USHINDI wa bao 1-0 iliyopata Namungo jana Jumamosi katika mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Ligi Championship, Mbeya Kwanza umemfanya ahueni kocha wa kikosi hicho, Mwinyi Zahera aliyesema amepata mwanga katika jukumu alilonalo la kubadili upepo mbaya wa matokeo katika Ligi Kuu Bara.
Licha ya kuonekana kucheza soka safi, Namungo imejikuta ikianza vibaya msimu huu wa Ligi Kuu kwa kupoteza mechi mbili mfululizo za nyumbani dhidi ya Singida Black Stars (2-0) na Tabora United (2-1).
Akiongelea kiwango walichokionyesha katika mchezo huo, Zahera alisema bado wana kazi kubwa ya kufanya na kuhakikisha wanakuwa bora zaidi;
“Tupo kwenye mwelekeo mzuri kwa maana na kiwango cha timu lakini kumekuwa na mapungufu madogomadogo ambayo tumekuwa tukiyafanyia kazi katika wiki hii ya kimataifa naamini tutakuwa bora zaidi katika michezo ijayo. Ni jambo zuri kucheza mchezo bila ya kuruhusu bao hata kama ni wa kirafiki,” alisema kocha huyo wa zamani wa Yanga.
Bao la Namungo katika mchezo huo wa kirafiki lilifungwa na Hassan Kabunda.
Akiiongelea Namungo, nyota wa Mbeya Kwanza, Boniface Nayagawa alisema; “Kiukweli wanatimu nzuri sana, huu ni upepo mbaya tu ambao umepita kwa sababu hata mechi walizopoteza walionyesha kiwango kizuri, ingekuwa mbaya kwao kama wangekuwa wakipoteza huku wakicheza hivyo.”
Baada ya kucheza mechi mbili nyumbani, Namungo ina mechi tatu ugeniniĀ mara Ligi Kuu itakaporudi kutokana kwenye mapumziko ya kupisha kalenda ya FIFA kwa timu za taifa, ikitarajiwa kucheza dhidi ya Dodoma Jiji, Coastal Union na Simba.