Mwanga. Ni pigo kubwa kwa makanisa, ndivyo inavyoweza kusemwa baada ya makanisa mawili, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Kanisa Katoliki, kufiwa na viongozi wao kutokana na ajali za barabarani zilizotokea katika maeneo mawili tofauti wilayani Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro.
Ajali hizo zimeacha pengo na huzuni kwa familia, waumini na jamii kwa ujumla, huku zikikumbusha umuhimu wa madereva kuchukua tahadhari barabarani ili kuepusha maafa zaidi.
Viongozi hao waliokufa katika ajali hizo ni pamoja na Mkuu wa Dayosisi ya Mwanga ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Chediel Sendoro na Padri Nicolaus Ngowi (54) wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu, aliyekuwa akihudumu katika Jimbo Katoliki la Ifakara, Mkoa wa Morogoro.
Inaelezwa kuwa viongozi hao kila mmoja akiwa anaendesha gari lake, walikuwa wakisafiri kwenda maeneo tofauti.
Askofu Sendoro alikuwa akitokea Njia Panda ya Himo akielekea nyumbani kwake Mwanga wakati Padri Ngowi alikuwa akitokea Jimboni kwake Ifakara, akielekea nyumbani kwao Marangu, Mkoani Kilimanjaro kwa shughuli za kifamilia.
Ajali iliyosababisha kifo cha Askofu Sendoro ilitokea katika eneo la Kisangiro, Wilaya ya Mwanga, saa 1:30 usiku, baada ya gari alilokuwa akiendesha aina ya Toyota Prado kugongana uso kwa uso na lori, huku iliyosababisha kifo cha Padri Ngowi ilitokea eneo la Kiruru wilayani Mwanga baada ya kugongana uso kwa uso na basi la Kilenga.
Akizungumzia ajali hizo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema
ajali iliyomuua Padri Ngowi, chanzo kilikuwa uzembe wa dereva wa basi la Kilenga ambaye alilazimisha kulipita gari lililokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari, hivyo kugongana uso kwa uso na gari la padri huyo.
Amesema mwili wa Ngowi umehifadhiwa katika Hospitali ya Kisangara, Mwanga, ukisubiri taratibu za mazishi.
“Hii ajali ya pili iliyosababisha kifo cha Askofu Sendoro, ilitokea majira ya saa 1:30 usiku katika eneo la Kisangiro, Njiapanda ya Himo, baada ya gari alilokuwa akiliendesha kugongana uso kwa uso na lori na ilitokea wakati Askofu Sendoro akijaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake,” amesema Kamanda Maigwa.
Askofu Sendoro ndiye Askofu wa kwanza wa Dayosisi ya Mwanga ambaye aliingizwa kazini Jumapili ya Novemba 6, 2016 baada ya kuzaliwa kwa Dayosisi hiyo mpya iliyotokana na kugawanywa kwa Dayosisi mama ya Pare.
Viongozi mbalimbali wa Kanisa hilo wakiwemo Maaskofu, wameeleza namna walivyopokea msiba huo na kumuelezea Askofu Sendoro enzi za uhai wake.
Mkuu wa KKKT-Dayosisi ya Pare, Askofu Charles Mjema amesema msiba huo umemgusa kwa kipekee kwa kuwa licha ya askofu huyo kuwa mtenda kazi mwenzake, pia alikuwa rafiki yake wa karibu.
“Dayosisi ya Pare ni dayosisi mama iliyozaa dayosisi ya Mwanga, huu ni msiba unaogusa kanisa ni msiba mgumu kwetu na kwa familia, tunashukuru Mungu familia imelipokea, tumeenda kwa baba na mama wakiwa watumishi wa Mungu wanajua maisha yetu yako mikononi mwa Mungu,” amesema na kuongeza;
“Tunawatia moyo watu wote kuwa maisha yetu yako mikononi mwa Mungu, saa ya mtu ikifika imefika hakuna mtu ambaye anaweza kuizuia, kwa hiyo wakati wa maisha ya baba askofu Chediel Sendoro imehitimishwa kwa namna hiyo kwa huzuni kubwa lakini ndiyo hivyo.”
Akizungumza Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Dk Fredrick Shoo amesema kifo hicho kimemshtua.
Ametoa pole kwa familia, Mkuu wa Kanisa na wana KKKT wote kwa msiba huo wa Askofu Sendoro.
“Kifo hiki kimenishtua na kunisikitisha sana, nitoe pole kwa familia, Mkuu wetu wa Kanisa na Wana-KKKT wote, tunalo tumaini la milele katika Kristo,” amesema Dk Shoo.
Kauli ya msaidizi wa askofu
Msaidizi wa Askofu Dayosisi ya Mwanga, Mchungaji Timoth Msangi amesema msiba huo ni pigo kwao kwa kuwa wamempoteza kiongozi shupavu na mashuhuri ambaye alisimama kuijenga Dayosisi hiyo na kuhakikisha kazi ya Mungu inasonga mbele.
“Askofu Sendoro tulianza naye kazi mwaka 2016 na tunaweza kusema sisi ndiyo waanzilishi wa dayosisi hii, tumepita naye katika maeneo mbalimbali na majukumu mbalimbali,” amesema Mchungaji huyo.
