Dar es Salaam. Wakati Shirika la Reli Tanzania (TRC) likiomba radhi kufuatia hitilafu ya kiufundi iliyotokea na kusababisha kuchelewa kwa safari treni ya umeme (SGR), abiria wamesimulia hali ilivyokuwa.
Hitilafu hiyo ya kiufundi, ilitokea jana jioni Jumatatu, Septemba 9, 2024, na kusababisha treni ya saa 10 jioni kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro kukwama Ngerengere kwa zaidi ya saa tatu huku abiria waliotakiwa kutoka saa 12 jioni kwenda jijini Dodoma wakikwama stesheni jijini Dar es Salaam.
“Kuchelewa kwa safari hii kulisababishwa na hitilafu za kiufundi. Changamoto ilitatuliwa na huduma za usafirishaji ziliendelea kutolewa. TRC inawashukuru abiria kwa uvumilivu kipindi cha changamoto,” inaeleza taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano TRC, Jamila Mbarouk, aliyoitoa leo Jumanne, Septemba 10, 2024.
Hadi taarifa hiyo inatolewa, tayari Mwananchi ilikuwa imekwisha zungumza na baadhi ya abiria waliokuwa wamekwama Ngerengere wakitokea Dar es Salaam na kueleza hali ilivyokuaw.
Kwa mujibu abiria, treni ilikwama saa 11:40 jioni na hadi saa 2 usiku hawakuwa na matumaini ya kuondoka.
“Sasa hivi ndiyo milango imefunguliwa, hakuna taarifa yoyote tuliyopewa zaidi ya kuambiwa ni hitilafu, haijulikani ni ya nini, tuko hapa tunasubiri,” alisema abiria huyo aliyezungumza na Mwananchi wakiwa Ngerengere walipokwama.
Kufunguliwa kwa milango kunatajwa kuchangiwa na kelele za wasafiri ambao walizidiwa na joto lililowafanya kuwasimamia wahudumu wa treni hiyo kuwataka wafanye mawasiliano na wahusika ili milango ifunguliwe watu wapate hewa.
Kukwama kwa treni hiyo kunatajwa kuwaumiza baadhi ya watu waliokuwa wakitarajia kuunganisha safari kwenda maeneo mbalimbali ya wilaya za Mkoa wa Morogoro na hata jijini Dodoma.
Mbali na wao kukwama Ngerengere, abiria wengine waliotakiwa kusafiri na treni ya saa 12 jioni kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma walikwama stesheni kwa zaidi ya saa tano bila taarifa yoyote.
Mmoja wa abiria aliliambiwa Mwananchi hadi saa tano usiku walikuwa kituoni hapo na hakuna taarifa yoyote iliyotolewa.
“Hatuambiwi kuna shida gani, tupo tu, abiria wengine wameshachoka,” amesema abiria huyo.