Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo Septemba 10, 2024 ametembelea Chuo cha Ufundi Stadi VETA Kasulu Mkoani Kigoma kuona utekelezaji wa mafunzo ambapo ameridhishwa na maendeleo ya Chuo hicho ambacho mpaka sasa kimepokea wanafunzi zaidi ya 180 wa fani mbalimbali za muda mrefu na mfupi.
Prof. Nombo amepata nafasi ya kuzungumza na walimu na wanafunzi katika Chuo hicho ambapo amewasisitiza kutunza vifaa vilivyonunuliwa kwa gharama kubwa ili viweze kutumika kwa muda mrefu zaidi.
Katika ziara hiyo Mkoani humo, Prof. Nombo amewataka Wathibiti Ubora wa Shule Kigoma DC na Ujiji kufanya tathmini za kina shuleni kwa kuzingatia hali ya utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa na mapendekezo ya utatuzi wa changamoto mbalimbali.
Katibu Mkuu ameambatana na Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Dkt. Fredrick Salukele ambaye pia amewasisitiza Wathibiti Ubora kukagua pia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) eneo la mtaala wa Sekondari na maadili.
Prof. Nombo leo Septemba 11, 2024 anatarajia kushiriki kikao cha Kamati Tendaji ya mradi wa Uwezeshaji Kupitia Ujuzi (ESP) unaotekelezwa Nchini na Jumuiya ya Vyuo na Taasisi za Ufundi Canada (CICan) kinachofanyika katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kasulu (Kasulu FDC).
The post 𝗣𝗥𝗢𝗙. 𝗡𝗢𝗠𝗕𝗢 𝗔𝗦𝗜𝗦𝗜𝗧𝗜𝗭𝗔 𝗨𝗧𝗨𝗡𝗭𝗔𝗝𝗜 𝗪𝗔 𝗩𝗜𝗙𝗔𝗔 𝗩𝗬𝗔 𝗠𝗔𝗙𝗨𝗡𝗭𝗢 𝗩𝗘𝗧𝗔 𝗞𝗔𝗦𝗨𝗟𝗨 appeared first on Mzalendo.