Maboresho yaliyofanyika katika taasisi za umma yameleta mafanikio katika sekta ya biashara

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Seleman Jafo, ameeleza kwamba maboresho yaliyofanyika katika taasisi za umma yameleta mafanikio makubwa, hususan katika sekta ya biashara na usajili wa kampuni.

“hadi kufikia Septemba 10, 2024, zaidi ya biashara 250,000 zimesajiliwa nchini, jambo linaloashiria kuimarika kwa mazingira ya biashara”Waziri Jafo,

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 19 ya Biashara ya Afrika Mashariki yaliyofanyika katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza, Dk. Jafo alisema kuwa maonesho haya ni muhimu kwa kuonyesha maendeleo ya sekta ya biashara na kuwapa wafanyabiashara fursa ya kujitangaza na kubadilishana uzoefu na wenzao kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, Ofisa Biashara kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), Sweetness Madata, alibainisha kuwa maboresho yaliyofanywa na Brela yamerahisisha usajili wa biashara, na katika maonesho hayo, huduma ya usajili inatolewa papo hapo. Hii imekuwa msaada mkubwa kwa wafanyabiashara, hasa wale wanaotaka kuingia rasmi katika soko la biashara.

Msaidizi wa Usajili wa Brela, Selemani Selemani, alisisitiza umuhimu wa wafanyabiashara kujisajili na Brela ili waweze kufaidika na fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali. Alisema kuwa usajili ni hatua muhimu kwa biashara yoyote inayotaka kuimarika na kupata faida zaidi, hususan katika mazingira ya sasa ambapo ushindani kwenye soko ni mkubwa.

  

Related Posts