KESHO, Jumatano, historia inaandikwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo mjini Babati, mkoani Manyara, wakati Fountain Gate FC ikiikaribisha KenGold.
Huo utakuwa ni mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara kuchezwa mkoani humo ikiwa ni historia kwa wananchi wa eneo hilo kuanza kushuhudia mechi za Ligi Kuu.
Manyara yenye wilaya tano za Kiteto, Simanjiro, Mbulu, Babati, Kiteto na Hanang’ tangu ilipotengwa kutoka Mkoa wa Arusha 2002 haijawahi kushuhudia mchezo wowote wa Ligi Kuu Bara ukichezwa katika ardhi hiyo.
Licha ya kuwa na utajiri wa madini ya Tanzanite na vivutio vya utalii kama Hifadhi ya Tarangire, Mlima Hanang’, Mlima Kwaraa, Ziwa Babati na maeneo mengine, lakini kisoka bado iko nyuma.
Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo mjini Babati umechaguliwa na timu za Fountain Gate na Dodoma Jiji kutoka Dodoma kwa michezo ya nyumbani msimu huu.
Gerald Mtui, mwenyekiti wa Chama Cha Soka Wilaya ya Babati (BDFA), alisema mechi za Ligi Kuu ni furaha kubwa kuchezwa mkoani humo kwani anaamini zitarudisha hamasa ya soka ambayo imepotea.
“Kwetu hii ni sehemu ya historia lakini pia ni sehemu ya burudani kwa wadau wa michezo hapa Babati ambao walikuwa wanatamani siku moja mechi za Ligi Kuu zichezwe hapa kwetu,” alisema Mtui.
Alisema mechi za ligi kupigwa Babati ni fursa ya kimaendeleo kwa wafanyabiashara mbalimbali lakini pia ni chachu kwao kama FA Wilaya kuwasihi wadau kuweka nguvu za timu zao ambazo zinashiriki Ligi Daraja la Tatu Mkoa.
Kwa upande wake mchezaji wa zamani wa Usalama FC ya Babati ambayo iliwahi kushiriki Ligi Daraja la Pili (First League), Keneth Makotha amezipongeza timu za Fountain Gate na Dodoma Jiji kuuchagua Uwanja wa Tanzanite Kwaraa kwa mechi zao za nyumbani.
Alisema kama wadau watazipa sapoti timu ambazo zimewakata kiu ya kukaa miaka 22 bila kuona mechi za Ligi Kuu zikipigwa Manyara.
Kocha wa Fountain Gate, Mohamed Muya alisema wanaridhishwa na sapoti kubwa ambayo wanaendelea kuipata kutoka kwa wakazi kwa Babati na Mkoa wa Manyara kwa ujumla.