Balaa la walimu waliozaliwa miaka ya 1980

Ualimu ni taaluma inayotaka nidhamu na maadili ya hali ya juu.Hilo ni kwa kuwa ndio taaluma inayohusiana moja kwa moja na malezi ya watoto.

Hata hivyo, uzoefu unaonyesha kada hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo utovu wa maadili na ukengeukaji wa miiko miongoni mwa walimu.

Matukio kama vile walimu kuwa na uhusiano na wanafunzi wao, ulevi na hasira kubwa kwa wanafunzi wanapowarudi, sio mageni nchini, na bila shaka yanaweka doa katika taaaluma hiyo nyeti na adhimu.

Taarifa za Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) zinaonyesha tangu mwaka 2016, tume hiyo imepokea mashauri ya kinidhamu 11,396 yakiwahusu walimu 7579.

Makosa waliyokutwa nayo ni pamoja na kughushi vyetu mashauri 1438 (sawa na asilimia 33.5), uhusiano wa kimapenzi mashauri 328, ulevi 89 na uzembe kazini mashauri 56.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Kamishna wa TSC, Mariam Mwanilwa, walimu waliozaliwa kati ya mwaka 1980 hadi 1988, wameonekana kuwa vinara wa mashauri hayo kuliko rika jingine katika kada hiyo ya ualimu.

“Kwa kuangalia takwimu hizo, ufanyike utafiti kuangalia aina ya makosa, umri na jinsi ambayo walimu wamekuwa wakituhumiwa kuyafanya zaidi,”anasema.

Utovu wa nidhamu umekuwa ukiimong’onyoa taaluma ya ualimu nchini, ndio maana haikuwa ajabu mwaka 2022 TSC kuweka bayana kuwa jumla ya walimu 919 walifukuzwa kazi kwa sababu hiyo.

Walimu hao walifukuzwa kazi atika kipindi cha Machi, 2021 hadi Septemba mwaka 2022 kutokana na makosa mbalimbali ya kinidhamu huku kosa la utoro likiongoza kwa asilimia 68.9 ya makosa yote.

Akitangaza hatua hiyo, Katibu wa TSC, Paulina Nkwama alisema walimu 1,952 walifunguliwa mashauri ya kinidhamu na kati ya mashauri yaliyofunguliwa, 1,362 (sawa na asilimia 69.8) yalihusu utoro.

Alisema mashauri 260 (asilimia 13.3) yalihusu kughushi vyeti, 119 (asilimia 6.1) yalihusu uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi, 98 (asilimia 5) yalihusu ukaidi, 66 (asilimia 3.4) yalihusu ulevi huku 16 (asilimia 0.8) yalihusu ubadhirifu na 31 (asilimia 1.6) yalihusu makosa mengineyo. Alisema katika mashauri 1,642 yaliyoamriwa na tume hiyo, walimu 919 sawa na asilimia 56 ya adhabu zilizotelewa, walifukuzwa kazi.

Kamishna wa tume hiyo, Jane Mtindya anasema hatua hiyo ya kufanya utafiti, ni ya msingi kwani hata miaka ya nyuma walishaagiza ufanyike.

Alisema utafiti huo ulibaini kuwa walimu waliozaliwa miaka ya 1990 waliamua kusomea kada ya ualimu kwa lengo la kupata mikopo ya elimu ya juu iliyokuwa ikitolewa na Serikali na sio kusukumwa na wito wa kusomea taaluma hiyo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, (Udom) Dk Paul Loisulie anasema ni vizuri kufanya utafiti ili kuona ni nini hasa kinasababisha walimu wengi wa miaka hiyo kukutwa na makosa ya nidhamu.

Hata hivyo, alishauri kuwa ni vizuri kupanua wigo wa watakaoshiriki kwenye utafiti huo na kuwa itafaa kuwatumia pia wale waliozaliwa miaka ya nyuma ili kufanya mlinganisho mzuri.

“Lakini ni vizuri pia kutazama tabia za makundi ya vizazi zilizoonekana kwenye mitandao wakati wa maandamano ya Gen Z kule Kenya,”anasema.

Anasema inawezekana hali hiyo ya walimu hao inatokana na umri wao, kwani huo ndio muda wao wa harakati kubwa za kujipanga kimaisha, akisema ni umri wa kujitafuta.

Anasema katika harakati za kujitafuta, huenda wakajikuta wakifanya shughuli nyingine nyingi nje ya ualimu zinazoweza kuwaingiza matatizoni.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Kirumo wilayani Bagamoyo, Sara Gilla anasema katika umri huo walimu wanakuwa na majukumu mengi lakini kipato chao bado kidogo, hali inyowafanya kuwa na msongo mwingi wa mawazo.

Unakuta anahangaika kutafuta kipato kingine, akiangalia nyumbani ana majukumu, nyumbani, wazazi na watoto wanamuangalia. Akiangalia kila kitu kinamuangalia mwenyewe hapo lazima stress (msongo wa mawazo) unakuwepo,”anasema.

