Sh1.4 bilioni kukuza wajasiriamali wabunifu Tanzania

Dar es Salaam. Vijana na wanawake wabunifu wanatarajiwa kunufaika na Mradi wa Ubunifu wa Funguo, unaotekelezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) ambao umepanga kutoa Sh1.4 bilioni kwa lengo la kuliinua kundi hilo.

Msimamizi wa mradi huo, Joseph Manirakiza amesema hayo leo Jumanne, Septemba 10, 2024 jijini Dar es Salaam mbele ya Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo.

Manirakiza amesema mradi huo kwa kushirikiana na mfuko wa Imbeju wa CRDB Foundation, una lengo la kubadilisha mwenendo wa ufadhili wa wajasiriamali wabunifu.

Amesema ushirikiano wa kimkakati unalenga kutumia ruzuku inayotolewa na Umoja wa Ulaya kwa kampuni changa na kufungua fursa ya kupata mikopo ya riba na masharti nafuu kutoka kwa CRDB Foundation, ili kuongeza uwezo wa kimtaji kuwawezesha wajasiriamali kukua kwa haraka.

“Sh1.4  bilioni inalenga kuwawezesha wanawake walioanzisha biashara zenye ubunifu ndani yake, angalau asilimia 40 ya ufadhili uliopo umetengwa kwa ajili ya biashara zinazomilikiwa na kuongozwa na wanawake, ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 30 ukilinganisha na mwaka jana, ili kutilia mkazo dhamira ya ujumuishi wa kijinsia na kuunga mkono uongozi wa wanawake katika ubunifu,” amesema.

Tangu kuanziswa kwake mwaka 2022 kwa ufadhili kutoka Umoja wa Ulaya kupitia mpango wa BEGIN unaoratibiwa na kitengo cha mazingira ya biashara katika Ofisi ya Rais – Mipango na Uwezeshaji, Funguo imewekeza Sh3.8 bilioni katika kampuni changa 43, ikichangia kutengeneza na kuendeleza takribani ajira 4,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa vijana wa Tanzania.

Naibu Waziri Nyongo amesema mipango ya uwekezaji kwa vijana wa Tanzania ni rasilimali kubwa kwa Taifa, kwa kuwa wamejaa mawazo ya kibunifu na maarifa ya kutengeneza mustakabali ulio bora zaidi kwa Taifa.

“Kwa kuwawezesha na mitaji ya kuanzisha na kuendeleza biashara zao, msaada wa kitaalamu, mafunzo na kadhalika, vijana wetu wanakuwa wamepata zana wanazohitaji kujenga biashara zenye mafanikio na zinazoweza kukua kwa haraka na kuchangia uchumi.

“Hili ni muhimu tunapolenga kukuza sekta binafsi yenye nguvu inayoweza kutengeneza ajira na kuhamasisha ubunifu katika uchumi wetu.

“Ningependa kuwashukuru washirika wetu wa maendeleo, Umoja wa Ulaya, Serikali ya Uingereza na UNDP kwa kuunga mkono miradi ya aina hii,” amesema Nyongo.

Dhamira ya mpango huu ni kuongeza idadi ya kampuni za ubunifu zenye uwezo wa kustawi haraka ili kuharakisha kufikia malengo ya maendeleo endelevu ya Tanzania.

Wafadhili wengine wa mradi ni pamoja na Serikali ya Uingereza kupitia mpango wa Africa Technology and Innovation Partnerships (ATIP) na UNDP katika mkakati wake wa kuwawezesha vijana kiuchumi.

Ufadhili huo unalenga biashara changa bunifu zinazoongozwa na vijana na kumilikiwa kwa wingi na raia wa Tanzania.

Funguo na Imbeju hazitoi tu msaada wa kifedha, bali pia zinawawezesha wajasiriamali vijana, wanawake na makundi maalumu kwa kuwapa zana muhimu za kubadilisha mawazo yao ya biashara kuwa miradi yenye mafanikio na yenye athari kubwa kwa jamii.

Christine Grau, Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, amesisitiza dhamira ya Umoja wa Ulaya katika kukuza mazingira ya biashara yanayochochea ukuaji wa ubunifu nchini Tanzania.

Muyeye Chambwera, Naibu Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, amesema: “UNDP imejitolea kusaidia vijana kutambua uwezo wao na kufungua milango ya upatikanaji wa fedha kupitia miradi yao, tunaamini tunaweza kuleta athari kubwa kupitia ushirikiano huu na CRDB Foundation ambao ni ushahidi wa juhudi nyingi tunazofanya kufungua milango zaidi ya kufanya kazi pamoja na wadau mbalimbali.”

Tully Mwambapa, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Foundation, amesisitiza uwezo wa mabadiliko wa ushirikiano huu kwa biashara za vijana.

“Mpango wa Imbeju umejizatiti kwa dhati kuwawezesha kizazi kijacho cha wajasiriamali wa Kitanzania, kwa kuunganisha ujenzi wa uwezo, elimu ya kifedha na maendeleo ya ujuzi wa ujasiriamali, Imbeju haipatii msaada wa kifedha tu, bali tunatoa mfumo kamili utakaokuza vipaji vya vijana,” amesema Mwambapa.

Richard Craig, Mkuu wa Idara ya Uchumi katika Ubalozi wa Uingereza, amesisitiza dhamira ya Uingereza ya kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa ajili ya kuhakikisha uchumi wa nchi unakua.

“Programu ya Funguo ni sehemu ya ushirikiano mpana wa kiuchumi kati ya Uingereza na Serikali ya Tanzania, kama ilivyoainishwa katika ushirikiano wetu katika Ufanisi wa Pamoja, biashara changa bunifu ni muhimu katika njia ya ukuaji wa uchumi shirikishi,” amesema Richard.

Related Posts