LICHA ya kutopata ushindi kwenye mechi tano na kufunga mabao mawili pekee, Nahodha wa Pamba Jiji, Christopher Oruchumu amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo akisisitiza ni kipindi cha mpito na kwamba itaanza kufanya vizuri kuanzia mchezo ujao dhidi ya Azam FC.
Mechi tano za Pamba Jiji tangu Agosti, mwaka huu, chini ya Kocha Goran Kopunovic imefungwa mabao 2-1 na Geita Gold, suluhu dhidi ya Biashara United, Tanzania Prisons na Dodoma Jiji na sare dhidi ya Vital’O ya Burundi. Keshokutwa itakuwa ugenini kuivaa Azam FC kuanzia saa 1:00 usiku Chamazi, Dar es Salaam.
Oruchum, raia wa Kenya aliyewahi kuzitumikia Namungo, Tusker na FC Leopald, alisema tayari kikosi chao chini ya Kopunovic kimetumia vyema mapumziko ya wiki mbili kufanya masahihisho na wako tayari kupambana na kuvuna pointi tatu ugenini mbele ya Azam FC.
“Sisi hatuna presha tunawaambia wana Mwanza tunajua matarajio yao ni makubwa wasife moyo, hivi karibuni mambo yatakaa sawa matokeo mazuri yataanza kutiririka, ni mpito tu kuna wakati mambo hayaendi hata kama unatia bidii na timu siyo mbovu,” alisema Oruchum na kuongeza:
“Wakati sahihi tu mambo yatakaa sawa lakini siyo jambo la kutia mtu hofu. Tunawaheshimu Azam kama wapinzani wetu wengine, tunakwenda kupambana kupata ushindi ili tuanze ligi vizuri, tunaahidi kupambana kwa kila namna kuwapa furaha mashabiki wetu.”€
Nahodha huyo alisema mechi za kirafiki dhidi ya Geita Gold (1-2) na Biashara United (0-0) zimewasaidia kuondoa upungufu na benchi la ufundi limeona maeneo yenye changamoto, hivyo wana matumaini ya kuanza vizuri Ligi Kuu na kuwapa furaha na matumaini mashabiki wao.
“Hatuna changamoto kubwa labda kwenye ufungaji ama kiungo bali ni mambo tu hayajakaa sawa kwa hiyo tuna tumaini kwamba kuelekea mechi ya Azam tutakuwa tumeimarika zaidi kushinda zile mechi za awali,” alisema Oruchum.
Pamba Jiji ambayo imepanda daraja msimu huu baada ya kupita takribani miaka 22, imeanza ligi bila ya kupata ushindi wala kufunga bao ikishuka dimbani mara mbili huku pia haijaruhusu nyavu zake kutikiswa.
Katika msimamo wa Ligi Kuu, Pamba Jiji inashika nafasi ya 7 ikiwa na pointi mbili baada ya mechi mbili wakati Azam ni ya 11 ikishuka dimbani mara moja na kupata pointi moja.