BAADA ya kikosi chake kupata nafasi ya kupachika bao moja kwenye sare ya 1-1 dhidi ya Geita Gold, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Paul Nkata ameuona mwanga kwenye safu ya ushambuliaji kabla ya kuikabili Tabora United.
Kesho Jumatano, Kagera Sugar itakuwa ugenini kuikabili Tabora United kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi mbili za mwanzo nyumbani dhidi ya Singida Black Star 1-0 na kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Yanga.
Akizungumza na Mwanaspoti, Nkata alisema ana kikosi kizuri ambacho kipo imara lakini shida iliyopo ni namna ya kutumia nafasi huku akikiri kuwa mchezo dhidi ya Geita Gold inayoshiriki Championship umempa mwanga.
“Kwenye mechi zote mbili tulizopoteza sio kwamba tulikuwa tunazidiwa sana, ukiangalia umiliki wa mpira kwa timu yangu ni mzuri na ni wapambanaji lakini shida ni kwenye kutengeneza nafasi tatizo ambalo naendelea kulifanyia kazi na naamini nikifanikiwa nitakuwa na timu nzuri,” alisema na kuongeza.
“Kitendo cha kufika lango la wapinzani wetu na kufanikiwa kufunga bao ni mwanzo mzuri na naamini wachezaji wangu wakiendelea kufanya hivyo tutaweza kufikia malengo kuelekea mchezo wa Jumatano ambao tutaingia kwa kuwaheshimu wapinzani na kutekeleza mipango yetu.”
Nkata ambaye huu ni msimu wake wa kwanza kuinoa Kagera Sugar, ameizungumzia ligi kwa ujumla akisema anatarajia ushindani mkubwa kutoka kwa timu zote na mwanzo wake licha ya kutokuwa mzuri ana imani kubwa na kikosi chake.
“Ligi itakuwa bora zaidi ya msimu uliopita, hilo lipowazi, hii ni kutokana na namna timu zilivyojipanga na kusawazisha mapungufu yao na sasa wamewekeza nguvu kuhakikisha hawarudii makosa,” alisema kocha huyo raia wa Uganda na kubainisha kwamba kutokana na ugumu huo atahakikisha anaimarisha timu yake ili kutoa ushindani.