BASHE: KILIMO NI SAYANSI NA IGUNGA IMEKUWA KINARA CHA UZALISHAJI PAMBA

 

*Serikali haiwezi kuleta dawa feki; Serikali haiwezi kuleta mbegu feki 

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) ameongea na Wakulima wa zao la Pamba katika Wilaya ya Igunga, mkoani Tabora na kusema kuwa kilimo ni sayansi na kinahitaji tija na ubora na hiyo imekuwa dhamira ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa mbegu bure, ruzuku ya mbolea, zana za kilimo na maafisa Ugani kutoa utaalamu kuongeza uzalishaji. 

“Tumeiteua Igunga kuwa Kituo cha Uzalishaji wa Mbegu za Pamba, na zitaleta pampu za maji zaidi ya elfu moja kusaidia Wakulima kulima Kilimo cha umwagiliaji.  Lengo ni Wilaya ya Igunga kuzalisha tani 100,000 ambazo ni kilo milioni mia moja,” amesema Mhe. Waziri Bashe. 

Mhe. Waziri Bashe amekemea siasa inayoingizwa kwenye dhana ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuinua na kuikuza Sekta ya kilimo, hususan kuimarisha uzalishaji na kuleta tija kwa wakulima. “Ifike mahala tuweke pembeni siasa kwenye maisha ya watu.  Kuchezea Sekta ya Kilimo sitoruhusu, kuna uwekezaji mkubwa kwa manufaa mapana ya wakulima,” ameeleza Mhe. Waziri Bashe. 

Uzalishaji wa Pamba nchini ni katika Mikoa 17; Halmashauri 59 na Wilaya 54.  Aidha, asilimia 94 ya Pamba yote ya Mkoa wa Tabora inatoka Wilaya ya Igunga.  Aidha, Wilaya ya Igunga ina vijiji 139 na Maafisa Ugani 31 ambao Mhe. Waziri Bashe amesema wanahitaji kuongezwa ili kuongeza uzalishaji wenye tija kwa wakulima.



Related Posts