Wadau wafunguka kiini cha mauaji nchini

Dar es Salaam. Wimbi la vitendo vya mauaji katika siku za hivi karibuni, limehusishwa na kukithiri kwa matatizo ya afya ya akili, mmomonyoko wa maadili, uelewa duni wa namna ya kuishi, huku umasikini uliopitiliza nao ukitajwa kama moja ya sababu.

Kwa mtazamo wa kisaikolojia, wanazuoni wanasema vitendo hivyo ni dalili ya jamii kupunguza uwezo wa kufikiri vema na kufanya uamuzi sahihi, kunakosababishwa na changamoto ya  afya ya akili.

Lakini, viongozi wa dini wamekwenda mbali zaidi na kuhusisha vitendo hivyo na dalili za mwisho wa ulimwengu kama ilivyotabiriwa katika vitabu vitakatifu, huku mmomonyoko wa maadili ikiwa ni sababu nyingine waliyoitaja.

Msingi wa hoja za wanazuoni na viongozi hao wa dini ni mwenendo wa matukio ya mauaji ya watu, yaliyotokea katika miezi miwili kuanzia Julai hadi Agosti mwaka huu.

Suala hilo la mauaji, lilizungumzwa pia na Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni jana alipokuwa akitoa wito kwa wote walioamua kuingia kwenye shughuli za kidini kufuata misingi ya kisheria.

Alipokuwa mkoani Arusha katika hafla ya Kanisa la Waadventisti Wasabato jana Jumamosi, Septemba 7, 2024, Masauni alisema katika kipindi cha Julai na Agosti, kumeshuhudiwa ongezeko la matukio yanayohusisha mauaji ya kikatili na sababu ni masuala mbalimbali ikiwemo imani za kishirikina.

“Hili jambo linachangiwa na mmomonyoko wa maadili, hakuna mtu hata mmoja ambaye ana haki ya kutenda kitendo chochote kiovu, kinacholenga kuleta athari au madhara kwa mwingine. Dini zote zinakataza maovu hayo,” alisema.

Miongoni mwa matukio hayo ni la Septemba 6, mwaka huu, mama na bintiye walikutwa na mauti baada ya kufanyiwa ukatili wakiwa nyumbani kwao mkoani Dodoma.

Mama, Mwamvita Mwakibasi (33) alikutwa kitandani akitokwa na damu maeneo ya shingoni ikisadikika alichinjwa, huku bintiye Salma Ramadhan (13), alikutwa chini ya kitanda naye akitokwa damu puani na haja kubwa.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Dodoma, Daniel Dendarugano akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Muungano katika Kata ya Mkonze jijini Dodoma waliofika nyumbani kwa mama na mwanaye waliouwa usiku wa kuamkia leo na watu wasiojulikana. Picha ndogo ni Mwomvita Mwakibasi (33) ambaye yeye na mwanaye wameuwawa usiku wa kuamkia leo nyumbani.

Tukio lingine ni la Julai 8, mwaka huu, uhai wa mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Kalunde mkoani Tabora, Salma Mussa (15) ulipokatishwa alipokuwa akielekea shuleni.

Siku hiyohiyo katika Mkoa wa Dodoma, Stephen Mabula (44), aliingia mikononi mwa Polisi baada ya kumnyonga mwanawe wa kambo hadi kufa, baada ya ugomvi uliohusisha wivu na mapenzi na mwenza wake.

Kama hiyo haitoshi Julai 27, mwaka huu mkazi wa Mgongola ‘A’ mkoani Tanga, alipoteza maisha baada ya kukatwa kichwa na watu wasiojulikana akiwa anachuma mboga shambani.

Tukio hilo lilifuatiwa na lililotokea usiku wa kuamkia Julai 31, mwaka huu, wivu wa mapenzi ulikatisha uhai wa Mary Mushi, mkazi wa Moshi, mkoani Kilimanjaro, aliyeuawa kwa kukatwa mapanga na  mwili wake kutupwa shambani kwao.

Agosti 9, mwaka huu mkoani Dodoma, maisha ya Angela Joseph yalikatishwa baada ya kuuawa na mpenzi wake kwa kile kinachodaiwa ni wivu wa mapenzi.

Marehemu Angela Stephano (aliyepo nyuma) akiwa kwenye picha ya pamoja na mama yake mzazi, Mary Msuya enzi za uhai wake.

Angela aliuawa kikatili na mwili wake kufungwa kwenye mfuko wa nailoni kisha kuingizwa kwenye kiroba na baadaye kutupwa porini.

Kesho yake, Agosti 10, mwaka huu, Mganga wa Kienyeji, Nkamba Kasubi alikamatwa na Jeshi la Polisi akidaiwa kuua na kuwafukia watu 10 katika mikoa ya Dodoma na Singida. Baadhi yao inadaiwa walizikwa wakiwa hai.

Katika Mkoa wa Tabora, Agosti 14, mwaka huu, Juliana Mbogo (40) alinyongwa hadi kufa na mwenza wake na mwili wake kufichwa uvunguni mwa kitanda. Wivu wa mapenzi ulitajwa kama moja ya sababu.

