WAZIRI DKT. GWAJIMA AKABIDHI MASHINE ZA ZAIDI YA SH. MIL. 500 KWA MABINTI MBEYA, SONGWE

NA MWANDISHI WETU, MBEYA

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amekabidhi mashine na vifaa mbalimbali kwa wanawake na wasichana zaidi ya elfu 40 wa mikoa ya Songwe na Mbeya kwa lengo la kuboresha shughuli za uchumi na kuwaepusha na mazingira hatarishi dhidi ya maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU).

“Waziri Dkt. Gwajima* amekabidhi mashine hizo zenye thamani ya shilingi 500,841,000/= zilizotolewa na Shirika la HJFMRI kupitia mradi wa DREAMS, unaofadhiliwa na mfuko wa Rais wa Marekani PEPFAR, Septemba 10, 2024 mkoani Mbeya.

Akizungumza na viongozi, wananchi na wanufaika wa vifaa hivyo, Waziri Dkt. Gwajima ametoa wito kwa Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa katika mikoa ya Mbeya na Songwe, kuweka nguvu za makusudi kusimamia mradi huo kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii, Maafisa Maendeleo ya Jamii na wataalamu wengine na kuhakikisha mabinti wengi zaidi wanafikiwa.

“Mashine hizi zitaongeza fursa na upatikanaji wa soko la uhakika kwa bidhaa na huduma zitakazotolewa na mabinti zetu hawa. Kilichonifurahisha ni namna ambavyo, mradi huu haulengi tu kuwasaidia mabinti hawa kuondokana na mazingira hatarishi bali utaongeza tija katika mnyororo wa kiuchumi kwa mabinti na wataweza kujipatia kipato, kuendesha maisha yao pamoja na wategemezi wao.” amesema Waziri Dkt. Gwajima.

Ameendelea kuwashukuru Wadau kwa ushirikiano na Serikali katika shughuli za Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii hususan katika afua za uimarishaji wa kiuchumi kwani wanatekeleza maeneo ya Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA II) 2024/25 – 2028/29 uliozinduliwa Mei 2024.

Aidha, “Waziri Dkt. Gwajima* ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kwa kuunga mkono jitihada za Serikali na wadau katika kuhakikisha wananchi wanawezeshwa kiuchumi na kujiepusha na mazingira hatarishi.

Related Posts