Rais Samia aomboleza kifo cha Askofu Sendoro

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mwanza, Askofu Chediel Sendoro.

Askofu Sendoro alifikwa na mauti usiku wa jana Jumatatu, Septemba 9, 2024 kwa ajali ya gari iliyotokea eneo la Kisangiro, Wilaya ya Mwanga ambapo gari aina ya Toyota Prado alilokuwa akiendesha kugongana uso kwa uso na lori.

Katika gari hilo, Askofu Sendoro alikuwa na mwanawe ambaye anaendelea na matibabu.

Kutokana na kifo hicho, watu mbalimbali wameanza kutuma salamu za rambirambi akiwemo Rais Samia aliyetuma pole kwa Mkuu wa KKKT, Askofu Alex Malasusa, ndugu, jamaa na marafiki.

Rais Samia ametumia akaunti zake za kijamii akisema:”Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Baba Askofu Chediel Elinaza Sendoro, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mwanga.”

“Natoa pole kwa Mkuu wa KKKT Baba Askofu Dk Alex Gehaz Malasusa, Maaskofu wote, waumini, familia, ndugu, jamaa na marafiki. Nawaombea faraja kwa neno kutoka katika Biblia Takatifu Kitabu cha Waebrania 13:14; “Maana hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao,”amesema.

Related Posts