Majaliwa ataja mbinu kuwafichua waharibifu wa mazingira

Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wadau kuwafichua wanaofanya shughuli zinazoharibu mazingira kwa kuwaripoti kwenye mamlaka zilizo karibu ili kuisaidia Serikali kuwachukulia hatua.

Majaliwa amesema hayo leo Jumanne, Septemba 10, 2024 alipofunga mkutano maalumu wa viongozi, wataalamu na wadau kuhusu mwenendo wa hali ya mazingira nchini.

Majaliwa amemtaka kila mdau kufuatilia mwenendo wa mazingira nchini na kutoa taarifa kwenye mamlaka za eneo husika, mahali anapooona kuna uharibifu.

Amesema kwa kufanya hivyo kutasaidia Serikali kuhoji kwa nini kunafanyika shughuli inayoharibu mazingira.

“Hii itasaidia sana katika kutambua matatizo tuliyonayo, namna ya kukabiliana nayo lakini pia na utatuzi wake,” amesema Majaliwa.

Ametaka pia kuongeza ushirikiano miongoni mwao katika kulinda mazingira waliyonayo na elimu kwa jamii juu ya mazingira.

Majaliwa amewataka pia kuzingatia usafi wa mazingira kwenye maeneo yao kwa halmashauri kusimamia hilo na kuweka mpango wa wazi kwa baraza la madiwani hadi ngazi ya chini ya vitongoji.

 “Wizara itafute namna nzuri ya kukutanisha wadau wa mazingira na itengeneze maonyesho yatakayowaleta pamoja Watanzania wengi kuja kujifunza kwa wiki nzima ama wiki mbili. Ni muhimu Watanzania wajue umuhimu wa uhifadhi wa mazingira,” amesema.

Amewataka kuhamasisha matumizi ya sheria na kanuni zilizopo zisaidie katika kukinga uharibifu wa mazingira.

Akisoma maazimio ya mkutano huo ulioanza jana Jumatatu, Mbunge wa Kuteuliwa (CCM), Dk Bashiru Ally amesema wadau hao wameazimia kufanyike kwa marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ili kujumuisha masuala ya masuala ya biashara ya hewa ukaa.

“Kuifanyia marekebisho Sheria ya Mazingira ili kujumuisha masuala ya biashara ya hewa ukaa na kuifanya NEMC (Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira) kuwa mamlaka kamili,” amesema.

Dk Bashiru amesema Sheria ya Ugatuzi wa Madaraka iimarishwe kwa kutumia mbinu bunifu za upatikanaji wa rasilimali fedha na kujenga uwezo wa jamii katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira.

“Kuimarisha muundo wa ugatuzi wa madaraka katika ngazi zote kwa kuhakikisha unazingatia mahitaji ya usimamizi wa mazingira kulingana na matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ikiwamo uanzishaji wa vitengo vya mazingira katika wizara, taasisi za umma na sekta binafsi  na kamati za mazingira katika mitaana vijiji,” amesema Dk Bashiru.

Amesema, pia idara ya mazingira katika mamlaka ya Serikali za mitaa irejeshwe na kupewa hadhi stahiki ili kuimarisha utendaji na uhifadhi katika mazingira.

Dk Bashiru amesema wameazimia kufanya mapitio ya sheria ili kuhuisha sheria zinazokinzana katika uhifadhi wa mazingira ikiwamo Sheria ya Misitu inayotambua mkaa kama chanzo cha mapato.

Amesema sheria hiyo inakinzana na malengo ya uhifadhi wa misitu na jitihada za upandaji wa miti.

Dk Bashiru amesema wameazimia kuwekwa kwa mazingira wezeshi ikiwamo kutoa ruzuku, yatakayohakikisha gharama nafuu ya upatikanaji wa nishati safi ya kupikia.

“Kuwezesha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia katika ujazo mdogo ili kusaidia wananchi wa kipato cha chini kuweza kumudu gharama,” amesema.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Ashatu Kijaji amesema washiriki walitaka mkutano huo kutoka na azimio la mazingira la Dodoma.

“Na sisi tukasema (Serikali) wanahitaji kuja na azimio la Dodoma ambalo linahusu mazingira yetu, lakini tukakubaliana kama wanasemina wote kuwa mpaka liwe azimio ni lazima lifuate taratibu ndani ya Serikali yetu,” amesema Dk Kijaji.

Amesema ofisi yake italiandaa vizuri azimio hilo na kupeleka serikalini, kabla ya uzinduzi utakaofanyika jijini Dodoma.

Related Posts