Zilikuwa ni dakika 90 za moto wakati Makamu wa Rais wa Marekani na mgombea urais kupitia Democrats, Kamala Harris alipochuana na mpinzani wake, Donald Trump wa chama cha Republican.
Ulikuwa ni mdahalo wa kwanza kati ya mahasimu hao uliofanyika Jumanne usiku Philadelphia nchini Marekani.
Mada muhimu zilizojadiliwa katika mdahalo huo zilihusu uchumi, uhamiaji, afya na utoaji mimba.
Katika mdahalo huo, mara kwa mara Harris alimchanganya rais huyo wa zamani kwa mashambulizi binafsi, yaliyomtoa kwenye mwelekeo na kuongeza joto kwenye shindano hilo.
Mashambulizi yake ya moja kwa moja kuhusu ukubwa wa mikutano ya hadhara ya Trump, tabia yake wakati wa ghasia za Capitol na maofisa waliohudumu kwenye serikali yake, ambao sasa wamekuwa wakosoaji wakubwa wa kampeni yake, mara kwa mara yalimwacha Trump akiwa hana cha kujibu.
Mfumo wa mdahalo huu mkubwa ulikuwa Harris kumlazimisha mpinzani wake Trump kujitetea kwa muda mrefu kuhusu matendo na kauli zake za zamani.
Harris aliponda mahudhurio ya Wamarekani katika mikutano ya Trump alipokuwa akijibu swali kuhusu uhamiaji.
“Watu huanza kuondoka mapema kwenye mikutano hiyo kwa uchovu na kuchoka,” alisema.
Kauli hiyo ilimchanganya wazi Rais huyo wa zamani, kwani alitumia muda mwingi wa jibu lake juu ya mada ambayo ingeweza kuwa eneo lake la nguvu, akitetea kuhusu ukubwa wa mikutano yake na kudharau mikutano ya Harris.
Trump alitumia muda wake mwingi kuzungumzia masuala ya uhamiaji akisisitiza kukaza zaidi udhibiti.
Katika hilo alijikita kwenye ripoti iliyokanushwa, kwamba wahamiaji wa Haiti katika mji wa Springfield, Ohio, walikuwa wanateka nyara na kula wanyama wa majirani zao.
Wakati maoni ya wananchi wa Wamarekani yakionyesha wengi hawaridhiki na jinsi utawala wa Joe Biden ulivyoshughulikia mfumuko wa bei na uchumi, Harris amebadilisha mada hiyo kwa kupeleka mashambulizi kwa Trump kuhusu ajenda yake ya ushuru wa asilimia sawa kwa kila kitu, ambao aliuita “ushuru wa mauzo wa Trump.”
Pia amekosoa Mradi wa 2025 (Project 2025), aliosema ni wa kihafidhina wa kujitegemea kwa ajili ya utawala wa Republican wa baadaye.
Kama alivyofanya hapo awali, Trump alijitenga na mradi huo na kutetea mpango wake wa ushuru, akibainisha kuwa utawala wa Biden uliendelea na ushuru mwingi katika urais wake wa kwanza.
Kuhusu utoaji mimba, Trump alitetea jinsi alivyoshughulikia suala hilo, akisema kuwa Wamarekani kote walitaka ulinzi wa hukumu ya Mahakama maarufu kwa jina la Roe v Wade, inayoruhusu utoaji wa mimba ubatilishwe na Mahakama ya Juu – kauli ambayo uchunguzi wa maoni hauungi mkono.
Alijitahidi kufanya msimamo wake uwe wazi na wakati mwingine jibu lake lilikuwa la kupindapinda.
Wakati huohuo, Harris alitumia fursa hiyo kutoa ombi la kibinafsi kwa familia ambazo zimekumbwa na matatizo makubwa ya ujauzito na kushindwa kupata huduma za utoaji mimba katika majimbo ambayo yamepiga marufuku utaratibu huo, maarufu kwa jina la “marufuku ya utoaji mimba ya Trump,” akisema “Ni tusi kwa wanawake wa Marekani.”
Katika hitimisho lao, Harris alisema anazingatia mustakabali wa nchi hiyo, huku Trump alijibu kwa kuuita mpango huo kuwa ni “Marekani taifa linaloshindwa.”
Pia Trump alijaribu kumfananisha Harris na Rais Joe Biden akionyesha kuwa wote ni wanasiasa aina sawa.
Harris alijibu kwa kwa kuhoji kama Trump anastahili wadhifa huo, huku akimwita “fedheha.”
Aidha, Kamala alionekana akimdhihaki Trump na kuna wakati alionekana akijizuia kucheka wakati Trump akizungumza.
Akitumia mbinu zinazofanana na za Trump, Harris alimwita mgombea wa Republican “mnyonge.” Aliyageuza mashtaka ya Trump kwamba ulimwengu ungecheka uongozi wa Marekani.
Trump alimwonyesha Harris kama mwanasiasa wa mrengo wa kushoto kupita kiasi, akipotosha rekodi yake. Katika majibu yake, rais wa zamani alimwita Harris “mkomunisti.”
“Anapanga kunyang’anya bunduki za kila mtu,” Trump alisema, akiongeza chumvi.
Harris alijibu kwa kusema kwamba yeye na mgombea mwenza wake, Tim Walz, kwa kweli ni wamiliki wa bunduki.
Kwa ujumla, majibu ya Harris yalikuwa ya kueleweka na yenye mwelekeo zaidi kuliko ya Trump, lakini bado haijulikani kama utendaji wake kwenye mdahalo utakuwa na athari kwenye kinyang’anyiro cha urais.
Hata wachambuzi kwenye vituo vya kihafidhina kama Fox News walikubali kwamba Harris alionekana kumchanganya Trump.
Kama hiyo haitoshi, katika dakika chache baada ya mdahalo, mwanamuziki maarufu Taylor Swift alitangaza kumuunga mkono Harris.
Kwa upande wake Trump, ilielezwa alikuwa na majibu yasiyo na mwelekeo, akirudia mara kwa mara kuzungumzia uhamiaji
Hotuba ya Trump wakati wa mdahalo iliruka-ruka kwenye mada mbalimbali, mara chache akibaki kwenye masuala yaliyoulizwa na waandaaji.
Kwa wakati mmoja, Trump angekuwa akizungumza kuhusu uchumi, kisha kwa ghafla, akazungumzia mabomba ya mafuta.
Katika pumzi moja, angeongelea huduma za afya, na katika pumzi inayofuata, alirudi kwenye uhamiaji. Kisha akabadilisha mada tena, halafu akarudi kwenye uhamiaji.
Trump alishindwa kudhibiti ujumbe wake wakati wa mdahalo mzima. Majibu yake hayakuwa na umakini na alionekana kuwa na nia zaidi ya kumshambulia Harris kuliko kuzingatia hoja za sera.
Hata hivyo, Trump amekuwa akijulikana kwa mtindo wake wa kuzungumza bila mpangilio, hivyo haijulikani kama wapiga kura watamuona vibaya zaidi baada ya utendaji wake wa mdahalo wa Jumanne.
Baadaye Trump alijitokeza kwenye chumba cha waandishi wa habari akidai ushindi, huku kambi ya Harris, ikifurahia pia utendaji wake, ikitaka mdahalo wa pili.
Gavana wa California Gavin Newsom alisema baadaye kwamba Trump alilazimika kujitetea “akizungumzia mbwa na ukubwa wa mikutano.”
Imeandaliwa na Elias Msuya kwa msaada wa BBC, Aljazeera