Mambo matatu yanayoibeba Simba kwa Al Ahli Tripoli

Dar es Salaam. Timu ya Simba inatarajiwa kushuka uwanjani Jumapili ijayo kwenye mchezo wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika utakaopigwa nchini Libya dhidi ya Al Ahli Tripoli.

Al Ahli inakutana na Simba baada ya kuiondosha Uhamiaji ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 5-1, ambapo mchezo wa kwanza ilishinda mabao 2-0 kabla ya mechi ya pili kupata ushindi wa mabao 3-1 mechi zote zikipigwa Libya.

Simba inaanza kucheza raundi ya kwanza kutokana na kuwa juu kwenye viwango vya soka Afrika ikiwa inashika nafasi ya saba huku Al Ahli Tripoli ikishika nafasi ya 33 Afrika.

Hata hivyo, kuna sababu kadhaa ambazo zinaifanya mechi hiyo kuonekana kuwa upande wa Simba zaidi, kuliko vijana hao wa Libya ambao kwa hivi karibuni hawana rekodi kubwa zaidi kwenye soka Afrika.

Mlinda mlango namba moja wa klabu ya Al Ahli, Mohammad Nashnoush (36) yupo nje ya uwanja akiuguza majeraha ya goti, hivyo atawakosa Simba katika michezo yote miwili. Nashnoush ambaye ni kipa mzoefu sana akiwa amecheza michezo mingi kwenye mashindano ya kimataifa nafasi yake itachukuliwa na kipa namba mbili Suleiman Al Tihar (22), ambaye si mzoefu katika mechi za kimataifa ambapo amecheza mechi mbili tu dhidi ya Uhamiaji ya Zanzibar akiruhusu bao moja.

Simba imefanya usajili wa wachezaji wengi wenye umri chini ya miaka 25, kama Joshua Mutale, Edwin Balua, Valentin Nouma, Jean Ahoua,Steven Mukwala, Valentino Mashaka na Leonel Ateba ambao wanacheza mpira wa kasi kuelekea lango la timu pinzani.

Al Ahli ina wachezaji wengi wenye umri mkubwa ambao wanaweza wasimudu kasi ya wachezaji wa Simba, wakongwe waliopo ni kama Mohammed Al Munir (32), Sanad Al Werfalli (32), Ahmed El Trbi (32), Thierry Manzi (28), Bakhit Khamis (30), Abdullah Al Sharif (28), Mourad Hedhli (33), Ahmed Krawaa (35), Ali Bouargoub (32), Agostinho Mabululu (32) na Abdllah Al Orfey (30), wakati wachezaji wengine wana wastani wa miaka 22-27, huku wanaoanza wengi ni wenye miaka 27-35.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Klabu ya Simba inashika nafasi ya saba ikiwa na alama 39, wakati Al Ahli Tripoli ikiwa nafasi ya 33, hivyo kwenye takwimu za makaratasi Simba inaonekana kuwa na kiwango cha juu zaidi ukilinganisha na wapinzani wanaokwenda kukutana nao.

Simba ambayo inaondoka kesho alfajiri inakwenda kwenye mchezo huu ikiwa imefanya maandalizi mazuri ambapo imecheza michezo miwili ya kirafiki mmoja dhidi ya Al Hilal ya Sudan ikitoa sare ya 1-1, mchezo mwingine dhidi JKT Tanzania ikishinda mabao 2-0.

Simba inatakiwa kuwa makini sana na mshambuliaji wa Tripoli, Agostinho Cristóvão Paciência, maarufu kama Mabululu ambaye amekuwa akiitumikia timu ya Taifa ya Angola kutokana na kiwango cha juu na uzoefu ambao amekuwa nao kwenye michuano ya kimataifa Afrika.

Staa huyo ambaye ameshazichezea timu kadhaa kubwa Afrika kama Al Ittihad ya Misri, Petro de Luanda na Libolo, ameshacheza timu ya Taifa ya Angola michezo 36 na kufunga mabao 12 akiwa kati ya wachezaji waliocheza michezo michache na kufunga mabao mengi kwenye timu hiyo.     

Kocha wa Simba Fadlu Davids, alisema wamejiandaa vizuri kuwakabili Al Ahli Tripoli wakiwa wamekamilisha sehemu kubwa ya maandalizi yao.

“Al Ahli Tripoli ni timu nzuri na imekuwa na historia ya kufanya vizuri kwenye mashindano haya huko nyuma. Hata hivyo, sisi ni timu kubwa naamini tunaweza kufanya mambo makubwa kwenye mchezo huu wa Jumapili ijayo.”

Related Posts