Swali: Anti nahisi changamoto za maisha zinaondoa msisimko wa penzi zetu. Kwani mwenza wangu simuelewi kabisa, hasa siku ambazo hali nyumbani inakuwa ngumu, hasisimki hata nikimshika maeneo ninayojua huwa anasisimka.
Angalau kidogo kukiwa na nafuu, hasa siku ninazowalipia watoto ada ya shule, mke wangu anakuwa na ushirikiano sana. Simlaumu kwani ni mvumilivu sana hali yangu kiuchumi inaposumbua, kuna wakati hata mimi mwenyewe huwa nakata tamaa ila yeye hajawahi kulalamika wala kufikiria kuniacha.
Naomba nisaidie nifanye nini ili uhusiano wetu uwe na msisimko licha ya changamoto za maisha tunazopitia, kwani wakati hali ikiwa ngumu, namuhitaji zaidi kuliko wakati mwingine.
Jibu: Kwanza kabisa hili suala la msisimko kuingiliwa na ugumu wa maisha mnapaswa mlimalize kwa pamoja, kwani msisimko kwenye uhusiano ndiyo kila kitu. Mnaweza kulimaliza hilo kwa kulijadili kwa pamoja. Lifanye ndiyo mada na mlizungumze mara kwa mara, hasa wakati mkiwa hampo sawa kiuchumi. Kwenye uhusiano majadiliano ya wenza ndiyo humaliza changamoto zinazojitokeza.
Pia hakikisha una muda wa kutosha kuwa na mwenza wako hata kama huna pesa. Hakikisha unaweka kumbukumbu nzuri kwenye akili yake kwa kufanya yale mambo anayoyapenda yasiyohitaji kutumia pesa. Mfano unaweza kupika pamoja naye hata kama ni chakula cha kawaida kabisa, kufua naye, kutembea pamoja matembezi ya jioni na vitu kama hivyo.
Licha ya kutafuta maisha, maisha kuwa magumu bado penzi linahitaji kumwagiliwa ili liwe la kuvutia, hakikisha unampa hata zawadi ndogondogo mwenza wako kwa pesa hiyohiyo kidogo unayoipata. Usiache kabisa kufanya hivi, kwani naye ni binadamu na anahitaji upendo kama ulivyokuwa unamfukuzia.
Muhimu zaidi mfanye sehemu ya utafutaji wako kwa kumshirikisha katika kila hatua ili ajue kinachopatikana, mnachoweka kwa ajili ya miradi au akiba na mtakachokitumia.
Hii itamfanya awe sehemu ya utafutaji wako na matumizi ili mhurumiane na kubaki katika lengo lilelile la kuanzishwa kwa uhusiano wenu.
Nahisi ana changamoto ya afya ya akili
Swali: Anti naomba nisaidie ni kwa namna gani nitamtambua niliye naye kama ana changamoto ya afya ya akili au la. Kuna vitu anavifanya simuoni kama yupo sawa, ila nashindwa kujua kama ndiyo dalili za changamoto hiyo au ameamua kubadili tabia tu.
Jibu: Kutambua changamoto za afya ya akili kwa uliyenaye inawezekana isiwe jambo rahisi kwa kumuangalia kwa macho au kulinganisha matendo yake. Suala hilo linahitaji vipimo zaidi vya kitabibu.
Ingawa kuna ishara zinazoweza kukufanya uchukue hatua ya kuwasiliana na wataalamu wa afya ya akili kwa matibabu zaidi.
Miongoni mwa dalili hizo ni mabadiliko makubwa ya tabia zake, mfano anakuwa na huzuni ya muda mrefu, hasira au kutokuwa na hamu ya kushiriki katika shughuli za kawaida. Mambo ambayo hapo awali hakuwa nayo. Akiwa na wasiwasi, msongo wa mawazo vinavyochukua muda mrefu ni kiashiria kuwa hayupo sawa.
Pia kama haikuwa kawaida yake kujitenga na marafiki, kutozungumza, lakini hali hiyo inajitokeza na imedumu kwa muda mrefu si dalili nzuri na ikiendelea inaweza kumletea shida zaidi.
Muangalie ulalaji na ulaji wake, kama anakosa usingizi anakesha usiku kucha au amepoteza hamu ya kula na kukata tamaa, hii pia si dalili nzuri.
Kujilaumu, kujidhuru na kunywa pombe kupita kiasi kwa ghafla pia unapaswa uvifanyie kazi.
Kwa sababu mwenye changamoto hiyo hajijui na inawezekana ukimueleza ikakuletea shida, hakikisha unawashirikisha watu wake wa karibu ambao anawaheshimu kwa ajili ya kumkutanisha na mtaalamu wa afya ya akili. Hili ni muhimu sana kuhakikisha anapata tiba, ushauri mapema kabla hajafanya vitu vibaya. Hizi ni dalili na si wote wanaokuwa nazo wanakuwa na changamoto hiyo.
Pamoja na hayo usisahau kuchukua hatua za kujikinga, ikiwamo kukaa mbali unapomuona amechukia sana. Pia si wote wenye changamoto ya afya ya akili wanakuwa na dalili hizi. Waone wataalamu wa afya ya akili uwaeleze kwa kirefu mambo anayoyafanya wao watajua wanaanzia wapi.