Tanga. Familia ya aliyekuwa mjumbe wa sekretarieti ya Chadema, Ali Kibao imeiomba Serikali kuharakisha uchunguzi wa kifo kada huyo na ipewe taarifa ya kinachoendelea.
Kibao aliuawa baada ya kutekwa na watu wenye silaha, jioni ya Ijumaa ya Septemba 6, 2024 eneo la Kibo Complex, Tegeta jijini Dar es Salaam akiwa ndani ya basi la Kampuni ya Tashriff kwenda mkoani Tanga.
Baada ya kuondoka naye akiwa amefungwa pingu, mwili wake uliokotwa eneo la Ununio, Dar es Salaam ukiwa na majeraha na inaelezwa alimwagiwa tindikali usoni.
Mwili wake ulizikwa jana Jumatatu, Septemba 9, 2024 katika Kijiji cha Tarigube, Kata ya Togoni na kuhudhuriwa na waombolezaji mbalimbali akiwamo Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni.
Leo Jumanne, Septemba 10, 2024, Waziri Masauni amefika nyumbani kwa Kibao kutoa mkono wa pole kwa niaba ya Serikali na kukabidhi rambirambi ya Sh5 milioni na kuzungumza na familia.
Akizungumza mbele ya Waziri Masauni kwa niaba ya familia, Mariam ambaye ni mtoto wa marehemu Kibao ameiomba Serikali kufanya uchunguzi wa kifo cha baba yao huku akiomba familia iwe inapatiwa taarifa za uchunguzi huo.
Amesema isipite muda mrefu bila matokeo ya uchunguzi kutoka huku akiomba majibu ya uchunguzi yawafikie familia kwa njia rasmi na sio kusikia kupitia vyombo vya habari.
“Tumesikia Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza vyombo vya uchunguzi vifanye uchunguzi wa kifo cha baba yetu, sisi kama familia tutakuwa tunapataje taarifa za uchunguzi huo, najua kuna muda inakuwa ni vigumu kuwafikia viongozi wa juu huko serikalini hasa kwa kesi kama hii ni jambo nzito.
Tunachoomba ni ushirikiano wenu kama Serikali kwetu sisi maana hata sisi hatujui nani amefanya huo utekaji na mauaji ya baba yetu. Muhimu tunaomba huo uchunguzi ufanyike kwa haraka ili ukweli ujulikane na haki ipate kutendeka,” amesema Mariam.
Kwa upande wake, Waziri Masauni amewasilisha salamu za pole kutoka kwa Rais Samia na ameiomba familia hiyo kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho wamempoteza mpendwa wao huku akiwaomba wawe na subira ili vyombo husika vikiendelea na uchunguzi wa tukio hilo la kutekwa na kuuawa kwa mzazi wao.
“Mheshimiwa Rais amesikitishwa na kusononeshwa sana na tukio hili pamoja na Serikali nzima tumesikitika sana, ni jambo ambalo halikupaswa kutokea hasa katika nchi ambayo imekua inatajwa kuwa na amani.
“Maelekezo ya Rais yashaanza kutekelezwa ili kubaini chanzo cha tukio hili, Serikali yenu iko pamoja na ninyi, nchi hii inaendeshwa kwa mujibu wa sheria, kwa hiyo kila mtu ana haki ya kuishi, niwaombe sana muwe na mola wa subira tumuombe Mwenyezi Mungu aijalie safari ya marehemu wetu iwe nyepesi na sisi tumuombe Mungu mwisho mwema,” amesema Masauni.
Waziri Masauni ameongozana na Meya wa Jiji la Tanga, Abdulrahman Shiloow na Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mjini, Japhari Kubecha. Marehemu Ali Kibao ameacha wajane wawili na watoto kumi.