Anasema kwa kuangalia mwalimu kama huyo anaweza kufanya chochote kile na hata wakati mwingine ukamuuliza swali anaweza kukujibu vingine kwa kuwa kichwa chake kina mambo mengi.

Anasema ukiangalia walimu wengi katika umri huo, ni wale waliotoka katika familia ambazo hazina kipato cha kutosha, hivyo zinawategemea watoto wao hao katika kutatua changamoto mbalimbali.

“Wengine vituo vya kazi hawaendi vizuri na wakuu wao. Mwalimu akienda kazini anaona kwa moto. Anaweza kuwa na matatizo mwalimu mkuu hamsikilizi. Lakini akirudi nyumbani anakutana na changamoto za kifamilia,”anasema.

Kuhusu nini kifanyike kunusuru walimu hao, Sara anasema kwanza Serikali imuangalie mwalimu kwa kuhakikisha kuwa inamuongezea kipato, kupandishwa madaraja na stahiki kwa wakati pamoja na walimu kujengewa nyumba za kuishi kwa kuwa wengine wanakaa nyumba za shule zisizoeleweka. “Kifupi Serikali ingeboresha mazingira ya mwalimu, kwa hali zote ikiwemo makazi na kipato. Hii ingesaidia kumrudisha mwalimu katika kwenye standard (viwango) vyake,”anasema.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Bakari Mtembo anasema ukiachana na fani ya ualimu, unapokuja katika maisha ya kawaida ya mtaani wavunjaji wa maadili wengi wanatokana na watu wenye umri huo.

“Kama kizazi hicho ndicho chenye mwenendo wa kuvunja maadili hayo kwa kiwango kikubwa, kwa hiyo tafsiri yake hata wale walioingia katika fani mbalimbali wako hivyo. Bahati nzuri TSC wameamua kufanya tathimini hiyo lakini hata ukiamua kuifanya katika kada nyingine utakuta changamoto nyingi zinakuwa kwa rika hilo,”anasema.

Mtembo anasema kosa si walimu bali kizazi cha umri huo ndio kimekuwa kikituhumiwa kuharibu sana misingi ya maadili ya Kitanzania na ya kibinadamu.

Anasema ili kukabiliana na changamoto hiyo, maadili yaendelee kuboreshwa kupitia viongozi wa dini, kwa njia za mila na desturi.

Anasema zamani ilikuwa inachukua muda mrefu kugundua kwamba mtu anavuta bangi kwa sababu watu walikuwa wakifanya kwa vificho lakini sasa hivi watu wanatoka hadharani.

Anatoa mfano wa matukio ya udhalilishaji ambayo watu wanafanya na kujirikodi na kutuma katika mitandao ya jamii, ambayo kwa miaka ya nyuma watu walikuwa wakiyafanya kwa usiri mkubwa.

“Lakini hivi sasa vijana wameamua kufanya mambo hayo hadharani, kujirekodi na kurusha mtandaoni. Lakini kada nyingine hazijaamua tu kufanya tathimini na kuweka wazi, kama wangefanya hivyo tungebaini ni rika hilo hilo,”anasema..

Naye mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St John, Dk Shadidu Ndossa anasema Dk Ndossa anasema sio kitu kizuri kusikia kuwa baadhi ya walimu, wamekuwa watovu wa nidhamu kwa sababu wao ndio kiwanda cha kutengeneza rasilimali watu.

“Hivyo wanapokuwa, wanaonekana kuwa ni watovu wa nidhamu, wana matatizo, hawafanyi kazi zao sawasawa inatia wasiwasi kuwa future (mustakabali) wa Taifa iko kwenye shaka,”anasema.

Anaeleza kuwa huo ni umri wa ujana, hivyo inawezekana makosa hayo yanasababishwa na kukosekana kwa uzoefu wa kutosha katika kazi yao.

“Kila aina ya kosa ina sababu yake na jinsi ya kukabiliana nayo. Kwa mfano, kutoingia darasani inatofautiana na makosa ya kukosa uaminifu kama kutumia vibaya mali za taasisi,”anasema.

Anasema moja ya njia ya kudhibiti makosa hayo ni walimu kupewa mafunzo ya mara kwa mara kuhusiana na utumishi wa umma, masuala ya maadili au uhifadhi wa siri za taasisi.

Dk Ndossa anasema bahati mbaya walimu wengi wamekosa mafunzo kwa muda mrefu hasa wale wanaotoka maeneo ya pembezoni.

Kwa upande wa utoro, anasema hilo linaweza kuchangiwa na mwalimu kuwa na shughuli nyingine ya kumuongezea kipato kama biashara au shughuli za kilimo.

“Mara nyingi ukizungumza na walimu wanazungumzia changamoto ya maslahi madogo. Kama watajiridhisha kuwa changamoto ni maslahi, solution (suluhisho) ni kuwaongezea maslahi kazini. Japokuwa mshahara hauwezi kukidhi kila kitu, lakini uwe mshahara ambao unafanya kazi ya ualimu inaonekana ni kazi ya staha,”anasema.

Related Posts