Mwanza. Wakati miti zaidi ya milioni 266.9 ikipandwa mwaka 2023/24 kupitia kampeni ya upandaji na utunzaji wa miti milioni 1.5 kwenye halmashauri zote nchini, Serikali imeshauriwa kusimamia upandaji miti asili ili kuwezesha upatikanaji wa dawa za asili.
Akizungumza leo Jumapili Septemba 8, 2024, Profesa Suleiman Mwenda kutoka Shirika la Kimataifa la Revoobit linalojishughulisha na dawa za asili amesema licha ya juhudi za jamii kupanda na kutunza miti, kuna changamoto ya kuingizwa kwa mbegu na matunda ambayo siyo ya asili ya Afrika.
Profesa Mwenda amesema hayo kwenye ziara ya wafanyakazi wa shirika hili waliyoifanya katika Hifadhi ya Taifa ya Saanane.
“Tunapoanza kutoa mmea huu na kuweka mwingine wa kisasa, kama embe la kisasa au mpera wa kisasa, tunapoteza asili yetu na tunaingia kwenye mimea ambayo siyo ya kwetu, na katika utengenezaji wa dawa za asili, huenda mimea hiyo isifanye vizuri,” amesema Profesa Mwenda.
Ameongeza kuwa, “itafika siku tutatafuta mti wa mwarobaini tusiuone, mronge tusiuone, au mbuyu usionekane hivyo, katika upandaji wa miti, nashauri tupande ya asili.”
Katika ziara hiyo yenye lengo la kujionea mimea mbalimbali ya asili pamoja na vivutio vya kitalii, ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali kukuza utalii kwa wazawa na wageni, Profesa Mwenda amesema Tanzania ina uwezo mkubwa wa kupanda miti ya asili, mingi ikiwa ni mimea ya dawa na kuilisha dunia, hivyo kujipatia fedha nyingi za kigeni.
Meneja wa Revoobit Mkoa wa Mwanza, Catherine Christopher ameshauri jamii kutumia vyakula vya asili kwa wingi, kwa madai kuwa vya viwandani vina athari kubwa mwilini, hususan kwenye seli hai. Akizungumzia umuhimu wa miti ya asili, Silvester Hande ameshauri kuwa mkakati wa kitaifa wa upandaji miti uweke mkazo kwenye upandaji na utunzaji wa miti ya asili.
“Turudi kwenye mimea yetu ya asili ili kupunguza magonjwa mengi kama tunavyoona sasa. Pia, tutumie dawa za asili kwa sababu zinaenda moja kwa moja kwenye seli za mwili na kuongeza kinga. Unapokuwa na kinga ya kutosha, mwili unakuwa na uwezo wa kupambana na magonjwa,” amesema Christopher.