Moshi. Ni msiba mzito, ni maneno aliyoyatumia Askofu wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Benson Bagonza kuelezea namna alivyoguswa na msiba wa Askofu wa Dayosisi ya Pare ya KKKT, Elinaza Sendoro.
Ajali iliyochukua uhai wa Askofu Sendoro ambaye ndio Askofu wa kwanza wa Dayosisi ya Mwanga, akihudumu kwa miaka minane hadi umauti ulipomkuta, ilitokea jana Septemba 9,2024 saa 1:30 katika eneo la Kisangiro wilayani Mwanga.
Askofu Sendoro ndiye askofu wa kwanza wa Dayosisi ya Mwanga aliyeingizwa kazini Novemba 6, 2016 baada ya kuzaliwa kwa dayosisi hiyo iliyotokana na kugawanywa kwa dayosisi mama ya Are, baada ya mgogoro wa miaka 18.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, aliiambia Mwananchi kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya gari aina ya Toyota Prado alilokuwa akiendesha kutokea Njiapanda ya Himo kugongana na lori aina ya Scania lililokuwa likitokea Tanga.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, chanzo cha ajali hiyo bado kinachunguzwa lakini uchunguzi wa awali unaonyesha marehemu alikuwa anajaribu kuyapita magari yaliyokuwa mbele yake, ndipo alipogongana uso kwa uso na lori hilo.
Mmoja wa watu waliofika eneo la ajali muda mfupi baada ya ajali ni muumini wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Basil Lema alyeisema ajali hiyo ilikuwa mbaya na gari la Askofu liliharibika vibaya na alishuhudia mtoto wake akitoka salama.
“Nilifika pale saa moja baada ya ajali na nimekuta mwili wa baba Askofu umeshaondolewa na kupelekwa Hospitali ya KCMC. Kwa namna ajali ilivyo kwa kweli ni mbaya, ila mtoto wake wa kiume nilimuona alitoka salama,”alisema.
Alichokisema Askofu Bagonza
Askofu Bagonza alisema baada ya Askofu Sendoro alipopata wito wa kuwa Askofu wa Dayosisi mpya ya Mwanga iliyozaliwa mwaka 2016, alimtafuta na kumuomba ushauri ambapo alimwambia aupokee kwa kuwa ni wito wa Mungu.
“Alipopelekewa wito alikuwa kwenye shirika la United Evangelical Mission au UEM alikuwa ni mratibu wa Kanda ya Afrika. Kwa hiyo alipopewa huo wito alinitafuta nikamwambia huo ni wito wa Mungu. Nafasi aliyokuwepo ilikuwa kubwa,”alisema.
“Ni msiba mzito sana kwangu, hata sijui nisemeje. Unajua baada ya kuwekwa wakfu ile Novemba 16, baba Askofu Sendoro aliniandikia barua akiniomba niwe mentor (mshauri) wake. Tumekuwa na ushirikiano mkubwa sana,”alieleza.
Askofu Bagonza amesema mbali na ombi hilo, lakini alimuomba waanzishe ushirikiano kati ya Dayosisi ya Mwanga na ya Karagwe, lakini yeye (Bagonza) akamshauri waongeze ya tatu ambayo ni Dayosisi ya Pare ya KKKT.
“Kwa hiyo tukaanzisha ushirikiano huo. Wakakusanya wachungaji wote wa Dayosisi ya Pare na Mwanga wakaja hapa Karagwe tukawasambaza katika majimbo yetu. Jambo hilo lilikuwa zuri sana na lilifungua milango ya uponyaji”
“Tulianzisha kitu tunakiita Trinity Partnership. Kwa hiyo kukiwa na ubarikio kwao nakwenda na sisi tukiwa nao huku wanakuja. Ni pigo kubwa sana kwa Trinity yetu. Nilipopokea taarifa hizi niliona kama naota lakini yote ni mipango ya Mungu”
Wachungaji Mwanga wamlilia
Mchungaji wa Usharika wa Mruma katika dayosisi hiyo ambaye kwa sasa yuko mapumzikoni kwa matibabu, Richard Muzze alisema wamepokea kwa mshituko msiba huo na awali yeye binafsi aliona kama ni taarifa za kuzusha.
“Sasa kadri muda ulivyokuwa unaenda nikaendelea kupokea simu kutoka kwa wachungaji wenzangu na waumini, baadhi wakiniuliza kama ninafahamu na wengine wakinielezea ajali hiyo. Kwa kweli ni askofu alikuwa na maono,”alisema.
Kwa upande wake, mchungaji kiongozi wa Usharika wa Lambo wa Dayosisi hiyo, David Assery, alisema askofu wao alikuwa ni kiongozi wa kiroho mwenye maono makubwa na walikuwa na matarajio makubwa naye ya kuwafikisha Kanani.
Mmoja wa washarika alishiriki katika mchakato wa kuzaliwa kwa Dayosisi ya Mwanga, Rodgers Msangi alisema Jumamosi ya Septemba 7,2024 alikutana na baba Askofu, akashusha kioo na wakaongea ma chache, kisha akaondoka.
“Mwenyezi Mungu ampe pumziko la milele kwa kweli. Mbali na masuala ya kiroho, lakini nitamkumbuka kwa namna alivyokuwa mkereketwa wa mazingira na nilikuwa bega kwa bega kuhakikisha mifugo haizagai na kuharibu mazingira”