Watumia miaka miwili kujenga daraja la Sh10 milioni

Tabora. Wananchi wa Kata ya Chemchem Manispaa ya Tabora, wamefanikiwa kukamilisha ujenzi wa daraja lenye urefu wa futi 12 na upana wa futi 10 kwa gharama ya Sh10 milioni baada ya watu kusombwa na maji katika eneo hilo.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Septemba 8, 2024, Diwani wa Chemchem, Kasongo Risassi amesema waliamua kuchukua hatua baada ya eneo lilipo daraja hilo kusababisha vifo vya zaidi ya watu wanne waliosombwa na maji.

“Kweli wakazi wa Chemchemi wamechangishana zaidi ya shilingi milioni 10 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa daraja kwenye Mto KLenge  la kuvukia kwa miguu na magari baada ya kuwepo kwa adha ya watu kushindwa kuvuka hususan nyakati za masika kwa kuwa maji yanakuwa mengi,” amesema Rissasi.

Amesema kutokana na uwepo wa changamoto hiyo, waliamua kuanza hamasa ya kuchangia ujenzi huo na wakafanikiwa kukusanya Sh10,247,000.

“Kaya 500 kutoka mitaa ya Bakari, Baruti na Chemchem walichangia ili daraja hili liweze kupatikana na sasa ujenzi wake umekamilika,” amesema diwani huyo.

Khadija Mrisho mkazi wa Chemchem amesema eneo ambalo limejengwa daraja hilo limekuwa kero ya muda mrefu kwa wakazi hao ambapo kukamilika kwake kutaleta afueni.

“Mwanzo eneo hili la mto Kenge watu tulikuwa tunashindwa kuvuka maji yakijaa, wakati wa kiangazi watu wanavuka bila tatizo lakini ukifika wakati wa masika, eneo hili linakua halifai maana kuna watu wanne wameshafariki baada ya kusombwa na maji, kiukweli ilikuwa kero kubwa lakini wananchi tumeamua na tumeweza,” amesema Mrisho.

Akiunga mkono hoja hiyo, Christopher Abraham amesema wakati wa masika maji huwa mengi jambo linalosababisha baadhi ya shughuli kukwama.

“Mvua kubwa ikinyesha mto huu unajaa maji na wakati mwingine maji yanaingia kwenye makazi ya watu lakini kutokana na ujenzi wa daraja hili kukamilika, utaleta nafuu kubwa na watu watavuka kwa amani,” amesema mkazi huyo.

Zakayo Mussa mkazi wa chemchem amesema,

“Mfano hapa kwetu kwa mwaka huu tu watu watatu walinusurika kufariki baada ya kusombwa na maji na kuokolewa, hivyo miradi kama hii inayotusaidia wenyewe kama tunaweza kuchangia lifanyike ili tuokoe familia maana hapa waliokuwa wanazama walikua wanafunzi kwa kiasi kikubwa,” amesema.

Related Posts