Mwanza. Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo amesema baadhi ya taasisi za Serikali zinachangia vijana kukwama kuanzisha biashara, kusajili kampuni na kujiajiri, huku akizitaka ziweke mazingira rafiki na kuondoa vikwazo kwa wafanyabiashara.
Amesema tangu mwaka 2022, wastani wa vijana 47,000 hadi 70,000 huitimu vyuo vikuu na vya kati nchini, lakini wengi wao wanakosa ajira kutokana na Serikali kutokuwa na uwezo wa kuwaajiri.
Amebainisha sekta ya viwanda na biashara ni eneo muhimu katika kutatua tatizo la ajira.
Dk Jafo ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Septemba 10, 2024, wakati akifungua Maonesho ya 19 ya Biashara Afrika Mashariki yanayofanyika katika Uwanja wa Furahisha, jijini Mwanza.
Maonesho hayo yanahudhuriwa na kampuni mbalimbali za ndani na nje ya nchi, wajasiriamali na wadau wa taasisi za umma, yakiwa na lengo la kufungua fursa za bidhaa na kuwapatia washiriki mbinu mpya za biashara na uzalishaji.
“Kazi ya mtaalamu siku hizi si kutafuta kanuni au sheria inayokwamisha, bali kutafuta njia zinazoweza kufungua biashara. Badala ya kuwa vizuizi, watumishi wa Serikali wanapaswa kuwa wawezeshaji ili biashara ziende vizuri,” amesema Dk Jafo.
Waziri huyo ameupongeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) kwa kupunguza muda wa usajili wa kampuni kutoka miezi mitatu hadi siku tatu, huku akitoa wito wa kuanzisha dirisha maalumu kwa wafanyabiashara wadogo wasioweza kukidhi masharti magumu ya usajili ili kuvutia vijana wengi zaidi kujiingiza kwenye biashara.
“Niwapongeze Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) kwa sababu, licha ya kusajili biashara 250,000, tayari mmesajili majina ya biashara zaidi ya 551,000. Hii yote inaongeza vijana kwenye soko la ajira katika sekta binafsi. Msibweteke, bali endeleeni kuongeza juhudi katika kurahisisha mifumo na taratibu za usajili ili wazidi kuongezeka,” amesema Dk Jafo.
Akizungumza kuhusu hali ya usajili wa leseni, Ofisa Biashara kutoka Brela, Sweetness Madata amesema wameendelea kutoa elimu kuhusu usajili na umuhimu wa kurasimisha biashara kwa wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa katika maonesho hayo, huku wakiwasajili papo kwa hapo.
Makamu Rais wa Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), Boniphace Ndengu amesema bado Taifa halijafanikiwa kuunda mazingira rafiki ya ufanyaji biashara.
Ameishauri Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufanya maboresho ya sheria zinazoongeza adhabu na kuweka ugumu unaowakatisha tamaa wafanyabiashara vijana, hivyo kuwafanya wabaki katika sekta isiyo rasmi.
Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara Mkoa wa Mwanza, Gabriel Chacha amesema maonesho hayo yaliyoanzishwa mwaka 2006 yamekuwa na manufaa mbalimbali kwa wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa.