Hii Taifa Stars usiikatie tamaa

GHAFLA Taifa Stars imepindua meza kibabe na kurudi njia kuu kwenye matumaini ya kufuzu ushiriki wa Fainali za Mataifa Afrika, baada ya kuichapa Guinea kwa mabao 2-1 tena ikiwa ugenini.

Mchezo huo wa Kundi H ulipigwa huko Ivory Coast, kulikochaguliwa na Guinea kuwa uwanja wa nyumbani, huku ikitoka kupoteza mbele ya DR Congo wakati Tanzania ikilazimishwa suluhu nyumbani na Ethiopia.

Tofauti na matokeo ya mechi ya kwanza, Stars ilifanya kweli na kuibuka na ushindi huo ulioifanya ifikishe pointi nne nyuma ya DR Congo inayoongoza kwa pointi sita na itakaokutana nao katika mechi mbili zijazo za michuano hiyo mwezi ujao kusaka tiketi ya Afcon 2025 zitafazofanyikia Morocco.

Guinea imesalia mkiani ikiwa haina pointi hata moja, nyuma ya Ethiopia iliyokusanya alama moja kundini na mechi za Oktoba timu hizo zitakutana zenyewe kwa zenyewe kama ilivyo kwa Tanzania na DR Congo.

Licha ya Stars kushinda dhidi ya Guinea lakini bado timu hiyo haikuwa na dakika 45 bora za kwanza ambapo ilishindwa kuwa na mbinu za kufanya kitu kikubwa kwenda langoni kwa wapinzani.

Stars ilimaliza dakika 45 za kwanza ikiwa imepiga mashuti mawili pekee ambayo hata hivyo yote hayakulenga lango wakati wenzao wakiwa na mashuti manne huku moja likiwa limelenga lango.

Stars pia ilikuwa chini kwenye umiliki wa mpira ikimiliki mpira kwa asilimia 41.7 wakati wenyeji wakionyesha kutulia kupanga mashambulizi kwa asilimia 58.3.

SAFU YA USHAMBULIAJI BADO

Kocha Hemed Morocco lazima akae chini kukuna kichwa kuhakikisha anafanya kitu ili kurudisha ufanisi wa safu yake ya ushambuliaji ambayo imeonekana kukosa makali ya kufanya jambo la kuipa mabao timu yake.

Athari chanya kwa washambuliaji wa Stars zipo lakini sio kubwa ambazo zinaweza kuifanya timu hiyo kuwa salama kwa kutengeneza ushindi hasa kwenye mechi tatu zilizosalia.

Mabadiliko ambayo Morocco aliyafanya kwenye safu ya kiungo ya timu hiyo yalionyesha uhai kwa Stars na kuonyesha inazuia vizuri na hata kushambulia tofauti na mechi ya kwanza dhidi ya Ethiopia.

Ubora zaidi wa safu hiyo ni kwamba mabao hayo mawili ya Stars yalitokana na viungo wake wawili Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Mudathir Yahya.

Matokeo hayo ya Stars yamerudisha matumaini upya lakini sasa itatakiwa kuvuna pointi angalau sita ndani ya mechi tatu zilizosalia itakapozifuata ugenini Ethiopia, DR Congo na ile ya nyumbani dhidi ya Guinea ili ipate tiketi ya kwenda Morocco.

Hamasa kubwa kwa Stars kuanzia ushindi wa juzi ndani yake una ahadi ya mamilioni ya fedha walizoahidiwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan ambaye amewaahidi wachezaji wa timu hiyo kiasi cha Sh500 milioni kama watakata tieti hiyo ya kwenda Morocco 2025.

Kocha Morocco akizungumzia matokeo hayo alisema umetokana na wachezaji wake kujiuliza na kuamua kutafuta ushindi muhimu kwa ajili ya Taifa lao.

Morocco alisema matokeo hayo yataifanya Stars sasa kuwa na hesabu mpya mbele ya mechi tatu walizobakiza ambazo wataendelea kuimarika kwa kwenda kuyafanyia kazi makosa waliyoyabaini.

“Haikuwa mechi rahisi kwani tulitoka kupata sare ambayo ilitushtua nyumbani lakini tulitulia na kujiuliza tunakosea wapi na tukafanya mabadiliko machache,” alisema Morocco, ambaye alikosolewa sana kwa kujaza wachezaji wanane wa asili ya kujilinda katika kikosi kilichoanza cha mechi ya nyumbani dhidi ya Ethiopia iliyomalizika kwa 0-0.

“Bado tuna nafasi ya kufanya vizuri zaidi lakini kwasasa tunatakiwa kukaa chini na kufanya maboresho kwenye makosa tuliyoyabaini kabla ya kwenda kwenye mechi tatu zinazofuata.

“Bado hatuwezi kutumia nafasi tunazotengeneza kwa kiwango cha kutosha, kuna maboresho tunatakiwa kuyafanya tunapokwenda katika eneo la mwisho la wapinzani.”

Related Posts