Halmashauri ya Jiji la Arusha imeonyesha nia ya kushirikiana na wadau pamoja na vituo vya kuibua na kulea vipaji vya michezo ili kutoa nafasi kwa vijana kutimiza ndoto na malengo yao.
Hayo yamesemwa na Naibu Meya wa Jiji la Arusha, Abraham Mollel wakati akifungia tamasha la michezo kwa vijana walio chini ya umri wa miaka 21 lililoandaliwa na taasisi ya Compassion ikishirikiana na makanisa ya Kiinjilisti Kanda ya Mlima Kilimanjaro.
Tamasha hilo linafanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Enaboishu kwa kushirikisha timu saba katika soka, riadha, kuogelea, netiboli, muziki, uchoraji na ubunifu kwenye tekinolojia.
Mollel amesema kwa kutambua umuhimu wa michezo katika kuitangaza nchi wataendelea kushirikiana na vituo mbalimbali pamoja na wadau walioonyesha nia thabiti ya kuwekeza katika sekta hiyo kupitia vijana.
“Milango iko wazi kwa wadau ambao wanataka kutimiza ndoto za vijana sisi kama serikali tutatoa sapoti ya taifa ili kuwazalisha mastaa wa baadae,” amesema Mollel.
Ameipongeza pia taasisi ya Compassion kwa kutambua umuhimu wa kuibua vipaji na kuendeleza michezo kupitia makanisa na kuwaomba tamasha ilo kuwa endelevu.
Faraji Mleli ni mratibu wa tamasha ilo anafunguka kuwa zaidi ya wanamichezo 300 wanashiriki ambapo ushindani umekuwa mkubwa kutokana na ubora wa wachezaji.
“Watakaonekana bora ili tamasha wataendelezwa kwa kupelekwa katika taasisi ambazo zinahusiana na michezo yao husika,” amesema Mleli.
Kwa upande wa Zelote Lukumay mwakilishi wa taasisi ya Compassion amesema wanashirikiana na makanisa kuwakomboa vijana ambao wana hali ngumu ya maisha kwenye umaskini kupitia michezo.
“Lengo letu kubwa ni kuibua vipaji vya michezo kwa vijana ili kuweza kumfanya kila mmoja kuweza kutimiza ndoto,” amesema Lukumay.
Tamasha hilo litafikia tamatai Jumamosi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, uliopo jijini Arusha ambapo timu saba zinazoshiriki zinatoka Arusha Mashariki, Arusha Kati, Arusha Magharibi, Kikatiti, Meru, Karansi, Moshi Mwanga, Same, Nyumba ya Mungu, Siha, Hai, Korogwe, Mkata na Handeni.