Kikosi cha KMC kimeendelea kusalia Dodoma baada ya kukosa sehemu ya malazi mjini Singida ambako itacheza kesho dhidi ya Singida Black Stars mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Kwa mujibu wa ofisa habari wa timu hiyo, Khaleed Chukuchuku, wameshindwa kusafiri leo kwenda Singida kwakuwa timu imekosa mahali pa kufikia.
“Tumeshindwa kufika kituo cha mechi mpaka muda huu kwa sababu Singida hakuna hoteli yenye nafasi, hoteli zote zimejaa, hata chumba kimoja hakuna tumelazimika kulala Dodoma,” amesema.
Aidha, Khaleed ameongeza kuwa timu hiyo itaenda mkoani Singida kesho ambayo ni siku ya mchezo.
“Tutaenda Singida siku ya mchezo ambayo ni kesho,” amesema.
Hiyo inamaanisha kwamba KMC haitafanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja wa mechi (CCM Liti) na italazimika kutembea umbali wa KM 245 kufika Singida kwaajili ya mechi hiyo inayotarajiwa kuchezwa kuanzia saa 10:00 jioni