KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA UTEKELEZAJI WA MRADI WA SEQUIP-AEP


Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Michael Ng’umbi akitoa maelezo ya utekelezaji wa Mradi wa kuimarisha ubora wa elimu ya Sekondari kwa njia mbadala (SEQUIP-AEP) Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo ilipofanya ziara katika kituo cha Taasisi hiyo mjini Kibaha, Pwani leo Septemba 11, 2024.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mhe. Husna Juma Sekiboko (mwenye ushungi) akiongozana na Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Michael Ng’umbi (mwenye suti), pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Nickson Simon (wa kwanza kulia) na wajumbe wa kamati wakiondoka katika kituo cha TEWW mara baada ya kukagua kituo hicho kilichopo mjini Kibaha, Pwani leo Septemba 11, 2024.

Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Michael Ng’umbi, akijibu hoja za wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo wakati wa kikao cha majumuisho kilichofanyika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, leo Septemba 11, 2024.

Na Mwandishi Wetu

Kamati ya Kudumu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Elimu, Utamaduni na Michezo imeridhishwa na kupongeza juhudi za Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) katika kutekeleza mradi wa kuimarisha elimu ya Sekondari kwa njia mbadala (SEQUIP-AEP).

Hayo yamebainishwa leo Septemba 11, 2024 kamati hiyo ilipofanya ziara kwenye kituo cha Taasisi hiyo kilichopo mjini Kibaha, Pwani kukagua utekelezaji wa Mradi wa SEQUIP-AEP.

Pamoja na mambo mengine, kamati hiyo imebaini kuwa ujenzi wa majengo ya kituo cha kutolea elimu cha taasisi hiyo umezingatia ubora na thamani ya fedha zilizotolewa, na kwamba kituo hicho kitatoa fursa kwa wananchi wengi kupata elimu.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Husna Sekiboko amesema kwa muda mrefu kumekuwa na changamoto na utofauti mkubwa wa miradi ambayo inatekelezwa na Taasisi ambazo zipo chini ya Wizara pamoja na miradi ambayo inatekelezwa na Serikali za Mitaa.

“Kupitia ziara hii katika kituo cha TEWW – Pwani, Bunge linatoa agizo kwa Wizara ya Elimu kushirikiana na kubadilishana uzoefu na TAMISEMI ili miradi inayotekelezwa wilayani iwe na ubora na thamani sawasawa na ile ambayo inatekelezwa na Taasisi za Serikali kwa sababu miradi yote hiyo inatumia fedha za Serikali,’ amesema Mhe. Sekiboko.

Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Prof. Michael Ng’umbi amesema kuwa nje ya ujenzi na ukarabati wa vituo, taasisi yake imedurusu moduli na kuandaa miongozo; imefanya uhamasishaji wa programu, imesimamia ufundishaji na ujifunzaji vituoni; pamoja na kufanya ufuatiliaji na tathmini.

Pia, Kiongozi huyo ameiambia Kamati ya Bunge kuwa katika kipindi cha 2021 – 2024 Taasisi yake imetumia kiasi cha Tsh. 2,976,637,185 kujenga vituo vipya vya kutolea elimu katika Mikoa 11 ya Tanzania Bara na kufanya ukarabati uliogharimu kiasi cha Tsh. 1,036,640,255 wa vituo vilivyokuwepo katika mikoa minane (8).

Related Posts