Hayo ameyasema leo Septemba 8, 2024 katika tukio la Maazimio ya Kizimkazi lililolenga kuzindua kipindi maalum cha ‘Pika Kijanja’ lililolenga kuwahamasisha Mama, Baba Lishe mkoa wa Dare es Salaam kuanza kutumia nishati safi na salama.
Amewasihi watanzania kushirikiana na Serikali katika kutekeleza ajenda yake ya matumizi ya nishati safi ili kuepusha madhara yanayotokana na matumizi ya nishati sisizo safi na salama
“Niwaombe watanzania tushirikiane na kuanza kutumia nishati safi ili kuondokana na matatizo yanayotokana na nishati zisizo safi kwa kuwa ubaya wa athari zinazotokana na nishati zisizo safi hazionekani leo, na waathirika wakubwa ni wanawake” amesisitiza Dkt. Biteko
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amewataka wananchi kutumia nishati safi kwa kuwa inapatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu.
Akizungumzia ushiriki wa STAMICO katika tukio hilo, Afisa Uhusiano Bi.Bibiana Ndumbaro ameipongeza TBC kwa kuandaa tukio hilo lilowakutanisha mama na baba lishe zaidi ya 2000 ili kuwapa elimu ya matumizi ya nishati.
Ameishukuru Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe.Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kufanya matumizi ya nishati safi kuwa agenda ya kitaifa ambapo Mama Samia amekuwa kinara kati utumiaji wa nishati hiyo.
“Kwa kutambua umuhimu wa mazingira, STAMICO imeamua kuunga mkono agenda hii kwa kutengeneza mkaa mbadala wa Rafiki Briquettes ili kuongeza chachu katika utunzaji mazingira.” alisema Bibiana
Ameeleza kuwa STAMICO inaendelea kuongeza uzalishaji ili kuwafikia watanazania wengi zaidi kwani kwa sasa Inaweza kuzalisha tani 40 kwa saa kupitia viwanda vyake vikubwa vilivyoweka Kisarawe mkoani Pwani na Kiwira mkoani Songwe.
STAMICO inajivunia ushirikiano mkubwa inaoupata kutoka baadhi ya taasisi wadau zikiwemo Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambao ni wawezeshaji kwa watumiaji wa nishati hii, Magereza Tanzania na Mgodi wa Geita (GGML) (ambao ni wanunuzi wa Rafiki Briquettes)
STAMICO inaendelea kutoa wito kwa wananchi kutumia fursa zilizopo katika biashara hii ya nishati mbadala ya Rafiki Briquettes kwa kuwa mawakala, wasambazaji na wauzaji wa mkaa huo ili kuongeza chachu ya Kuhamasisha utunzaji wa mazingira.
STAMICO inashiriki katika utunzaji wa mazingira kupitia jukumu lake la kuchimba na kuongezea thamani madini ambayo ni makaa ya mawe.