MASHINDANO ya gofu ya wazi kwa wanawake yanaanza kesho katika viwanja vya gofu vya Arusha Gymkhana, huku Tanzania ikiwa na mtihani wa kuthibitisha ubora nyumbani baada ya kufanya vizuri viwanja vya ugenini.
Madina Iddi ambaye ni bingwa wa mataji matatu Zambia na Uganda, amesema wako imara kwa mashindano hayo ambayo pia yataiwezesha Tanzania kupata kikosi bora cha michuano ya gofu ya Afrika nchini Morocco mwishoni mwa mwaka.
Kwa mujibu wa katibu wa mashindano kutoka Chama cha Gofu ya Wanawake Tanzania (TLGU), Rehema Athumani ni wachezaji saba wa kigeni ndiyo wanashiriki mashindano ya mwaka huu.
Madina ambaye ana uzefu mkubwa na mashindano ya kimataifa, anaamini Watanzania watafanya vizuri baada kujifua ipasavyo kupitia mashindano ya wazi ya Zambia, Kenya na Uganda
“Tumetengeneza vipaji bora kwa kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa nafikiri tutakuwa na timu bora katika michuano ya Afrika nchini Morocco,” alisema Madina ambaye ni mwanachama wa Arusha Gymkhana.
Mashindano ya wazi yanatarajiwa kupigwa kesho asubuhi kwa mashimo 18 kabla ya kuendelea Jumamosi ambapo 18 ya pili yatachezwa na kufanya jumla kuwa mashimo 36. Mchezo huu wa mashimo 54 utafikia tamati Jumapili ambapo mashimo 18 ya mwisho yataamua nani bora katika gofu mwaka huu.
Wachezaji 40 wakiwemo saba kutoka nje ya Tanzania wapo Arusha tayari kwa ajili ya mashindano hayo.
Wachezaji nyota wa Tanzania, akiwemo Madina Iddi aliyeshinda mataji mawili nchini Uganda na moja nchini Zambia, Hawa Wanyeche aliyemaliza nafasi ya pili nchini Uganda na Neema Olomi aliyefanya vizuri nchini Kenya na Uganda, wanategemewa kuonyesha kiwango bora zaidi katika mashindano haya.