Dar es Salaam. Waziri wa Maji nchini Tanzania, Jumaa Aweso amesema uwepo wa kiwanda cha mabomba ya maji mkoani Simiyu, kutarahisisha utekelezaji wa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda mikoa mbalimbali nchini na kuzalisha ajira kwenye eneo hilo.
Aweso ameyasema hayo mkoani Simiyu, katika ziara yake ambapo pamoja na mambo mengine ametembelea kiwanda hicho kilichopo wilayani Bariadi.
“Uwepo wa kiwanda hiki, utasaidia utekelezaji wa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria. Katika mradi huo, yatatumika mabomba haya, hivyo mwekezaji ametumia fursa kwa wakati sahihi,” amesema.
Kabla ya kiwanda hicho kujengwa, Serikali ilikuwa inafuata mabomba ya maji Dar es Salaam kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya mkoa huo na mikoa jirani.
Sambamba na hilo, ameeleza kufurahishwa na hatua ya kujenga kiwanda hicho katika Mkoa wa Simiyu, kwa kuwa imezoeleka wengi wangekimbilia kuwekeza Dar es Salaam.
Mbali na kusaidia upatikanaji wa vifaa vya utekelezaji wa miradi ya maji, Aweso amesema uwepo wa kiwanda hicho utaibua fursa za ajira kwa vijana wa mkoa huo.
“Angeweza kujenga kiwanda hiki jijini Dar es Salaam ama kwingine, lakini kaamua kuwa mzalendo kwa kukumbuka nyumbani kwanza, hivyo ajira zitamwagika kwa wingi kwa kuwa ni kiwanda cha kisasa,” ameeleza.
Fursa hizo za ajira, kwa mujibu wa waziri, zitakuza maendeleo ya wananchi na jamii kwa ujumla, akisisitiza uwekezaji huo ni matokeo ya kuboreshwa kwa mazingira ya biashara kunakofanywa na Serikali.
“Rais wetu ameweka wepesi wa wawekezaji kufanya kazi kwa moyo na kujituma kwa bidii,” amesema.
Mwekezaji wa kiwanda, Emmanuel Silanga amesema uwekezaji huo umetokana na mazingira mazuri ya biashara nchini.
Silanga amesema kutokana na mazingira hayo wawekezaji wakiwemo wazawa wanapata moyo na nguvu ya kuwekeza zaidi.