‘Gari la Serikali likikugonga unalipwa fidia’

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini Tanzania limebainisha changamoto kubwa inayowakumba wananchi kwa kutokujua haki zao wanapopata ajali zinazohusisha magari ya Serikali.

Licha ya magari hayo kutokuwa na bima, limesema fidia hutolewa kwa waathirika wa ajali hizo.

Hayo yameelezwa leo, Jumatano, Septemba 11, 2024 na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Deus Sokoni, ambaye ni wakili wa Kikosi cha Usalama Barabarani, wakati wa kutambulisha kongamano la pili la afya ya utengamao, litakalofanyika jijini Dar es Salaam kati ya Septemba 18-20, 2024.

 Kongamano hilo limeandaliwa na Asasi ya Rehab Health kwa kushirikiana na Wizara ya Afya.

Afya ya utengamao ni mkakati muhimu unaotoa msaada kwa wagonjwa, wakiwemo waliopata ajali, kupitia huduma za urekebishaji wa viungo, matibabu, na msaada wa kisaikolojia ili kuwarejeshea furaha yao.

Sokoni amesema wananchi wengi hawafahamu haki zao wanapopata ajali zinazosababishwa na magari ya Serikali, na hivyo kukosa fidia wanayoistahili.

“Tunahitaji kushirikiana ili kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ajali za barabarani na utaratibu wa kupata haki zao. Ni kweli magari ya Serikali hayana bima, lakini kuna mfumo wa fidia ambao unamwezesha mtu kupata haki yake endapo ataathirika kwenye ajali,” amesema Sokoni.

Kwa mujibu wa takwimu za Kikosi cha Usalama Barabarani, ajali 10,174 zilirekodiwa kati ya 2019 na 2023, ikiwa ni wastani wa ajali 2,035 kwa mwaka.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa zaidi ya nusu ya ajali hizo (asilimia 53) zilisababisha vifo vya angalau mtu mmoja, huku angalau mtu mmoja akijeruhiwa katika kila ajali.

Katika kipindi cha miaka mitano, Watanzania wanne hadi watano walifariki dunia kila siku kutokana na ajali za barabarani, huku wengine saba hadi wanane wakijeruhiwa kila siku.

Kuhusu kongamano hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Rehab Health, Remla Shirima, amesema litawakutanisha wataalamu wa afya, watoa huduma, watunga sera, na washirika wengine.

Ajenda kuu itakuwa kujadili mikakati ya kuendeleza na kuimarisha huduma za afya ya utengamao hadi kufikia ngazi za msingi.

Kongamano hilo litafunguliwa na Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, likiwa na kaulimbiu ya “Kuendeleza Ajenda ya Utengamao na Kuimarisha Mifumo ya Afya Nchini.”

Mkurugenzi wa Tiba, Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea, amesema huduma za afya ya utengamao ni sehemu muhimu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha mifumo ya afya, ikiwemo kusaidia watu wenye majeraha au maradhi ya muda mrefu kurejea katika hali ya kawaida na kurejesha furaha yao.

“Serikali imeweka msukumo wa kuhakikisha huduma hizi zinaboreshwa na kuifikia jamii nzima, hususan katika maeneo ya vijijini,” amesema Dk Nyembea.

Related Posts