Dar es Salaam. Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (Costech) imezindua rasmi programu mbili za Future Femtech na Kuza Femtech ambazo zinalenga kuwasaidia wasichana kitaaluma na kiteknolojia.
Programu hizo zimezinduliwa leo Septemba 10, 2024 Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Amos Nungu kwa lengo la kuwainua wasichana ili waweze kuendesha maisha yao na jamii kwa jumla.
Future Femtech ni programu maalumu kwa wasichana ambao ni waanzilishi wa kampuni changa ikiwa lengo la kuwasaidia kitaaluma na kuwapata mafunzo elekezi, kuwajengea uwezo na pia kuwapatia fedha kuwezesha biashara zao.
Kuza Femtech ni programu maalumu kwa wasichana ambao walishindwa kuendelea na masomo yao kwa sababu mbalimbali.
Programu hii ni mahsusi kwa wasichana wenye umri wa miaka 15 – 20, lengo likiwa ni kutoa ujuzi na taaluma ya kiteknolojia.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Dk Nungu amesema kutokana na utafiti uliofanywa mwaka 2023, vijana zaidi ya 180 waliomba kushiriki katika programu hiyo huku kukiwa na idadi ndogo ya wasichana.
“Mwitikio kwa wasichana umekuwa ni mdogo kwa kuogopa ushindani, hivyo tumezindua programu hizi maalumu ili mabinti waweze kupata mafunzo ya kidigitali,” amesema.
Amesema vijana zaidi ya 180 walipata mafunzo ya ujasiriamali, sayansi na teknolojia ambapo vijana hao waligawanywa katika makundi na kuanza kushindanishwa.
Dk Nungu amesema washindi wa makundi matano ya mwanzo walipewa Sh50 milioni kwa kutekeleza ubunifu ulioshindanishwa na makundi mengine.
Meneja wa Usimamizi na Uboreshaji kutoka Costech, Erasto Mlyuka amesema lengo la programu hiyo ni kutoa ujuzi na taaluma ya kiteknolojia ili wasichana waweze kubuni biashara zitakazoweza kuwasaidia kuendesha maisha na kusaidia jamii.
“Tunataka kutengeneza ajira kwa wanawake ili waweze kupata nafasi ya kuchangia kwenye pato la Taifa na kuwawezesha kupata kipato ambacho ni halali,”amesema.
Pamela Chogo ambaye ni mbunifu kutoka Arusha, pia, ni mnufaikaji wa programu ya Future Femtech.
Chogo amesema programu kama hizo ni muhimu kwa kuwa ni fursa kwa watoto wa kike na zinatoa elimu ya namna ya kufanya ujasiriamali na bunifu mbalimbali.
“Nimefanikiwa kushiriki mwaka jana na kupata mafunzo ambayo yalileta chachu kubwa katika biashara zangu na mambo ya ubunifu,” amesema Chogo.
Mnufaikaji huyo amesema anajihusisha na utoaji elimu kupitia mitandao, pia, anatengeneza mifumo mbalimbali ya kidigitali ambayo inahusika na utoaji wa elimu.