Hatima kesi ya Kabendera leo

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam leo Jumanne, Septemba 10, 2024 inatarajiwa kutoa uamuzi wa pingamizi la awali lililowekwa na kampuni ya huduma za mawasiliano kwa simu za mkononi ya Vodacom Tanzania Public Limited katika kesi iliyofunguliwa dhidi yake na Mwanahabari, Erick Kabendera.

Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa na Jaji mfawidhi wa Mahakama hiyo, Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo ya pingamizi la awali lililowekwa na Vodacom ikiiomba Mahakama hiyo isiisikilize, badala yake iifute.

Kabendera alitiwa mbaroni na askari polisi nyumbani kwake Julai 29, 2019 na kushikiliwa kwa siku kadhaa, kisha  akafunguliwa kesi ya uhujumu uchumi.

Kesi hiyo ilimalizika kwa utaratibu wa majadiliano na makubaliano ya kukiri makosa baina yake na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) unaojulikana kisheria kama plea bargaining.

Aliachiliwa huru Februari 24, 2020 baada ya kulipa fidia na faini aliyoamuriwa na Mahakama baada ya kumtia hatiani kwa kukiri makosa yake kulingana na majadiliano na makubaliano hayo na DPP.

Miaka minne baada ya kesi yake hiyo kumalizika, Kabendera  ameifungulia kesi Vodacom akiituhumu kufanikishwa kukamatwa kwake na askari polisi, tukio analoliita kutekwa,  kisha kufunguliwa kesi hiyo ya uhujumu uchumi.

Katika kesi hiyo ya madai namba 12799/2024, Kabendera anayewakilishwa na Wakili Peter Madeleka anadai kutokana na tukio hilo amepata madhara mbalimbali.

Anayataja madhara hayo ni ya kiuchumi na yasiyo ya kiuchumi, ya kijamii, maumivu ya kiakili na kimaono, ya kutokufurahia maisha, hasara ya maendeleo binafsi na hadhi yake katika jamii na kutoaminiwa kitaaluma.

Hivyo , anaitaka kampuni hiyo imlipe kiasi hicho cha pesa, Dola 10 milioni za Marekani (Sh28 bilioni) kama fidia ya hasara halisi na riba kwa kiwango cha Mahakama (asilimi) kuanzia tarehe ya hukumu mpaka kumaliza malipo yote.

Pia, anataka alipwe fidia ya hasara ya jumla kadri Mahakama itakavyotathmini, gharama za kesi na nafuu nyingine kadri itakavyona inafaa.

Hata hivyo, Vodacom kupitia wakili wake Aspar Nyika, Julai 9, 2024  iliwasilisha mahakamani maelezo yake ya utetezi wa maandishi sambamba na pingamizi la awali.

Katika maelezo hayo ya utetezi ambayo Mwananchi limeiona nakala yake kampuni hiyo inakana tuhuma zote zilizotelekezwa kwake na mwanahabari huyo kuhusu ushiriki wake kufanikisha kukamatwa kwake anakoita kutekwa.

Badala yake, kampuni hiyo imemtaka mwanahabari Kabendera kuthibitisha tuhuma hizo dhidi yake.

Katika pingamizi lake, kampuni hiyo inaiomba Mahakama hiyo iitupilie mbali kesi hiyo bila kuisikiliza ikidai kuwa haina mamlaka ya kuisikiliza kwa madai kuwa imefunguliwa nje ya muda uliowekwa kisheria.

Jaji Maghimbi aliamuru pingamizi hilo lisikilkzwe kwa njia ya maandishi na baada ya kukamilisha usikilizwaji huo ndipo akapanga kulitolea uamuzi leo.

Uamuzi huo ndio utakaotoa hatima ya uhalali wa kesi hiyo kuendelea kuwepo mahakamani hapo na kusikilizwa kwake, madai ya msingi ya Kabendera.

Ikiwa Mahakama katika uamuzi wake itakubaliana na pingamizi hilo la Vodacom, itaifutilia mbali kesi hiyo na huo ndio utakuwa mwisho wa kesi hiyo isipokuwa kama Kabendera atakata rufaa Mahakama ya Rufani na ikaamua vinginevyo.

Lakini kama Mahakama itatupilia mbali pingamizi hilo,  kesi ya msingi itaendelea na usikilizwaji na baadaye kuamua kama Kabendera atakuwa amethibitisha madai yake dhidi ya kampuni hiyo au la, kisha itatoa amri kulinga na uamuzi huo utakavyokuwa.

Simulizi ya kutekwa kwa Kabendera

Kwa mujibu wa hati ya madai katika kesi hiyo Kabendera ameeleza matukio yaliyojiri katika simu yake kabla ya tukio la kukamatwa kwake, kuwa ilianza kupoteza mawasiliano na kumfanya ashindwe kupata huduma ya mawasiliano.

Pia, ameelezea juhudi alizofanya kujua chanzo cha hali hiyo kwa  kufanya mawasiliano na mwakilishi wa huduma kwa wateja na hata kutembelea ofisi za kampuni hiyo lakini hakupata ufumbuzi wa tatizo hilo.

