WASHAMBULIAJI Wazir Junior, Clement Mzize na Cyprian Kachwele wana jukumu kubwa la kuiongoza safu ya ushambuliaji ya Taifa Stars katika mchezo wa leo dhidi ya Guinea utakaochezwa Uwanja wa Charles Konan Banny uliopo Yamoussoukro nchini Ivory Coast.
Guinea ambayo imeamua kutumia uwanja huo kwa mechi zake za nyumbani baada ya nchini kwao kukosa kiwanja chenye sifa kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), leo itaingia uwanjani ikiwa imetoka kufungwa 1-0 ugenini dhidi ya DR Congo katika mchezo uliopigwa Ijumaa iliyopita pale Stade des Martyrs, Kinshasa nchini DR Congo.
Stars yenyewe leo nayo ni mechi ya pili katika Kundi H kuwania kufuzu michuano ya Afcon 2025 baada ya kuanza na suluhu nyumbani dhidi ya Ethiopia.
Rekodi zinaonyesha kwamba, Guinea imepoteza mechi mbili mfululizo kwa matokeo ya 1-0, kabla ya hapo ilikuwa imeshinda mechi tatu mfululizo kwa matokeo ya jumla kuwa 13-2 ikiwa ni kipindi cha mwezi Machi na Juni mwaka huu, hivyo mchezo wa leo wataingia kwa hasira kubwa kuirekebisha rekodi yao mbovu.
Kwa upande wa Taifa Stars ambayo inaisaka Afcon ya nne tangu mwaka 1980, nayo haipo kinyonge kwani inatambua kwamba kushindwa kuondoka na pointi tatu leo itawaweka katika mazingira magumu ya kufuzu kwani hivi sasa ina pointi moja.
Stars ina kazi kubwa ya kufanya katika mchezo wa leo kwani tangu kuingia kwa mwaka 2024, imeshinda mechi tatu pekee kati ya 11 za kimashindano na kirafiki huku timu ikifunga mabao saba kupitia washambuliaji wanne, Kelvin John, Wazir Junior, Oscar Adam na Ibrahim Hamad Hilika, wakati Simon Msuva ambaye ni kiungo mshambuliaji kama ilivyo kwa Abdul Suleiman Sopu kila mmoja akifunga moja sawa na beki Novatus Dismas.
Mchezo uliopita dhidi ya Ethiopia uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Stars ilifanya mashambulizi mengi kuzidi wapinzani wake lakini haikuambulia bao.
Ndani ya dakika tisini za mchezo huo, Stars ilipiga jumla ya mashuti 9 dhidi ya 8 ya Ethiopia, huku mawili yakilenga goli la wapinzani ambao wenyewe hakuna hata moja lililolenga goli.
Hali hiyo inaonyesha kwamba Stars katika kufanya mashambulizi haina shida lakini suala la kufunga ndiyo kuna tatizo kitu ambacho benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Hemed Morocco linapaswa kulifanyia kazi na leo mabadiliko yawepo.
IKumbukwe kwamba, katika mchezo wa mwisho ambao Stars ilishinda ugenini 1-0 dhidi ya Zambia ikiwa ni kufuzu Kombe la Dunia 2026, Wazir Junior ndiye aliyefunga bao hilo pekee mapema tu dakika ya tano akimalizia pasi ya kiungo Mudathir Yahya.
Wakati Stars ikiwa inajiuliza katika hilo la ushambuliaji, safu ya ulinzi ya kikosi hicho imeonekana kuwa imara kwa kiasi chake kwani katika mechi hizo 11, imefanikiwa kuondoka na clean sheet sita lakini kwa jumla imeruhusu mabao tisa.
Hayo yote yakijiri, mchezo wa leo unazikutanisha timu ambazo mara ya mwisho kukutana ilikuwa Janauri 27, 2021 kwenye michuano ya Chan 2020 iliyofanyika nchini Cameroon ambapo zilikuwa Kundi D na matokeo kuwa sare ya mabao 2-2.
Ukiangalia kikosi cha mwisho ambacho Stars kilicheza dhidi ya Guinea, ni Bakari Mwamnyeto na Feisal Salum pekee wapo tena leo, waliobaki hadi Kocha Etienne Ndayiragije hawapo.
Kocha Hemed Morocco akiuzungumzia mchezo wa leo, amesema anafahamu itakuwa ngumu kucheza ugenini kwani wenyeji watataka kushinda, hivyo amewaandaa vijana wake kukabiliana na hali zote.
Morocco ameongeza kwamba suala la kutengeneza nafasi ni jambo moja na kuzitumia jambo lingine lakini anaamini katika mchezo wa leo watazitumia vizuri nafasi hizo kwani wameendelea kuifanyia kazi ishu hiyo.
“Katika mechi hizi za kimashindano hakuna kumdharau mpinzani, lakini ukiangalia katika kikosi chetu kuna wachezaji ambao walikuwepo katika Afcon iliyopita ingawa wapo pia vijana wanaochipukia.
“Tunaamini kwa maandalizi tuliyoyafanya tunaweza kupata matokeo mazuri tukiwa ugenini licha ya kwamba tufahamu mchezo utakuwa mgumu,” alisema Morocco.
Katika mechi za kufuzu Afcon 2025 michuano itakayofanyika Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026 nchini Morocco ikizihusisha timu 24, Stars ipo Kundi H na Guinea sambamba na DR Congo na Ethiopia waliopambana jana usiku Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kabla ya mchezo wa jana, DR Congo ilikuwa kileleni mwa msimamo wa Kundi H ikikusanya pointi tatu zilizotokana na kushinda mechi ya kwanza nyumbani dhidi ya Guinea, wakati Ethiopia ikiwa na moja iliyoipata mbele ya Stars. Guinea yenyewe haina kitu.