na wale wenye changamoto kaeni mzitatue,”amefafanua Waziri Mchengerwa.

Related Posts