Taifa Stars imeitoa kimasomaso Tanzania baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Guinea katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 iliyochezwa katika Uwanja wa Charles Konan Banny, Yamoussoukro, Ivory Coast.
Guinea walikuwa wa kwanza kupata bao katika 57 kupitia kwa Mohamed Bayo.
Bayo alifunga bao hilo baada ya kuunasa mpira uliochelewa kuokolewa na safu ya ulinzi ya Tanzania baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ alipokuwa akimdhibiti mshambuliaji huyo wa Guinea.
Hata hivyo bao hilo lilidumu kwa dakika nne tu kwani dakika ya 61 Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliisawazishia Taifa Stars kwa shuti kali la mguu wa kulia akimalizia pasi ya Waziri Junior.
Zilikuwa ni juhudi binafsi za Fei Toto kwani alipokea pasi akiwa zaidi ya umbali unaokadiriwa kuzidi mita 24 na kupiga shuti hilo ambalo lilimshinda kipa Ibrahim Kone na kujaa wavuni.
Dakika ya 71, Taifa Stars ilifanya mabadiliko ya kuwatoa Edwin Balua na Waziri Junior na kuwaingiza Himid Mao na Pascal Msindo.
Mabadiliko hayo yaliiongezea nguvu Taifa Stars na kuifanya ipunguze kasi ya mashambulizi ya Guinea huku ikipishana nayo mara kwa mara katika dakika hizo 45 za pili kulinganisha na ilivyokuwa kipindi cha kwanza.
Furaha kwa Watanzania ilipatikana dakika ya 88 baada ya Mudathir Yahya kuifungia bao la pili na la ushindi akimalizia mpira uliotemwa na kipa Konte.
Mpira huo uliotemwa na Konte ulitokana na shuti kali la Fei Toto ambalo lilimshinda Konte na mpira kumkuta Mudathir aliyeukwamisha nyavuni.
Licha ya refa wa akiba kuongeza dakika nane baada ya dakika 90 kumalizika, Taifa Stars ilikuwa imara kulinda mabao yake na hadi filimbi ya mwisho ilipopulizwa, Guinea ililala nyumbani kwa mabao 2-1.
Matokeo hayo ya leo yameifanya Taifa Stars kusogea hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi H ikiwa na pointi nne huku kinara ikiwa ni DR Congo yenye pointi sita.
Taifa Stars itarejea uwanjani Oktoba 6 kwa kukabiliana na DR Congo ugenini na kisha timu hizo zitarudiana Oktoba 14 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.
Timu mbili zitakazomaliza zikiwa juu ya msimamo wa kundi H zitafuzu fainali za Afcon ambazo zitafanyika Morocco mwakani.