Kibaha. Uvumi na mfululizo wa vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino, umeisababishia familia ya mtoto, Nurudin Bakari mwenye hali hiyo, kufunga safari kutoka Mkoa wa Mwanza hadi Pwani, kwa ajili ya kuokoa maisha yake.
Safari hiyo ilifanyika miaka 21 iliyopita, Nurudin akiwa na umri wa chini ya miaka mitano, baada ya eneo alilokuwa akiishi mkoani Mwanza kuwa na uvumi wa vitendo vya ukatili dhidi ya wenye ualbino.
Kutoka mkoani Mwanza, wazazi wake walifunga safari hadi ilipo taasisi ya Wipahs, Kibaha mkoani Pwani, mwaka 2003 na hapo alianza elimu ya awali.
Akizungumza na Mwananchi, Septemba 7, 2024, kwenye mahafali ya darasa la saba shuleni hapo, baba mdogo wa Nurudin, Bakari Nyinje amesema uamuzi wa kumuhamishia Pwani ulitokana na hatari za kiusalama zilizokuwepo.
“Tulikuwa na hofu kubwa maana shule aliyokuwa anasoma ilikuwa pembezoni mwa mji na wakati huo kulikuwa na taarifa za watoto wenye ualbino kutekwa, kunyofolewa viungo. Tulipambana siku hadi siku na baadaye tukapata ufumbuzi wa kumleta hapa,” amesema.
Baada ya kufika kwenye taasisi hiyo, amesema alipokelewa na asilimia 70 ya gharama za masomo zililipwa na shule hiyo.
“Miaka hiyo ilikuwa hatari sana kuishi na mtoto mwenye ualbino, hasa kwa usalama wake. Watu wenye nia mbaya wanaweza kumchukua kwa nguvu na kuwajeruhi. Tunaushukuru uongozi wa taasisi hii kwa kutusaidia,” amesema.
Katika mazingira aliyokuwepo mtoto huyo awali, amesema hali ilikuwa mbaya kiasi cha baadhi ya shule kukataa kuwapokea watoto wenye ualbino.
Ameishauri jamii kuachana na imani potofu kuhusu watu wenye ualbino, akisisitiza kufanya hivyo ni kuvunja sheria na kutothamini utu wa mtu.
Akizungumza katika mahafali hiyo, Nurudin amezitaka taasisi nyingine kujielekeza zaidi kusaidia jamii, hasa yenye mahitaji maalumu, badala ya kuzingatia faida pekee.
Awali, muasisi wa taasisi hiyo, Haji Sahebu amesema katika kuunga mkono juhudi za Serikali wamekuwa wakiwasomesha wanafunzi wenye mahitaji maalumu bila malipo.
“Tumekuwa tukitenga bajeti ya kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa lengo la kuhakikisha hakuna kundi linaloachwa nyuma katika suala la elimu ambayo ndiyo mkombozi wa maisha,” amesema.
Amesema walimpokea mwanafunzi huyo akiwa kwenye umri mdogo na kumuanzishia masomo cha kushukuru hakuna changamoto yoyote iliyojitokeza hadi sasa anapotimiza miaka 10 ndani ya taasisi hiyo.
“Nurudin ni mmoja wa wanafunzi wengi wenye mahitaji maalumu na wale wanaotoka kwenye familia za kipato cha chini tuliokubaliana tukiwasaidia ili wapate elimu tunaamini tunawapa ufunguo wa maisha,” amesema.
Kaimu Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Hassani Myanza amesema kuna umuhimu wa wazazi na walezi kushirikiana na taasisi mbalimbali kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalumu wanapata haki zao za msingi, ikiwemo elimu.
Amesema Serikali inatoa ushirikiano kwa taasisi binafsi zinazoonyesha nia ya kusaidia makundi maalumu, ikitambua binadamu wote ni sawa na wanahitaji kufikia malengo yao.