Askofu Sendoro wa KKKT afariki dunia kwa ajali Kilimanjaro

Mwanga. Askofu wa Dayosisi ya Mwanga ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Chediel Sendoro amefariki dunia usiku wa Jumatatu, Septemba 9, 2024 kwa ajali ya gari.

Ajali hiyo imetokea eneo la Kisangiro, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimaniaro, baada ya gari alilokuwa akiendesha Askofu Sendoro kugongana uso kwa uso la lori.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema ajali hiyo imetokea leo saa 1:30 usiku, wakati gari lililokuwa likiendeshwa na Askofu huyo kutokea barabara ya Njiapanda ya Himo-Mwanga kuyapita magari mengine na kugongana uso kwa uso na lori aina ya scania   lililokuwa likitokea Tanga -Arusha.

“Ni kweli leo saa 1:30 usiku huu kumetokea ajali na Askofu Sendoro amefariki dunia eneo la Kisangiro, Wilaya ya Mwanga ambapo gari aina ya Toyota Prado lililokuwa likiendeshwa na Askofu kutokea barabara ya Njiapanda ya  Himo-Mwanga lilipata ajali na kusababisha kifo chake,” amesema Kamanda Maigwa

Kamanda Maigwa amesema chanzo cha ajali bado kinachunguzwa na tayari mwili wa marehemu umechukuliwa eneo la tukio na kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mwanga.

Askofu Sendoro ndiye Askofu wa kwanza wa Dayosisi ya Mwanga aliyeingizwa kazini Jumapili ya Novemba 6, 2016 baada ya kuzaliwa kwa dayosisi hiyo mpya iliyotokana na kugawanywa kwa dayosisi mama ya Pare.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa zaidi

Related Posts