Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori wapewa mizinga 300

Mradi wa Kupambana na Ujangili na Biashara Haramu ya Wanyamapori (IWT) ulio chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, umekabidhi mizinga ya kisasa 300, vifaa mbalimbali vya kufugia nyuki na kusindika asali vyenye gharama ya shilingi milioni 50 kwa Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori (WAGA).

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) ameyasema hayo leo Septemba 10,2024 katika hafla ya makabidhiano ya mizinga hiyo iliyofanyika Wilaya ya Mafinga, Mkoani Iringa.

“Endapo WAGA watashiriki na kutumia vyema mafunzo yatakayotolewa na wataalamu, mizinga hiyo itaweza kuzalisha asali wastani wa tani 10 zitakazokuwa na thamani ya shilingi milioni 150 kwa mwaka” amesisitiza.

Ametoa rai kwa Jumuiya ya WAGA kutunza na kutumia ipasavyo mizinga na vifaa hivyo viweze kuleta matokeo chanya.

Katika hatua nyingine Mhe. Chana amefafanua kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii inakuja na Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Ufugaji Nyuki unaohusisha programu maalum ya kuwezesha vijana na wanawake kuzalisha na kufanya biashara ya mazao ya nyuki.

“Mpango huu utachangia kuongeza kiwango cha uzalishaji wa asali kutoka tani 32,000 hadi kufikia tani 185,379 kwa mwaka, kuongeza kiwango cha asali kinachouzwa nje ya nchi kutoka asilimia 5 hadi 30, kuongeza fedha za kigeni kutoka dola milioni 8 hadi dola milioni 20 kwa mwaka” amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu,Wizara ya Maliasili na Utalii, Mkuruganzi wa Misitu na Nyuki, Bw. Deusdedit Bwoyo amesema kuwa makabidhiano ya mizinga hiyo ni sehemu ya mpango wa kuwezesha jamii zinazozunguka hifadhi kwenye mfumo wa ikolojia ya Ruaha – Rungwa kujikimu ili kupunguza utegemezi wa maliasili.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 mradi utawezesha miradi yenye thamani ya shilingi milioni 337 kwa vikundi 21 vya ufugaji nyuki na kilimo katika Wilaya za Itigi, Mbarali na Mufindi.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali pamoja na wadau wa Sekta ya Nyuki pamoja na Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.

Related Posts