Agosti mwaka huu, mwili wa mfanyabiashara ndogondogo, maarufu Machinga, John Gerald (30) ulikutwa umetupwa baada ya kuuawa kwa kuchomwa visu kadhaa tumboni mkoani Dodoma.

Mkazi wa Mbuyuni kata ya Kizota, Michael Richard (36) enzi za uhai wake.

Agosti 28, mwaka huu mkoani Dodoma, Michael Richard alipoteza uhai baada ya kuuawa kisha nyumba yake kuchomwa moto, hali iliyowajeruhi mkewe na mwanawe. Sababu inadaiwa ni kisasi.

Alichokisema Askofu Malasusa

Kutokana na kushamiri kwa matukio hayo, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa akizungumza na Mwananchi jana Jumamosi, Septemba 7, 2024 amehusisha mwenendo huo na kukithiri kwa mmomonyoko wa maadili uliosababishwa na binadamu kuacha kumwamini Mungu.

Hali hiyo kwa mtazamo wa Askofu Malasusa, imesababisha binadamu kuamini katika ushirikina, jambo linalowafanya wengi kujikuta katika matendo ya mauaji.

Ameeleza matukio hayo si hatari kwa binadamu pekee, bali ni chukizi kwa Mungu na maombi ya kuzitakasa roho ziondokane na fikra za mauaji ndiyo silaha njema, itakayokabili changamoto zilizopo.

“Kwanza matukio haya ni chukizo mbele za Mungu. Watu wote tunahimizwa kuomba roho ya mauaji itoweke ili watu wasiishi kwa hofu,” amesema, Dk Malasusa ambaye pia ni Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

Umuhimu wa elimu hasa za kidini ndilo jambo alilopendekeza, ili kuwafanya binadamu watambue baadhi ya matendo hayampendezi Mungu.

“Tutambue ushirikina ni chukizo kwa Mungu. Ushirikina ni kazi ya shetani. Watu wamrudie Mungu na kuachana na imani potofu,” amesisitiza.

Sauti ya pamoja kukemea vitendo hivyo, amesema ndiyo njia muhimu inayopaswa kutumika kupunguza au kumaliza kabisa mwenendo huo.

“Upendo wa Mungu ukitawala hatutakuwa na roho ya mauaji,” amesema Askofu Malasusa.

Dalili za mwisho wa ulimwengu

Kwa mtazamo wa kiroho matendo hayo ni dalili za mwisho wa ulimwengu, kama inavyofafanuliwa na Mkuu wa Habari na Mawasiliano wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji John Kamoyo.

“Labda siyo rahisi kupata jibu la moja kwa moja. Nikiwa mchungaji na mtumishi wa mambo ya kiroho mimi nitakupeleka katika mambo ya kiroho zaidi, hii ni dalili ya mwisho wa maisha,” amesema.

Ameujenga mtazamo wake huo kwa kurejea kitabu cha Biblia Timotheo 3:1-5, akisema kuna aya zinazoakisi namna binadamu tunavyoishi siku za mwisho ambazo huwa ni za hatari.

“Ukisoma aya hiyo utaona inaeleza watu wenye kujipenda wenyewe na wasiowapenda wa kwao,” ameeleza.

Kujenga hofu ya Mungu mioyoni mwa watu, Mchungaji huyo ameitaja kama suluhu pekee ya matendo hayo, huku akisisitiza umuhimu wa kuwafundisha watu kuziepuka jamii zenye tabia mbaya.

“Tuwafundishe watu kuwa na hofu ya Mungu, japokuwa unabii huu utaendelea sana mpaka Yesu atakaporudi. Kuwafundisha watu wajiepushe na watu wa namna hiyo wakimwamini Yesu kwelikweli,” ameeleza.

Mwanazuoni wa masuala ya ustawi wa jamii, Dk Zena Mabeyo amesema uelewa duni wa namna sahihi ya kuishi na kutimiza malengo, ndiyo sababu kuu ya vitendo hivyo.

Katika ufafanuzi wake, amesema baadhi ya watu wanakwenda kwa waganga na kushauriwa wauwe ili kupata utajiri, wanajikuta wakitekeleza kwa sababu hawana uelewa wa njia sahihi za kutajirika.

Hata wale wanaouwa kwa sababu ya wivu wa mapenzi, amesema ni kwa sababu hawana uelewa wa mbinu za kukabili hisia zao au kudhibiti matendo yatakayowasababishia wivu huo.

“Kwetu (Tanzania) kuna shida ya elimu na uelewa sahihi wa nini binadamu anatakiwa afanye ili kufikia malengo yake,” amesema.

Umasikini uliopitiliza nao ni sababu nyingine iliyotajwa na Dk Zena kama chanzo cha watu kujihusisha na vitendo vinavyokatisha maisha ya wengine.

“Umasikini wa mali unasababisha umasikini wa fikra hatimaye kila unachoshauriwa unajikuta unafanya, ndiyo hawa tunaowaona wameua kisa watajirike na vinginevyo,” amesisitiza.