Kwa mujibu wa hati hiyo ya madai, hali hiyo ilianza Julai 27, 2019, saa 9:00 alasiri alipoiwasha simu yake aliyokuwa ameizima tangu jana yake usiku na kwamba ndipo alipobaimi haikuwa na mtandao.

Hivyo, aliazima simu nyingine akampigia mtoa huduma kwa mteja kujua mazingira yaliyosababisha kumkatia huduma katika simu yake bila kumjulisha kwanza.

Mwakilishi wa huduma kwa wateja wa Vodacom alimweleza namba yake ya simu ya Vodacom (+255767456796) ilikuwa na changamoto za kiufundi iliyomhitaji kutoa taarifa katika kituo cha huduma kwa wateja cha karibu kilichopo Tegeta.

Kabendera alimtaka mwakilishi huyo kuelezea tatizo ni nini kabla ya kwenda huko kituoni, lakini mwakilishi huyo alikataa  akidai kuwa ni suala nyeti ambalo linamtaka aende binafsi kituoni hapo.

“Hata hivyo (Kabendera alisita kwenda huko kituo cha huduma kwa wateja) kwa kuwa kulikuwa kuna matukio kadhaa ya watu kutekwa ama kutiwa mbaroni walipokuwa wakitembelea kituo cha huduma kwa wateja tangu mwaka 2016,” inasomeka sehemu nyingine ya hati hiyo na kuongeza:

Inaendelea kueleza Jumatatu, Julai 29, 2019 saa 4:00 asubuhi Kabendera alipiga tena simu ya huduma kwa wateja akilalamikia kuwa alikuwa akihitaji kutoa pesa kwenye simu yake hiyo kwa ajili ya kumnunulia dawa mama yake aliyekuwa mgonjwa.

Mwakilishi wa Vodacom aliyemhudumia alimweleza asubiri kidogo ili amuulize meneja wake na alirejea dakika chache baadaye na kumweleza kuwa kesi yake ilikuwa nyeti na kwamba ilikuwa juu ya uwezo wao kuitatua.

Badala yake walimshauri atembelee ofisi zao zilizoko Mlimani City, Dar es Salaam asubuhi hiyo.

Hata hivyo, saa 9:00 alasiri siku hiyohiyo ya Julai 29, ghafla tu simu yake ilianza kufanya kazi, kisha alipopigiwa simu na mwakilishi wa Vodacom ambaye alimtaka (Kabendera) amwelezee tatizo lake na baada ya Kabendera kumuelezea kwa takribani dakika tatu, alikata simu akiahidi kumpigia baadaye kidogo.

Baada ya takribani dakika tatu Kabendera alipokea simu iliyopigwa kutoka huduma kwa wateja Vodacom aliyoipokea akabaini ilikuwa ni sauti ya mwanamume, aliyemtaka Kabendera aeleze mahali alikokuwa na kwamba simu hiyo ilikuwa ikihanikiza na kukwaruza kama vile ilikuwa inarekodiwa.

“Kabla ya simu hiyo kukatwa mteja wetu alimsikia huyo aliyempigia simu hiyo akinong’ona kuwa alikuwa nyumbani kwake na kuongeza sogea karibu na nyumba yake,” inasomeka sehemu nyingine ya hati hiyo ya madai.

Kwa mujibu wa hati hiyo, maelezo hayo yalimstua Kabendera na akakimbia sehemu ya juu ya nyumba yake ambako aliweza kuona magari kadhaa ambayo hakuyafahamu, karibu ya nyumba yake, kisha lilitokea gari lingine aina ya Toyota Alphard lililoegesha mbele ya magari hayo upande wa kulia mwa nyumba yake.

Wakashuka watu wanne waliojitambulisha kuwa maofisa wa polisi lakini walikataa kutoa utambulisho.

Walimfunga pingu na kumshikilia kizuizini kwa siku mbili.

Hati hiyo inaendelea kueleza wakati wa mahojiano, maofisa wa polisi walifika katika chumba cha mahojiano wakiwa na karatasi zilizochapishwa kutoka katika kompyuta za akaunti ya pesa ya simu na za namba simu alizokuwa amezipiga kwa mwaka mzima.

Hivyo walimhoji lengo la kila muamala alioufanya kwa mwaka mzima nyuma yake na pia walimhoji uhusiano wake na watu aliokuwa amewasiliana nao miaka kadhaa.

Kabendera analalamika polisi na Serikali walitoa taarifa kadhaa zenye mgogoro kwa umma kuhusiana na ‘kutekwa’ kwake na kwamba walimtuhumu kwa kutokuwa raia na kumkashfu Rais (wa wakati huo) John Magufuli.

“Hatimaye alishtakiwa mahakamani kwa makosa ya utakatishaji fedha, uhujumu uchumi na ukwepaji kodi na matokeo yake walimuweka chini ya ulinzi mkali katika mahabusu ya gereza la Segerea,” inasomeka hati hiyo ya madai.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa zaidi

Related Posts