Uchaguzi serikali za mitaa: Vigogo ACT-Wazaledo wagawana tena mikoa

Dar es Salaam. Viongozi wakuu wa chama cha ACT-Wazalendo akiwepo kiongozi mstaafu wa chama hicho, Zito Kabwe wanatarajia kufanya ziara ya  awamu ya pili ya maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa kuanzia Septemba 11, 2024.

Ziara hiyo yenye lengo la kuimarisha chama hicho pamoja na kukagua utekelezaji wa azimio la halmashauri kuu ya chama la kuhakikisha kila kitongoji, kijiji na mtaa kina mgombea wa ACT- Wazalendo kwenye uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 27, 2024.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Septemba 8, 2024, jijini Dar es salaam, Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano kwa Umma wa chama hicho, Shangwe Ayo amesema ziara hiyo itahakikisha hakuna kitongoji, kijiji wala mtaa utakaokuwa hauna kiongozi kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa.

“Wanachama 418,000 wameandaliwa kuwa wagombea katika ngazi mbalimbali k uchaguzi huu wa serikali za mitaa,” amesema Shangwe.

Pia, amesema kama ilivyokuwa kwenye awamu ya kwanza ya ziara, awamu ya pili itawahusisha viongozi akiwamo kiongozi wa chama, Dorothy Semu, Makamu Mwenyekiti-Bara, Isihaka Mchinjita, Katibu Mkuu, Ado Shaibu na Zitto.

Amesema huo ni utekelezaji wa agizo la halmashauri kuu ya chama kuwa, kabla ya kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa ni lazima viongozi wakuu wa chama wafanye ziara kwenye kila jimbo katika majimbo yote 214 ya Tanzania Bara.

Shangwe amesema awamu hii ya ziara Dorothy atatembelea majimbo 25 yaliyomo kwenye mikoa ya Pwani, Dodoma, Manyara, Singida, Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga.

Kwa upande wa Mchinjita atatembelea majimbo 21 katika mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro huku Shaibu akitembelea majimbo 29 kwenye mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Geita, Mwanza, Simiyu, Kagera na Mara.

Naye, Zitto atatembelea majimbo 29 kwenye mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma, Mbeya na Songwe.

Hata hivyo, amesema ziara hiyo ya awamu ya pili inakamilisha utekelezaji wa agizo la kuhamasisha kampeni ya chama ya kusajili wanachama milioni 10 kwa miezi 10 ambayo ilizinduliwa rasmi Julai 22, 2024 na ilihusisha majimbo 125 yaliyopo katika mikoa 22, huku ikijiwekea lengo la kuwa Chama chenye idadi kubwa zaidi ya wanachama nchini ifikapo Aprili, 2025.

Related Posts