Mwananchi yaeleza manufaa kongamano la ‘Energy Connect’

Dar es Salaam. Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Victor Mushi amesema lengo la kuandaliwa kwa kongamano la ‘Energy Connect’ ni kuwezesha mazungumzo kuhusu matumizi ya nishati safi nchini Tanzania.

Kupitia kampeni isemayo, “ushirikiano wa kibunifu katika nishati safi ya kupikia, endelevu na mustakabali wa kijani,” watu watajifunza jambo kwa undani.

Kongamano hilo linatarajiwa kufanyika Oktoba 16 hadi 18, 2024 jijini Dar es Salaam likiandaliwa na MCL kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wato Huduma za Mafuta na Gesi (Atogs) na Chama cha Waingizaji na Wasambazaji wa Gesi ya Mitungi Tanzania (TZLPGA).

Mushi amesema katika siku hizo tatu suala la uvumbuzi katika eneo la nishati safi ni jambo litakalozingatiwa kutokana na manufaa yake kiafya, kiuchumi na kimazingira.

“Pia ni fursa za kipato, nia yetu ni kuunganisha nguvu kwa pamoja ili kuwezesha mdahalo ngazi ya kitaifa,” amesema Mushi.

Pia, zitaangaziwa changamoto mbalimbali ambazo zimekuwapo katika matumizi ya kuni na mkaa ikiwamo afya, mazingira na uhusiano wa nishati hizo na viashiria vya umasikini.

“Matumizi ya kuni na mkaa pia yananyima wanafunzi fursa ya kusoma kutokana na kutakiwa kwenda kutafuta nishati hiyo kwa ajili ya kupikia. Hivyo ni fursa ya sisi kuangalia namna tunavyoweza kuhama kutoka katika kuni na mkaa,” amesema.

Amesema wadau wa gesi ambao wameshirikiana na Mwananchi wanao uzoefu wa muda mrefu hivyo ni fursa kuona vitu vinavyofanyika kipi kinaweza kuchukuliwa na kukuzwa zaidi ili kuwezesha matumizi ya nishati safi na kupunguza uchafuzi wa mazingira.

Related Posts