Lakini yote hayo, Dk Zena amesema msingi wake ni uelewa duni wa namna ya kuishi, akifafanua iwapo watu wangeelewa kiungo cha mtu hakiwezi kukusababishia mafanikio wasingevitafuta.

Mwanazuoni huyo ambaye pia ni Mhadhiri katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii, amesema kunahitajika nguvu ya pamoja kukabili vitendo hivyo, isiachiwe Serikali pekee.

“Tunapaswa kujengeana uwezo wa kiuchumi kwa sababu wengine wanaingia huko kwa sababu za kukosa njia ya kujiinua kiuchumi,” amesema.

Amesema suluhisho lingine ni kuwachukulia hatua kali kwa watakaobainika kufanya vitendo hivyo, ili kujenga woga kwa wenye matarajio ya kufanya hivyo.

Dk Zena amesema ni vema kuwa na mbinu za kudhibiti mapema, wale wote wanaoibuka kutaka usajili wa kutoa huduma mbalimbali mathalan za tiba asili au za kiroho.

“Tunapaswa kudhibiti watu kuanzisha asasi mbalimbali za kiroho na kidini, wanaotaka usajili wachunguzwe wanakotoka na mwenendo wa maisha yao,” amesema.

Akizungumzia mwenendo huo, Rais wa Chama cha Wanasaikolojia Tanzania, Dk Magolanga Shagembe amesema ni dalili ya kukithiri kwa matatizo ya afya ya akili miongoni mwa wananchi wengi.

Tatizo la afya ya akili kwa mujibu wa Dk Shagembe, linaathiri uwezo wa binadamu kufanya uamuzi sahihi na hisia zake kwa ujumla, hivyo mara nyingi anajikuta akiangukia kuamua vibaya.

Katika ufafanuzi wake huo, ameeleza hata anayefanya mauaji kwa sababu za kishirikina, aghalabu hujikuta katika kitendo hicho baada ya kujiuliza maswali mengi na uwezo wake wa kufanya uamuzi umepungua kiasi cha kumshinikiza aue.

“Mtu mwenye akili timamu lazima atajiuliza kuna faida gani ya kupata ninachokitaka kwa mganga kama nitapoteza uhai wa mtu wangu wa karibu, kwa nini nifanye hivi kutimiza mahitaji yangu.”

“Akijiuliza hayo kama akili yake ipo sawa kabla hajafikia kutoa uhai wa mtu mwingine anakuwa ameshapata majibu yanayomuondoa kwenye nia ya kufanya mauaji,” amesema.

Dk Shagembe amesema kwa mtu mwenye matatizo ya afya ya akili anapojiuliza maswali kama hayo, mara nyingi hapati majibu chanya na ndipo anajikuta akifanya mauaji kama alivyoelezwa na mganga.

Mazingira hayohayo, amesema ndiyo yanayowakabili wale wanaokatisha uhai wao, akifafanua hufanya hivyo baada ya kujiuliza maswali mengi na kushindwa kupata majibu sahihi.

Lakini, mwenendo huo, Dk Shagembe amesema unaashiria uwepo wa ombwe la upatikanaji wa huduma za afya ya akili na msaada wa kisaikolojia katika jamii.

“Tunahitaji kufikiria namna ya kuzitoa huduma hizi nje ya hospitali na katika ustawi wa jamii ili kuruhusu hata watoa huduma binafsi waanzishe vituo vyao kwenye vijiji na mitaa, ili mtu akipata changamoto ajue eneo la kukimbilia kabla hajafanya maamuzi hatari,” ameeleza.

Malezi ni sababu nyingine iliyotajwa na Dk Shagembe, akifafanua baadhi ya watu wamelelewa kushindwa kukabiliana na changamoto za maisha na hivyo inakuwa rahisi kuamua vibaya pale anapokabiliwa nazo.

Ili kukabiliana na hayo, amesema ni muhimu kutoa elimu kwa jamii iwe na utambuzi wa masuala ya kisaikolojia na kuwawezesha wananchi kutatua changamoto zinazowakabili.

Ameeleza elimu hiyo ni vema ijikite kuwajuza wananchi kuwa haiwezekani kunufaika au kutatua changamoto zako kwa kukatisha uhai wa mwingine.

Amependekeza uwekezaji ufanyike kwenye utafiti wa kubaini sababu za kina za matendo hayo na mbinu za kitaalamu za kuyakabili.

Kadhalika, ametaka Serikali ije na sheria inayowatambua, kuwasajili na kuwasimamia watoa huduma za afya ya akili, saikolojia ili kuhakikisha zinatolewa kwa kuzingatia maadili.

“Kumekuwa na wimbi la watu wanaozitoa hizi huduma badala ya kusaidia watu, wanawaumiza zaidi hali inayosababisha wanakata tamaa na kujikuta wakifanya maamuzi yasiyofaa,” amesema.

Ameeleza kuna umuhimu wa shuleni kutolewa elimu ya stadi za maisha zitakazomwezesha mtu kukabili changamoto na ajue wapi anakopaswa kukimbilia pindi atakapotatizwa.

Related Posts