Aidha, amesema Askofu Sendoro alikuwa mhubiri Mzuri na walikuwa na mipango mingi kwa ajili ya Dayosisi hiyo, lakini Mungu amempenda iwe hivyo na cha kufanya kwa sasa ni kuendelea kumuombea pumziko la milele lakini pia kuiombea dayosisi isitetereke kutokana na kofo hicho.
Amesema kutokana na Katiba, msaidizi wa Askofu ndiye atakayeendelea na jukumu la kuiongoza dayosisi hiyo mpaka atakapopatikana askofu mwingine.
“Naweza kusema ni jukumu zito sana kwa sababu ni kitu ambacho sikuwa nimekitarajia nahitaji sana nguvu ya Mungu, aniwezeshe pamoja na wanadayosisi tuweze kusonga mbele na kuiwezesha dayosisi hii ambayo Mungu ametupa kusonga mbele,” amesema Mchungaji Msangi.
Akizungumza ratiba ya maziko, Askofu Mjema amesema Sendoro atazikwa Jumanne Septemba 17, 2024 katika Kanisa Kuu Mwanga.
“Tumepanga siku ya Jumanne Septemba 17 itakuwa ni ibada ya maziko ambayo yatafanyika katika Kanisa Kuu Mwanga, kwa sasa tunaendelea na taratibu za maandalizi ya mazishi,” amesema Askofu Mjema.
Akizungumzia hali za majeruhi, Askofu Mjema amesema majeruhi ambaye ni Mtoto wa Sendoro aliyekuwa naye kwenye gari anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) na hali yake inaendelea vizuri.
“Katika ajali hiyo iliyohusisha malori mawili na gari ya baba Sendoro, kulikwa na mtoto wake anayeitwa Eric ambaye alipata majeraha, lakini tunamshukuru Mungu kwamba amepimwa vipimo vyote vinaonyesha yuko vizuri majeraha ni ya juu tu lakini yuko vizuri,” amesema Mjema.
Wakizungumza baadhi ya waumini wa kanisa hilo, wamesema taarifa za kifo cha Askofu Sendoro zimewashtua kwa kuwa alikuwa ni kiongozi aliyekuwa akitegemewa na kanisa na jamii kutokana na misimamo yake ya kiimani.
“Kifo hiki kimetuumiza sana kama waumini wa Kanisa hili, ameacha alama kubwa kwa kanisa kutokana na utumishi wake, tutamkumbuka na kuyaenzi mafundisho yake,” amesema John Msangi.
Madereva wa magari yaliyohusika kwenye ajali wasimulia
Mmoja wa madereva wa lori, Athuman Jumanne amesimulia namna ajali ilivyotokea huku akisema Askofu Sendoro alitaka kuyapita magari mengine yaliyokuwa mbele akajikuta akisababisha ajali iliyochukua uhai wake.
“Nilikuwa natokea Tanga kwenda Arusha, ilipofika saa moja jioni eneo la Kisangiro ghafla tuliona Prado inayapita magari yaliyokuwa mbele, nilijitahidi kumkwepa lakini ikashindikana, alinifuata tukagongana uso kwa uso,” amesimulia dereva huyo.
Amesema baada ya kutokea ajali walikuja wasamaria wema kutoa msaada eneo la tukio na wakati wanaondolewa eneo la tukio aliyekuwa kwenye gari dogo (Askofu Sendoro) alikuwa tayari ameshafariki dunia.
Mark Antony, ambaye ni miongoni mwa madereva waliopata ajali eneo hilo la tukio, amesema muda mfupi baada ya gari lililokuwa likiendeshwa na Askofu Sendoro kuyapita magari mengine, alishuhudia likipinduka baada ya kugongana uso kwa uso na gari lililokuwa likitokea Mwanga kuja njia panda ya Himo.
“Safari yangu ilianzia Mkoa wa Arusha, muda kama saa 1:30 ndio tulikuwa mitaa hii hapa ajali ilipotokea, mimi uelekeo wangu ulikuwa barabara ya Mwanga na mwenzangu akitokea upande wa Mwanga sisi tukawa katikati kupishana, wakati tunapishana kumbe upande wa ubavuni kulikuwa kuna gari dogo ambalo lilikuwa linayapita magari mengine, mbele nikaona gari likigongana na gari jingine mara ghafla gari likapiga chini na sisi tukaangusha magari chini,” amesimulia dereva huyo.
Askofu Sendoro ameacha mjane na watoto wawili.
Akizungumzia tukio la ajali iliyomuua Ngowi, Padri John Matumaini wa Jimbo Katoliki la Moshi amesema alikuwa akitokea Morogoro kwenda nyumbani kwao Marangu, Moshi ambako kulikuwa na shughuli ya kifamilia iliyokuwa ifanyike Septemba leo Jumatano Septema 10, 2024.
Mwananchi pia imezungumza na Mkuu wa Shirika la Damu Takatifu Azizi ya Yesu, Vedasto Ngowi amesema; “Sijajua alikuwa anaelekea katika shughuli gani lakini alikuwa apokewe na ndugu zake njia panda (Himo), hivi sasa tunaelekea nyumbani kwake Marangu,” amesema Ngowi.
Hata hivyo, amesema taratibu zaidi zitajulikana baada ya kuwasiliana na familia yake lakini mazishi yatafanyika Manyoni Jimbo Katoliki la Singida kuliko na eneo la maziko ya mapadri wa shirika hilo.