Wakali 40 kushiriki vita ya fimbo

WACHEZA Gofu Wanawake 40 kutoka ndani na nje ya nchi wamethibitisha rasmi kuwania taji la ubingwa wa mashidano ya   Tanzania Open ambayo yanaanza siku ya Alhamisi jijini Arusha.

Idadi hiyo, kwa mujibu wa katibu wa mashidano, Rehema Athumani, inaweza kuongezeka kwani dirisha la usajili bado halijafungwa.

“Wacheza gofu 40 ndiyo waliothibitisha kushiriki hadi kufikia Jumamosi jioni na tunategemea wengine zaidi, hasa kutoka nchini Kenya ambako ni kiasi cha mwendo wa saa mbili kufika Arusha, kujiunga nasi,” alisema katibu huyo wa mashindano.

Akiendelea, alisema wengi wa wachezaji wanatoka nchini na nchi zilizokaribu na Tanzania za Kenya, Uganda, Rwanda na Zambia.

“Mialiko tuliyoituma kwa vyama na vikundi vyote vya gofu ya wanawake barani Afrika imenza kujibiwa na hadi kufikia Jumamosi hii tulikuwa na zaidi wacheza gofu 40,” alisisitiza.

Mashindano haya ya wazi  ni mtihani mwingine kwa wanawake  wa Tanzania kuthibitisha ubora wa nyumbani baada ya kufanya vizuri katika mashindano ya wazi ya wanawake katika nchi za Zambia, Kenya na Uganda.

Hali kadhalika, mashindano yatampa kipimo Madina Iddi ambaye amekuwa na ubora uliotukuka katikamashindano mbalimbali ya wanawake nje ya nje.

Madina, kutoka Arusha Gymkhana Club ameshinda mataji matatu ya ubingwa wa gofu ya wanawake katika nchi za Zambia na Uganda.

Pia watakuwa wachezaji tegemeo kwa upande wa Tanzana ni Neema Olomi kutoka Arusha ambaye aliyefanya vizuri nchini Kenya na Uganda pamoja na Aalaa Somji ambaye amejijengea uzoefu mkubwa kwa kucheza mashindano makubwa ya Zambia na Uganda.

Yakienda kwa jina rasmi la Tanzania Ladies Open, mashindano haya ni ya siku tatu na yatapigwa katika mashimo 54  ya viwanja vya gofu vya Arusha Gymkhana kuanzia Alhamisi, Septemba 13 hadi 15 mwaka huu, kwa mujibu wa chama cha gofu ya wanawake nchini,TLGU.

Licha ya Madina aliyeshinda mataji matatu, Tanzania pia inawategema wachezaji kama Hawa Wanyeche, Vicky Elias na Loveness Mungure ambao pia wamefanya vizuri katika mashyidano ya Kenya na Uganda.

Licha ya kuwa ni chipukizi Aalaa Somji  aliweza kupiga hole-in-One(ace) licha ya kumaliza katika nafasi ya nne nchini Uganda wakati Hawa Wanyeche alimaliza wa pili na Olomi wa tatu katika mashindano ya hivi karibuni ya John Walker Uganda Open.

Tanzania itatumia mashindano haya kwa ajili ya kupata wachezaji bora kwa ajili ya timu ya taifa itakayoshiriki katika mashidanano ya ubingwa wa  Afrika nchini Morocco.

Related Posts